kulia ni Mhandiisi wa RUWASA Mkoa wa Ruvuma Mhandisi Rebman Ganshonga akielezea mradi wa maji Lilambo Manispaa ya Songea,wakati Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Christina Mndeme alipokagua mradi huo uliogharimu zaidi ya shilingi milioni 100Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Christina Mndeme akipanda juu ya tanki la mradi wa maji Lilambo Manispaa ya Songea kwa lengo la kukagua.
===== ======= ======= ======== =======
Mradi mkubwa utakaomaliza kero ya maji Manispaa ya Songea unakuja
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Christina Mndeme amesema serikali inakwenda kutekeleza mradi mkubwa unaofadhiliwa na nchi ya India ambao unakwenda kumaliza kero ya maji katika Manispaa ya Songea.
Akizungumza ofisini kwake kuelekea maadhimisho ya wiki ya maji inayoanza Machi 16 hadi 22 mwaka huu,Mndeme amesema mradi huo unaofadhiliwa na serikali ya India unagharimu zaidi ya Dola za Marekani milioni 45.3.
“Kinachoendelea hivi sasa kupitia Wizara yetu ya Maji,ni hatua za manunuzi ya wakandarasi wa kutekeleza mradi huo mkubwa ambao utahusisha ujenzi wa bwawa la kuhifadhia maji ambalo litakuwa na uwezo wa kuhifadhi maji lita bilioni tano’’,alisema Mndeme.
Amesema mradi huo pia utahusisha upanuzi wa mtambo wa kusafisha maji na kutibu maji safi zaidi ya lita milioni 51.4 kwa siku,ujenzi wa matanki manne ya kuhifadhi maji yenye uwezo wa lita milioni 18.2 na ulazaji wa mabomba yenye uwezo wa kusafirisha maji kilometa 190.3.
Mndeme amesema mradi huo utakapokamilika zaidi ya asilimia 95 ya wakazi wa Manispaa ya Songea watakuwa wanapata huduma ya maji safi na salama.
Amesema wananchi wa Manispaa ya Songea ambao hawajafikiwa na huduma ya maji,kupitia mradi huu mkubwa watapata maji na kuwezesha asilimia ya usambazaji maji kwenye manispaa hiyo kuongezeka toka asilimia 86.2 hadi 95 na kwamba lengo ni kufikia asilimia 100 ya kutoa maji katika miji ya Songea,Tunduru na Mbinga.
Hata hivyo amesema katika miji ya Mbinga na Tunduru serikali inatenga fedha kwenye bajeti ya kila mwaka kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya usambazaji wa huduma ya maji kwa wananchi.
Kwa upande wake Meneja wa RUWASA Mkoa wa Ruvuma Mhandisi Rebman Ganshonga amesema ili miundombinu ya maji iwe endelevu, wananchi wanatakiwa kuilinda miundombinu na kuvitunza vyanzo vya maji kwa sababu serikali inawekeza fedha nyingi kwenye miradi hiyo.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...