NA BALTAZAR MASHAKA, Mwanza
WAFANYABIASHARA baadhi jijini Mwanza wanadaiwa kuvamia kiwanja cha Msikiti wa Ijumaa wilayani Nyamagana na kujenga miundombinu ya biashara kwenye kiwanja kinachomilikiwa na msikiti huo.
Kiwanja hicho Namba 50, chenye hati namba 033027/98,katika Kitalu Q kilichopo kwenye maungio ya Barabara ya Uhuru na Mtaa wa Mission, kinadaiwa kuvamiwa na wafanyabiashara hao mwaka jana na kujenga maduka na mkaa kinyume cha Sheria ya Mipango Miji ya Halmashauri ya Jiji la Mwanza.
Katibu wa Bodi ya Msikiti wa Ijumaa,Alhaji Abdallah Amin Abdallah, akizungumza na gazeti hili jana, alisema wafanyabiashara hao wamevamia kiwanja hicho mali ya taasisi ya dini ya Kiislamu kisha wakavunja uzio na kujenga miundombinu ya kudumu ya biashara yao.
Alisema uzoefu unaonyesha mali za taasisi zimekuwa zikiporwa kwa njia hiyo na kusababisha migogoro hivyo Bodi ya Wadhamini ya Msikiti wa Ijumaa,baada ya kubaini hilo, Oktoba Mosi,2020 iliuandikia uongozi wa Jiji la Mwanza barua yenye kumb.Na.RTJM/GEN/TEMP 2020 ikilalamikia kiwanja chake kuvamiwa na kujengwa miundombinu ya biashara.
Alhaji Abdallah alisema barua hiyo ilijibiwa Oktoba 21, 2020 kwa barua yenye kumb.Na.MCC/L/2007/53/VBP na kusainiwa na A.R.Kasuka kwa niaba ya Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza na kupokelewa na Bodi ya Msikiti, Januari 14, 2021.
Barua hiyo ilieleza kuwa wamiliki halali wa kiwanja hicho ni Bodi ya Wadhamini wa Msikiti wa Ijumaa kwa hati namba 033027/98,hivyo kupitia hati hiyo wanawajibika kulinda mipaka ya kiwanja chao kisivamiwe wala kisiendelezwe na mtu au taasisi nyingine,kinyume cha sheria.
Pia wanao wajibu wa kuwaondoa watu/taasisi waliojenga ndani ya kiwanja hicho namba 50,Kitalu Q mali ya Bodi ya Wadhamini wa Msikiti wa Ijumaa.
Mwenyekiti wa Kamati ya Mpito ya Bodi ya Msikiti wa Ijumaa,Sheikh Amani Mauba,alikiri kiwanja hicho kumilikiwa na msikiti huo na kamati yake iliruhusu wafanyabiashara hao kujenga miundombinu ili kulinda usafi wa eneo na kuuingizia msikiti kipato.
“Tumewapa sisi baada ya kuona eneo limekaa mkao usio mzuri, pale kuna permit (kibali) cha kujenga ghorofa,uwezo haupo hivyo tukaona turuhusu ili msikiti upate kipato,kwa hiyo hakuna mtu amevamia,”alisema.
Alieleza kuwa mmoja wa wafanyabiashara aliyekutwa hapo aliwekwa na Abdallah Amin lakini kwa sababu ya mgogoro uliopo aliandika barua kwa Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza, akilalamikia kiwanja hicho kuvamiwa.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...