Na Munir Shemweta, WANMM LINDI
Katika
kinachoonekana kusogeza huduma za Mabaraza ya Ardhi na Nyumba katika
wilaya mbalimbali nchini, Serikali imewaelekeza Makatibu Tawala wa mikoa
kuhakikisha wajumbe Washauri wa Mabaraza ya Ardhi na Nyumba wanateuliwa
kwa ajili ya kuhudumia wilaya zisizokuwa na Mabaraza ili kuondoa kero
kwa wananchi kutembea umbali mrefu kuzifuata huduma hizo.
Hayo
yameelezwa na Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt
Angeline Mabula tarehe 5 Januari 2021 mkoani Lindi wakati akizungunza na
Watendaji wa Sekta ya Ardhi, uongozi wa mkoa wa Lindi na Wakurugenzi wa
halmashauri za mkoa huo akiwa katika ziara ya kukagua utendaji kazi wa
sekta ya ardhi na kuhamasisha ukusanyaji maduhuli ya serilali kupitia
kodi ya pango la ardhi.
Maelezo ya Dkt Mabula yanafuatia
kuelezwa na Mkuu wa mkoa wa Lindi Godfrey Zambi kuwa mkoa wake una
Baraza moja la Ardhi na Nyumba linalohudumia wilaya zote tano za mkoa
huo jambo alilolieleza kuwa limekuwa likileta usumbufu na kero kwa
wananchi kutembea umbali mrefu.
" Mkoa wetu una Baraza moja tu la
Ardhi na Nyumba la wilaya linalohudumia wilaya za mkoa huu, fikiria mtu
anatoka Liwale kuja hapa umbali wa kilometa 250 au Kilwa Kimeta 200 ni
kumuumiza mwananchi" Alisema Mkuu wa Mkoa wa Lindi Godfrey Zambi.
Kwa
sasa kuna jumla ya Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya 57 yanayotoa
huduma nchini wakati sheria inataka kuwa na Mabaraza 139 jambo
linalosababisha baadhi ya wilaya kukosa huduma za Mabaraza na kuwafanya
wananchi kuzifuata huduma kwa kutembea umbali mrefu.
Dkt Mabula
alisema, baada ya Serikali kuona wananchi wanapata shida ya kuzipata
huduma za Mabaraza ya ardhi sasa imeamua kuwaelekeza Makatibu Tawala wa
Mikoa kuteua wajumbe Washauri wa Mwenyekiti wa Baraza la Ardhi na
Nyumba la wilaya sambamba na Wakurugenzi wa Halmashauri kutakiwa
kutenga ofisi itakayoendesha Mashauri na kuwa na Watumishi kama Makarani
ili kuwawezesha Wenyeviti kufanya kazi kulingana na mahitaji ya wilaya
husika.
"Pamoja na kuwa na Mabaraza ya Ardhi katika wilaya
mbalimbali lakini tumeona bado kuna 'gape' mahali hasa zile wilaya
ambazo hazina Mabaraza ya Wilaya, maana Baraza la wilaya moja
linahudunia wilaya tatu kwa hiyo bado hatujatatua tatizo la wananchi
kusafiri umbali mrefu ili kusogeza huduma kwa wananchi wanaoteseka"
Alisema Dkt Mabula.
Baraza la Ardhi na Nyumba la Wilaya kwa
mujibu wa sheria Na 2 ya mwaka 2002 lina wajumbe wasiozidi saba na
watatu kati yao ni wanawake na kuteuliwa na Waziri wa Ardhi Nyumba na
Maendeleo ya Makazi kutokana na Mapendekezo ya Mkuu wa Mkoa kutoka
katika eneo la wilaya husika.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula
akizungumza katika ofisi ya Mkuu wa mkoa wa Lindi tarehe 5 Januari 2021
wakati wa ziara yake ya kukagua utendaji kazi wa sekta ya Ardhi na
uhamasishaji maduhuli ya serikali kupitia kodi ya pango la ardhi.
Kushoto ni Mkuu wa mkoa wa Lindi Godfrey Zambi na kulia ni Afisa Tawala
wa Wizara ya Ardhi Baraka Mraha.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...