Na John Nditi, Morogoro

MKUU wa Wilaya ya Morogoro ,Bakari Msulwa amewataka wananchi waliovamia na kuendesha shughuli za kilimo na ufugaji kwenye Kitalu cha uwindaji cha Gonabis kilichopo hifadhi ya jamii ya wanyamapori katika eneo la Duthumi kuondoka mara moja kwa vile uwepo wao ni kinyume cha sheria na wanachangia kuharibu uoto wa asili.

Msulwa ,alitoa agizo hilo kwa wananchi wa vijiji 11 vinavyopakana na eneo la Hifadhi ya jamii ya wanyamapori akiwa ameambatana na wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama ya Wilaya hiyo pamoja na viongozi wa Halmashauri ya wilaya ya Morogoro.

Alisema eneo hilo ambalo nimevamiwa limetengwa mahususi kwa ajili ya kuhifadhi na kutunza uoto wa asili ambapo ndani yake kuna vyanzo vya maji, mazalia ya wanyama wanaoingiliana na Hifadhi ya Mwalimu Nyerere.

" Eneo hilo ambalo limetengwa kwa hifadhi lakini kuna uvamizi mkubwa umekuwepo hapo kwa shughuli za kibinadamu na tunakata tuwapelekee ujumbe wananchi wa hapo ya kwamba wakati umefika wa kuondoka na jambo hili limekuwa muda mrefu takribani miaka saba “ alisema Mkuu wa wilaya .

Mkuu wa wilaya huyo , alisema : Lakini sasa imefikia mahali tumejipanga waachie uoto wa asili uendelee , sasa waondoke maeneo hayo , ni ujumbe ambao tunataka kuusimamia kwa sababu si ujumbe mpya na sasa tunataka tuusimamie tunataka wananchi katika maeneo hayo waanza kujidnaa kisakilojia ya kuondoka eneo hilo” alisisitiza Msulwa.

Hata hivyo ,Mkuu wa wilaya na ujumbe wake walishindwa kufika eneo la hifadhi hiyo kujionea uharibifu unaofanyika kutokana na shughuli za kibinadamu baada ya magari ya msafara wake kukwama kwenye njia ya kuelekea ndani ya hifadhi hiyo na kutotimiza lengo la ziara hiyo.

Mkuu wa Wilaya aliamua kukutana na uongozi wa Jumuiya ya Kuhifadhi Matumizi Bora ya Maliasili (JUKUMU) katika kijiji cha Duthumi ambao aliwapa majukumu ya kusimamia na kuhifadhi eneo hilo.

Pamoja na jukumu hilo pia aliitaka jumuiya hiyo kuhakikisha inatekeleza majukumu yake ipasavyo yakiwemo ya kusimamishwa wananchi kuendelea na shughuli za binadamu katika hifadhi hiyo.

Mkuu wa wilaya hiyo aliitaka pia kuhakikisha kusimamia maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya vitalu yabaki bila kuingiliwa na shughuli nyingine za kilimo na ufugaji na kuangaliwa upya kwa mikataba ya kampuni zilizowekeza kwa shughuli za uwindaji.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Morogoro, Rehema Bwasi, alisema kuwa kuna kila sababu ya kuhakikiwa upya mipaka ya eneo hilo na kuweka bikoni .

Bwasi pia alisema ya kwamba, halmashauri hiyo itahakikisha kuwa hifadhi hiyo inalindwa na sio kubadili matumizi kwani ina manufaa makubwa kuanzia ngazi ya vijiji, Halmashauri na Taifa.

Naye Mwenyekiti JUKUMU , Galeko Magawa alisema kuwa eneo hilo limevamiwa na wafugaji pamoja na wakulima na chanzo kinaweza kuwa ni Kampuni ya Morogoro Hunting Safari kushindwa kwalipa malipo yao ya ulinzi na usimamizi wa eneo hilo tangu mwaka 2018 walipofunga mkataba baina yao.

Magawa ,alisema kutokana na jambo hilo kampuni hiyo imeshindwa kuendesha shughuli zake ipasavyo kutokana na uvamizi ndani ya hifadhi hiyo.

Msemaji wa Kampuni hiyo yenye kitalu cha uwindaji cha Gonabis , Ally Kingalu , licha ya kupongeza uamuzi huo wa Mkuu wa Wilaya, alisema zoezi aliloanzisha si jepesi kiutendaji kwani wafugaji waishio eneo hilo hutumia mishale kujihami.

Hata hivyo , alisema ya kwamba viongozi waliopita hawakutambua majukumu yao wakidhani kuwa eneo hilo ni mali ya kampuni si ya kwao.

Eneo hilo la Hifadhi ya jamii ya wanyamapori limezungukwa na vijiji 11 ambavyo vimepewa mamlaka ya kusimamia hifadhi hiyo yenye kitalu cha Gonabis chenye wanyama aina ya tembo, Chui, Kongoni, Nyumbu na Swala wanaotajwa kutoweka kwa kasi kutokana na shughuli za binadamu . Hata hivyo , Kampuni ya Morogoro Hunting Safari inayomiliki kitalu hicho inashindwa kushindwa kuendesha shughuli zake kutokana na mahema yao kuchomwa moto na wananchi.


Baadhi ya askari na viongozi  wengine wakilinasua  gari lililokwama  kwenye  barabara kuelekea katika   hifadhi ya jamii ya wanyamapori ambapo mkuu wa wilaya hiyo, Bakari Msulwa ( hayupo pichani ) na wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya na kushindwa  kufika  eneo husika kwa ajili ya  kujionea uharibifu unaofanyika kutokana na shughuli za kibinadamu za kilimo na ufugaji ndani ya hifadhi hiyo.( Picha na John Nditi).

Mkuu wa Wilaya ya Morogoro ,Bakari Msulwa ( waili kutoka kulia) akisisitiza jambo kwa viongozi wa JUKUMU , Kampuni ya Morogoro Hunting Safari pamoja na wa Halmashauri ya wilaya ya Morogoro kuhusu usimamizi wa hifadhi .


 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...