WITO umetolewa kwa serikali kutazama  upya juu ya gharama kubwa za usajili wa dawa asili.

 Hayo yamesemwa  mjini Morogoro jana na Katibu wa Shirikisho la Vyama vya tiba asili nchini, Othaman  Shem, wakati wa maonesho ya  mimea dawa kwa wadau wa tiba asili yaliyoandaliwa na Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo.

 Akizungumza na waandishi wa habari kwenye  maonesho hayo, Shem alisema kuwa gharama kubwa za usajili wa dawa za asili imekuwa ni kikwazo kwa wataalamu wa tiba asili kuweza kuingiza dawa hizo kwenye soko la ndani na nje ya nchi.

“ Tiba asili zina umuhimu mkubwa na zinafanya kazi nzuri ya kutibu sawasawa na hata kuzidi tiba za kisasa. Kikwazo kikubwa kwa tiba asili kusambaa kwa wingi nchini ni gharama kubwa za  usajiri wa dawa hizo ili ziweze kukubalika kwa matumizi na kuingia sokoni.” Alisema Shem.

 Shem alisema kuwa kusajili  aina moja ya dawa ya asili ili iweze kukubalika kisheria ni Shilingi 1.5 Milioni, kiasi ambacho amekitaja kuwa ni kikubwa mno kwa wataalamu wa tiba asili kuweza kumudu.

“ Ni vema serikali ikatazama upya  sheria, vigezo na gharama za usajili wa dawa za asali. Tunao wataalamu wengi wa tiba asili ambao dawa zao zina uwezo mkubwa wa kutibu magonjwa mbali mbali lakini wanakwazwa na gharama kubwa , sheria na mlolongo mrefu wa usajili.” Alisema.

  Shem alitolea mfano wa sheria namba 23 ya tiba asili ya mwaka 2002, iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2017 kuwa sio rafiki kwa wataalamu wa tiba asili kwa kuwa pamoja na vipengele vingine ambavyo sio rafiki ina kipengele kinachozuia kutangaza tiba asili jambo ambalo amelilalmikia.

 Katika hatua nyingine Shem ameishauri serikali kufanyia mrekebisho muundo wa baraza  la tiba asili kwa kuwaondoa  wote ambao sio wataalamu wa tiba hizo.

“ Baraza la tiba asili linaundwa na Madaktari wa tiba za kisasa, hii sio sahihi kabisa, tunatoa wito kwa serikali kufanya marekebisho wa muundo wa baraza hilo ili liundwe na wataalamu wa tiba asili..” Alisema Shem.

 Naye Kaimu Naibu Makamu Mkuu wa Chuo   Kikuu cha Sokoine cha Kilimo, anayeshughulikia taaluma, Profesa Samwel Kabote, akizungumza kwenye maonesho hayo aliwashauri wataalamu wa tiba asili na wadau wote nchini kuanzisha vitalu na kupanda mimea tiba ili kuepuka na uharibifu wa mazingira kwa kuvuna mimea hiyo kwenye misitu  ya asili au misitu ya hifadhi.

 “ Kadri miaka inavyokwenda miti ya mimea tiba inakwisha, hivyo ni vyema wadau wa dawa za asili wakaanza kufikiria kuanzaisha vitalu vya mimea tiba kwa ajili ya kuifanya mimea hiyo kuwa endelevu.

 Profesa Kabote alisema kuwa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo ina kitengo maalum kwa ajili ya utafiti wa mimea tiba na kinatoa ushauri kwa wadau wanaotaka kuanzisha vitalu vya mimea tiba.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...