Na Mwandishi Wetu, Michuzi TV
NI Ushoraba Kisarawe!Ndivyo unavyoweza kuelezea baada ya Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani Jokate Mwegelo kutangaza kwamba kutakuwa na siku tatu za Ushoroba Kisarawe Festival kwa lengo maalum la kutangaza fursa na utalii uliopo wilayani hiyo.
Akizungumza na waandishi wa habari wakati akielezea kuwepo wa tamasha hilo lililopewa jina la Ushoroba Kisarawe Festival ambalo litaanza Februari 19 hadi Februari 21 mwaka huu, Jokate amesema kutakuwa na shughuli mbalimbali za utalii ambazo zifanyika katika siku hizo.
Pia wamewaalika Waziri wa Maliasili na Utalii Dk.Damas Ndumbaro pamoja na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI) Seleman Jafo ambao nao watashuhusia na kupata fursa ya kuona utalii uliopo ndani ya Wilaya ya Kisarawe hasa kwa kuzingatia wilaya hiyo imebarikiwa na kuna maeneo mengi ya utalii.
"Lengo la kuu la kuzindua Kisarawe Ushoroba Festival ni kuutangaza utalii tulioao Kisarawe, tunayo misitu ya mazingira ya asili hapa, hata panzi mwenye rangi ya bendera ya Taifa yuko hapa, tunayo maeneo ya kihistoria na yenye kusisimua ndani ya Wilaa hii, tunao utamaduni wetu kupitia kabila la Wazaramo.
"Tunayo maeneo ambayo yakitumika vizuri ni fursa kubwa katika kuendelea sekta ya utalii Kisarawe na Taifa kwa ujumla, hivyo tumeamua kuja na tamasha hilo ambalo linakwenda kuutangaza utalii tulionao na tutakuwa na shughuli mbalimbali ambazo zitafanyika kwa siku tatu mfululizo,"amesema Jokate.
Pia amesema maana ya Ushoroba ni njia ya mapito ya wanyama mbalimbali , lakini kwao Kisarawe ndio njia rahisi pia ya kwenda katika Hifadhi ya Taifa ya Mwalimu Nyerere.
"Kwa kutumia njia ya Kisarawe kwenda Hifadhi ya Taifa ya Mwalimu Nyerere ni karibu zaidi kuliko njia nyingine.Ndio maana Rais wetu Dk.John Magufuli alishatangaza na kutoa tamko kuhusu barabara hii, sisi ni wajibu wetu kuanza kujipanga , kwani usipojipanga utapanguliwa na wengine watapangwa kwa niaba yako, sasa sisi tumejipanga kupitia tamasha hili.
"Na ndio chimbuko la kuita hili tamasha Ushoroba, maaana hata Waziri wa Maliasili na Utalii aliyekuwepo kipindi kile alitamka hii njia kwasababu inatazamiwa kuwa njia rasmi ya watalii kuitumia kutoka Dar es Salaam ulipo Uwanja wa Ndege wa Kimataifa kuingia kwenye hifadhi yetu hii ya msitu.
"Kwa hiyo na sisi tukaita Ushoroba ili kuelezea yale matamanio ya viongozi wetu. Na tupo tayari kutoka maeneo ya ardhi bure kwa wale ambao wataonesha nia ya kuja kuwekeza katika sekta ya utalii, tunawakaribisha, waje tutazungumza,"amesisitiza Jokate.
Ameongeza Wilaya hiyo imekuwa na jitihada mbalimbali za kuhamasisha utalii na kwa sehemu kubwa wamefanikiwa kwani idadi ya wanaotembelea vivutio vilivyopo imeongezeka. Pia mapato yatokanayo na utalii wa Kisarawe nayo yameongezeka kutoka Sh.milioni nne hadi Sh.milioni 12
Jokate amewakaribisha wadau wa utalii kutoka maeneo yote kufika katika tamasha hilo kwani kuna mambo mengi yameandaliwa ikiwemo kutafuta panzi mwenye rangi ya bendera ya Taifa, kutembelea hifadhi ya msitu wa mazingira asilia ya Kazimzumbwi, kutembelea Hifadhi ya Taifa Mwalimu Nyerere pamoja na matukio mengine mengi yatakayofanyika.
Kwa upande wake Mhifadhi Mwandamizi Idara ya Utalii Hifadhi ya Mwalimu Nyerere Seth Mihayo amesema tamasha hilo ni muhimu hasa katika kushirikiana na Serikali kwa lengo la kuongeza idadi ya watalii nchini Tanzania , na Kisarawe ni sehemu ambayo imekaa kimkakati kwa ajili ya kiunganishi cha utalii kutoka Dar es Salaam kwenda Hifadhi ya Nyerere yenyewe pamoja na hifadhi nyingine ambazo ziko kwenye Ikolojia katika upande huo.
"Tunakupongeza Mkuu Wilaya ya Kisarawe kwa uamuzi huu wa kuja na hili tamasha kubwa ambalo linakwenda kuutangaza utalii wa Kisarawe na Taifa kwa ujumla. Tukuahidi tutaendelea kushirikiana nawe ili kutimiza azma ya kukuza sekta ya utalii nchini,"amesema Mihayo.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...