Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi akizungumza  na Wenyeviti pamoja na Wasajili Wasaidizi wa Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya wakati akitoa maagizo kwa wenyeviti kuanza kutumia lugha ya Kiswahili katika kuandika hukumu. Kulia kwa Lukuvi ni Naibu Waziri wa Ardhi Dkt Angeline Mabula na kushoto ni Katibu Mkuu Mary Makondo.

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi akizungumza na Wenyeviti na Wasajili Wasaidizi wa Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya nchini wakati akitoa maagizo ya kuanza  kutumika lugha ya Kiswahili kwenye hukumu za Mabaraza ya ardhi. (PICHA ZOTE NA MUNIR SHEMWETA)

*******************************************

Na Munir Shemweta, WANMM DODOMA

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi amewaagiza Wenyeviti wa Mabaraza ya ardhi na Nyumba ya wilaya kutumia lugha ya Kiswahili katika kuandika hukumu.

Lukuvi alitoa maagizo hayo tarehe 5 Februari 2021 jijini Dodoma alipozungumza na Wenyeviti pamoja na Wasajili wa Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya kwa nchi nzima kupitia Video (Video conference).

‘’Nasisitiza wenyeviti wa Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya mtumie lugha ya Kiswahili wakati wa kuandika hukumu zenu kama alivyoagiza mhe Rais Dkt John Pombe Magufuli na nitashangaa kumuona mwenyekiti akiandika hukumu kwa lugha ya kiswahili’’ alisema Lukuvi

Aidha, Lukuvi aliwataka pia wenyeviti hao wa Mabaraza kuchapa hukumu za maamuzi wanayotoa wao wenyewe bila kutegemea Makarani na hukumu hizo zitoke kwa wakati na kusisitiza kuwa katika dunia ya leo suala la uzembe halina nafasi.

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi aliongeza kwa kusema kuwa, pamoja na kuwepo uchache wa watumishi kwenye baadhi ya ofisi za Mabaraza ya Ardhi lakini watendaji hao wanatakiwa kuwajibika na kuacha visingizio pamoja na kufanya kazi kwa mazoea kwa kuwa serikali iko katika juhudi za kuhakikisha inajaza nafasi.

Kwa mujibu wa Lukuvi, hivi sasa ni wajibu wa watendaji wa mabaraza ya ardhi kufanya kilicho sahihi na kuwa wabunifu sambamba  na kuwajibika kwa kutoa hukumu kwa wakati  na kusisitiza wananchi masikini wanategemea sana matumizi ya Kiswahili.

‘’Maamuzi yetu kama wenyeviti wa Mabaraza yawe rahisi na sisi tuwe wa kwanza kuwasaidia wananchi na kila mwenyekiti atekeleze maamuzi haya kwa lugha ya Kiswahili’’ alisema Lukuvi

Kwa mujibu wa Waziri Lukuvi, wapo wananchi waliokosa haki zao ama kuchelewa kukata rufaa kutokana na kutokujua kilichoandikwa katika hukumu kwa kuwa kimeandikwa kwa kiingereza.

Kwa upande wake Msajili wa Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya Stella Tullo aliwataka Wenyeviti wa Mabaraza kuanza kutekeleza maagizo ya Waziri wa ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi mapema kwa kuzingatia sheria na taratibu.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...