
Waziri wa Kilimo Prof. Adolf
Mkenda ( kulia) akiwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Taasisi ya Utafiti wa
Kilimo (TARI) Dkt. Yohana Budeba ( kushoto) jana alipotembelea makao
makuu ya TARI yaliyopo Makutupola Dodoma kukagua utendaji kazi wa
taasisi hiyo .Pichani wakikagua shamba mama la uzalishaji wa mbegu za
zabibu.Waziri
wa Kilimo Prof. Adolf Mkenda akiongea na waandishi wa habari jana
alipotembelea shamba mama la zabibu lililopo makao makuu ya Taasisi ya
Utafiti wa Kilimo (TARI) Makutupola Dodoma ambapo alihimiza utolewaji wa
elimu ya kuhamasisha wakulima na wananchi kuanzisha mashamba ya zabibu
ili nchi ijitosheleze malighafi za viwanda vya kutengeneza mvinyo.
*****************************************************
Wizara ya Kilimo imejipanga kuhakikisha inaleta mapinduzi ya sekta ya kilimo kwa kuboresha huduma za ugani ili wakulima waweze kuzalisha kwa tija na kuongeza pato la taifa kwa kuwa na mazao mengi na bora.
Hatua hiyo itafikiwa kutokana na mipango mahsusi ambapo wizara imeandaa mkutano maalum wa maafisa kilimo wa mikoa na halmashauri nchini kujadili changamoto na suluhisho la upatikanaji wa huduma bora za ugani ili wakulima wapate tija na kuongeza uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara.
Waziri wa Kilimo Prof. Adolf Mkenda ametoa taarifa rasmi ya kufanyika mkutano huo jana (04.01.2021) Jijini Dodoma wakati alipotembelea Makao Makuu ya Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) Makutupola.
Prof. Mkenda alisema mkutano huo utakaofanyika mapema wiki ijayo utahusisha Maafisa Kilimo wa mikoa na Halmashauri zote nchini ili kuweka mikakati itakayoingizwa kwenye bajeti ya wizara ya mwaka 2021/2022 kuwezesha kutatua kwa hatua changamoto za huduma za ugani kwa wakulima.
“Tunataka tutenge fedha mahsusi kwenye bajeti ijayo 2021/2022 kwa ajili ya kuboresha huduma za ugani kwa kuwafundisha maafisa ugani kanuni bora za usimamizi wa mazao mfano zabibu, pamba nk ambapo kwa kuanzia tutachagua mikoa baadhi ya kuanza utekelezaji ili baada ya mwaka mmoja tupime matokeo yake kwenye uzalishaji na tija” alisema Prof. Mkenda.
Waziri huyo wa Kilimo aliongeza kusema wizara inataka kupitia bajeti ijayo fedha zitatengwa itoe mafunzo kwa maafisa ugani ( re-training) juu ya mazao mbalimabli ambayo hawana ujuzi ili wayajue na kufundisha kanuni bora kwa wakulima nchini.
“Kwa kweli tunahitaji mapinduzi ya kilimo kwani tunazungumza kwamba kilimo ni uti wa mgongo sasa maneno maneno yametosha lazima twende kwenye vitendo kuhakikisha tija kwenye kilimo na kuongeza huduma za kumsaidia mkulima kuongeza uzalishaji “ alisisitiza Prof. Mkenda.
Prof. Mkenda alisema wizara ya kilimo inathamini shughuli za ugani hivyo kufanya kila jitihada kuwakutanisha wataalam hawa na kuwajengea uwezo wa kufanya kilimo cha kisayansi na kuachana na kilimo cha mazoea ili kuleta mapinduzi ya kiuchumi.
Ametoa wito kwa Makatibu Tawala Mikoa Tanzania Bara na Wakurugenzi wa Halmashauri zote kuwaruhusu maafisa kilimo wao mara barua za mialiko zitakapofika ili wakashiriki mkutano huo ambao wizara ya kilimo inauratibu.
Prof. Mkenda amebainisha maeneo manne ya kipaumbele kwa wizara ya kilimo kuhakikisha mapinduzi ya kilimo yanafikiwa kwanza, kuhakikisha mbegu bora zinapatikana kwa wingi na kwa gharama nafuu.
Pili, kuhakikisha wakulima wanafikiwa na elimu juu ya kanuni bora za kilimo ili wakuze tija na uzalishaji na tatu upatikanaji wa masoko ya uhakika ya mazao ya wakulima
Nne, wizara ya kilimo itahakikisha suala la upatikanaji mitaji ya kuendeleza shughuli za kilimo inapatikana kwa wakulima na wawekezaji kwa riba nafuu ikiwemo mikopo toka taasisi za kifedha.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya TARI Dkt. Yohana Budeba alisema taasisi yake itaendelea kuhakikisha wakulima wanapata mbegu bora za mazao ya kilimo zilizofanyiwa utafiti na kuthibitishwa kuwa na kiwango cha juu cha kumwezesha mkulima kupata tija na kukuza kilimo.
Dkt. Budeba aliishukuru serikali ya awamu ya tano chini ya Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuiwezesha taasisi ya utafiti wa Kilimo kutekeleza majukumu yake ikiwemo kutoa huduma za ugani kwa wakulima kwenye vituo vyote 17 nchini hali inayosaidia kukuza uzalishaji wa mazao nchini.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...