WILAYA ya Songea mkoani Ruvuma inatarajia kutumia zaidi ya
shilingi bilioni 5.799 kutekeleza miradi nane ya maji katika kipindi cha mwaka
2020/2021.
Meneja Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira vijijini
(RUWASA) Wilaya ya Songea Mhandisi
Mathias Charles amesema hadi kufikia Januari mwaka huu RUWASA Wilaya ya Songea
imepokea zaidi ya shilingi milioni 877 sawa na asilimia 15.12 ya bajeti
iliyopangwa.
“Hadi kufikia Januari
2021 wakazi wanaopata huduma ya maji wilaya ya Songea wanakadiriwa kuwa 132,362
sawa na asilimia 63.6 ya wakazi wote’’,alisema Charles.
Hata hivyo amesema hadi
sasa Mamlaka hiyo imetumia zaidi ya shilingi bilioni tatu kutekeleza miradi
tisa ya maji katika wilaya hiyo na
kwamba RUWASA inaendelea na kazi ya
uboreshaji wa huduma ya upatikanaji wa maji kwa kujenga miradi mipya.
Kulingana na Meneja
huyo,RUWASA inaendelea kukarabati miradi iliyokuwa imechakaa na kuboresha
usimamizi wa miradi ya maji iliyokamilika ili iwe endelevu kwa kuunda na
kusajili Jumuiya za watumiaji maji(CBWSOs) ambazo zitakuwa zinasimamia miradi
hiyo na kuhakikisha inatoa huduma wakati wote.
Amesema katika kipindi
cha mwaka 2019/2020 RUWASA Wilaya ya Songea
ilipanga kuunda na kusajili jumuiya za watumiaji maji 17 ambapo hadi
kufikia Juni 2020 jumuiya 10 zilikuwa zimeundwa na kusajiliwa.
Hata hivyo amesema kwa
mwaka wa fedha 2020/2021 jumuiya za watumiaji 28 zilipangwa kuundwa na
kusajiliwa ambapo hadi kufikia Januari 2021 jumuiya 11 zimeundwa.
Ameitaja miradi ya maji
iliyopangwa kutekelezwa katika Halmashauri ya Madaba kupitia P4R kuwa ni
Ndelenyuma,Lutukira na Mbangamawe ,kupitia PBR4 mradi mmoja wa maji katika
kijiji cha Igawisenga unatarajia kutekelezwa.
Kwa mujibu wa Meneja
huyo wa RUWASA,katika Halmashauri ya Songea vijijini kupitia P4R miradi ya maji
inatarajia kutekelezwa katika vijiji vya Lipaya,Lundusi na Maposeni,kupitia
PBR4 mradi mmoja wa maji unatarajia kutekelezwa katika kijiji cha Ndongosi na
mradi mmoja unatarajia kutekelezwa Ndilimalitembo Manispaa ya Songea.
Amesema RUWASA Wilaya
ya Songea imepanga kukamilisha zoezi la usajili Jumjuiya za watumiaji maji
ifikapo Juni 30 mwaka huu na kwamba RUWASA
imejipanga kuendelea kutoa elimu juu ya utunzaji vyanzo vya maji na
elimu kuhusu umuhimu wa ulipaji wa huduma ya maji ili kuifanya miradi iwe
endelevu.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...