Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi na viongozi wa Wilaya ya Manyoni kutatua mara moja mgogoro wa ardhi wa eneo la Majengo lililopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni ambao umesababishwa na Idara ya Ardhi ya halmashauri hiyo.
Mhe. Rais Magufuli ametoa agizo hilo leo tarehe 31 Januari, 2021 aliposimama kuwasalimu wananchi wa Manyoni wakati akiwa safarini kutoka Tabora kwenda Dodoma.
Baada ya kuwasalimu na kuwashukuru kwa kumpigia kura nyingi zilizomwezesha kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kipindi cha pili, Mhe. Rais Magufuli amesikiliza kero ya ardhi inayowakabili wananchi hao ambapo wamelalamikia kitendo cha Idara ya Ardhi kuchukua maeneo yao bila kuwalipa fidia na wengine kuamriwa kuondoka katika eneo hilo baada ya kupewa nyaraka za kupatiwa radhi (Offer) hali iliyozua mgogoro kati ya wamiliki wa asili wa eneo hilo na Idara ya Ardhi.
Mhe. Rais Magufuli ameagiza wananchi wenye Offer waruhusiwe kuendeleza maeneo waliyopatiwa, na wamiliki wa asili wa eneo hilo kulipwa fidia kwa mujibu wa sheria.
Ameagiza eneo lililokuwa mali ya Mama mmoja aitwaye Elizabeth Msalali (90) ambalo lilichukuliwa na Afisa Ardhi mmoja aitwaye Msafiri na kisha kupangishwa kwa kampuni ya simu za mkononi ambayo imeweka mnara wa mawasiliano, lirejeshwe mara moja kwa Mama huyo ambaye ndiye ataingia mkataba wa upangaji na kampuni hiyo.
Mhe. Rais Magufuli ameeleza kutofurahishwa na uelewa mdogo wa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya hiyo Mhe. Jumanne Mlagaza kuhusu masuala mbalimbali ya halmashauri ikiwemo masuala ya kibajeti, miradi na kero za wananchi, na amewataka Madiwani kote nchini kuwa makini na kufuatilia kwa ukaribu masuala yahusuyo halmashauri zao badala ya kuwaachia watendaji wafanye wanavyotaka.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasilino ya Rais, IKULU
Dodoma
31 Januari, 2021
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...