KAMPUNI ya Mohamed
Enterprises imetoa msaada wa vyakula na sabuni vilivyogharimu zaidi ya shilingi
milioni 1.8 kwa vituo vitatu vya kulelea watoto yatima mjini Songea mkoani
Ruvuma.
Mwakilishi wa Kampuni
hiyo Angel Samasuba akizungumza mara
baada ya kumaliza zoezi la ugawaji wa msaada huo,amevitaja vituo vya kulelea
yatima vilivyopata msaada huo kuwa ni Kituo cha SWACCO kilichopo Kata ya
Mwengemshindo, St.Antony cha Mfaranyaki na Kituo cha Mchungaji Mwema kilichopo
Mjimwema.
Samasuba amesema
Kampuni ya Mohamed Enterprises katika vituo vyote vitatu imetoa jumla ya lita 120 za mafuta
ya kula zilizogharimu shilingi 516,000
na mifuko ya unga wa sembe kilo 300 iliyogharimu shilingi 234,000.
Misaada mingine
iliyotolewa ni sabuni za miche katoni 12 zenye thamani ya shilingi
120,000, juisi katoni 30 zenye thamani ya shilingi 195,000 na
mbuzi sita wenye thamani ya shilingi 600,000.
“Sisi kama Kampuni ya
Mohamed Enterprises tumekuwa na kawaida ya kutoa misaada kwa makundi maalum na
vituo vya kulelea watoto yatima kwa lengo la kuunga mkono jitihada za serikali
za kuwasaidia watu wenye uhitaji ili kuwafariji na kuwatia moyo.’Alisema
Samasuba.
Akizungumza mara baada
ya kupokea msaada huo Mwakilishi wa kituo cha kulelea yatima cha Mchungaji mwema cha Mjimwema Sr. Maria
Veronika OSB ,ameishukuru Kampuni hiyo kwa msaada huo ambao amesema
utawasaidia watoto 39 ambao wanalelea na kituo hicho.
Naye Mwakilishi wa
kituo cha kulelea watoto yatima cha SWACCO Castrol Whero amesema kitendo
kilichofanywa na Mohamed Enterprise kimeleta faraja kubwa kwa sababu yatima ni
kundi maalum lililopo katika jamii linalohitaji msaada.
Amesema kituo cha
SWACCO kilianza mwaka 2000 kikiwa na watoto 50 ambapo hivi sasa kituo hicho
kinalea watoto 23 na watoto 31 wanahudumiwa wakiwa majumbani na walezi wao.
Vinsent Ndumbaro ni Kaimu
Afisa Ustawi wa Jamii Mkoa wa Ruvuma akizungumza kwa niaba ya serikali,ameipongeza na kuishukuru Kampuni
ya Mohamed Enterprise kuunga mkono juhudi za serikali za kuwasaidia watu wenye
mahitaji maalum ambapo ametoa rai kwa wadau wengine kuiga mfano huo.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...