Na Amiri Kilagalila, Njombe
WASHTAKIWA watano waliokuwa wakikabiliwa na kesi ya mauaji namba 84 ya mwaka 2014 ya Alice Mtokoma (56), mkazi wa kijiji cha Usalule kilichopo mkoani Njombe wamehukumiwa adhabu ya kunyongwa hadi kufa.

Wakisomewa shtaka hilo leo Machi 31, 2021 na mawakili wa serikali Andrew Mandwa na Matiko Nyangelo katika kikao cha mahakama kuu kilichofanyika mkoani Njombe mbele ya Jaji Firmin Matogolo, walisema watuhumiwa hao Mei 13, 2012 walimuua kwa kumpiga Alice Mtokoma kwa kitu chenye ncha kali, kosa ambalo ni kinyume na kifungu cha sheria na 196 na 197, kanuni ya adhabu, sura ya 16, marejeo ya 2019.

Wakili Nyangelo alieleza kuwa siku ya tukio hilo, watuhumiwa walimfuata nyumbani kwake marehemu na kumueleza kuna sehemu wanatakiwa kwenda naye ndipo walipotekeleza mauaji hayo.

Hukumu hiyo ya kunyongwa hadi kufa kwa washtakiwa hao ilitolewa na Jaji Matogolo katika kikao cha Mahakama Kuu kilichofanyika mkoani Njombe.

Alisema washtakiwa waliohukumiwa adhabu hiyo ya kunyongwa hadi kufa ni James Msumule, Emmanuel Ngailo, Izack Ngailo, Anitha Mbwilo na Upendo Mligo.

Alisema chanzo cha washtakiwa hao kutekeleza mauaji hayo ni kutokana na kifo cha mume wa Upendo Mligo, ambaye ni mtoto wa Anitha Mbwilo lakini baada ya kifo hicho ndipo wawili hao walikwenda kwa mganga ili kubaini chanzo cha kifo cha kijana huyo.

Alisema baada ya kwenda kwa mganga waliambiwa kuwa aliyemuua kijana wao ni marehemu Alice Mtokoma ambaye alikuwa mke mwenzie na mshtakiwa Anitha Mbwilo.

"Baada ya kupewa maelezo hayo ya mganga, Anitha na Upendo walikula njama ya kutafuta watu ili kumuua Alice Mtokoma," alisema Matiko.

Alisema Upendo Mligo na Anitha Mbwilo waliwatafuta washtakiwa wengine watatu ambao ni James Msumule, Emmanuel Ngailo na Izack Ngailo na kuwapa kiasi cha fedha Sh300,000 ili wafanye mauaji hayo.

Kutokana na kosa hilo walilotenda washtakiwa hao, Jaji Matogolo aliwahukumu adhabu ya kunyongwa hadi kufa kwa kufuata kifungu 197 cha kanuni ya adhabu, sura ya 16 marejeo ya 2019, ikisomwa pamoja na kifungu 322 (1)(2) cha sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai sura ya 20, marejeo ya 2019.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 1 mpaka sasa

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...