Na Mwandishi Wetu, Mwanza

SHIRIKA la Viwango Tanzania (TBS) limeendelea kufanya ukaguzi ukiendana na kutoa elimu kuhusiana na makundi 13 ya bidhaa za vipodozi kutokana na watu wengi kukumbana na changamoto ya kutambua nini maana ya bidhaa za vipodozi.

Hatua hiyo ni sehemu ya mkakati wa shirika hilo wa kufanya ukaguzi unaoendana na kutoa elimu kuhusiana na vipodozi kwa wananchi katika wilaya zote za mikoa ya kanda ya ziwa na tayari ukaguzi na elimu imetolewa kwenye Wilaya za Nyamagana na Ilemela, jijini Mwanza.

Akizungumza wakati wa ukaguzi wa bidhaa za vipodozi uliofanywa na Ofisi ya TBS Kanda ya Ziwa, Kaimu Mkuu wa Kanda hiyo, Evarist Mrema, alisema ukaguzi huo ukiendana na kutoa elimu unafanyika kwenye maduka ya rejareja, jumla, kwa wasambazaji, supermarkets, migahawa na kwingineko.

Akifafanua zaidi, Mrema alisema; " Tunafanya ukaguzi na kutoa elimu kwa upande wa vipodozi, kwani watu wamepata changamoto ya kujua ni nini maana ya bidhaa za vipodozi, tunaliona hilo nalo ni changamoto kwenye ukaguzi huu na tunahitajika kutoa elimu na tunatoa elimu na tunaendelea kutoa elimu wakati wa ukaguzi."

Alisema aina za vipodozi zipo katika makundi 13 na kundi la kwanza ni za bidhaa za watoto kama vile poda, shampuu na kundi la pili ni la bidhaa zinazotumika bafuni.

"Huko nako kuna bidhaa tofauti zinazotumika bafuni kama sabuni za kuogea pamoja na zile ambazo watu wanaziandaa katika maeneo yao ya kuogelea na vitu kama hivyo," alisema Mrema.

Alitaja kundi lingine kuwa bidhaa za nywele ambako kuna makundi yake kama mawili au matatu. Kwa mujibu wa Mrema kuna rangi za nywele ambazo zinatumika kwenye nywele, lakini pia kuna nywele zinazoongezwa ndani ya nywele asili kama rasta na wigi na kwamba hizo zote ni aina za bidhaa za vipodozi.

Bidhaa nyingine kwa mujibu wa Mrema ni zile ambazo zinapakwa juu ya ngozi kama mafuta ya kupaka, losheni na bidhaa nyingine zinatumika kwa upande vidole vya akina mama mfano kucha bandia na midomo ambazo nazo ni sehemu ya bidhaa za vipodozi.

Alitaja aina nyingine za bidhaa za vipodozi kwa upande wa urembo zinazotumika kwenye macho akisema zote hizo ni aina za vipodozi na wananchi wataendelea kufamua kaguzi zinazoendana na kutoa elimu kuhusiana na bidhaa hizo.

Wakizungumzia kuhusiana na ukaguzi huo, wananchi wengi walielezea kufurahishwa na hatua hiyo kwani wamekuwa wakibambikwa bidhaa za chakula na vipodozi zilizokwisha muda na vilevile kuuziwa vipodozi zenye viambata sumu.

"Kwa hiyo shirika linatusaidia kuwadhibiti na waendelee kwa nguvu hiyo hiyo hadi maduka ya vijijini," alisema mmoja wa wananchi aliyejitambulisha kwa jina la Machibya Samuel.

Wauzaji madukani wameomba shirika liwafikirie katika malipo ili walipe kwa mikupuo miwili au zaidi kama wanavyofanya TRA, kwani biashara ni ngumu.

Mkaguzi wa TBS akitoa bidhaa ambazo hazina muda wa matumizi

Bidhaa zilizoisha muda wake

Bidhaa zenye viambata sumu ambazo zimepigwa marufuku.

 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...