Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe William Lukuvi akizungumza na wananchi wa maeneo ya Chasimba, Chatembo na Chachui katika manispaa ya kinondoni alipokwenda kuhitimisha mgogoro wa muda mrefu katika eneo hilo baina ya wananchi na Kiwanda cha Saruji cha Wazo tarehe 13 Machi 2021.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe William Lukuvi akiwa na viongozi wa Chama na Serikali katika wilaya ya Kinondoni akikagua baadhi ya nyumba zilizojengwa eneo la mgogoro la Chasimba alipokwenda kuhitimisha mgogoro huo tarehe 13 Machi 2021.
Mgogoro huo wa kiwanja chenye ukubwa wa hecta 224.8 uliodumu kwa takribani Miaka Saba ukihusisha wananchi wapatao 4000 kutoka cha simba, chatembo, chachui pamoja na kiwanda cha saruji cha Wazo umemalizika leo.
Hatua hiyo imefikiwa baada ya Waziri wa Ardhi, nyumba na maendeleo ya makazi Mhe.William lukuvi kukutana na wananchi katika mkutano wa hadhara na kutoa mapendekezo yaliyofikiwa katika mazungumzo ya muda mrefu kati ya Serikali na bodi ya kiwanda cha saruji kuhusiana na mstakabali wa wananchi katika eneo ambalo thamani yake ni takribani bilioni 60 za kitanzania.
Amesema ” Leo tunabadilisha historia ya kuitwa wavamizi , na kuwa wamiliki halali baada ya kila mmoja wenu kutimiza wajibu wake unaompasa ndani ya miezi sita kuanzia Sasa, utakaompa kila mwananchi haki ya kumiliki kihalali baada ya taratibu zote za umilikishwaji kukamilika. Hii ndio Serikali ya Dr.John Pombe Joseph Magufuli inayojali wananchi wanyonge” Mhe. William Lukuvi..
Aidha amesisitiza kuwa lengo la Serikali si kuingilia muhimili wa mahakama, bali ni kutafuta suluhu yenye lengo la kunufaisha pande zote mbili kwa mstakabali wa nchi yetu.
Ameongeza kuwa kukamilika kwa wajibu wa kila mwananchi kutafuatiwa na taratibu za umilikishwaji wa ardhi kihalali na upatikanaji wa maeneo muhimu kama vile maeneo ya makazi, biashara, huduma za Jamii, maeneo ya shule, zahanati, ofisi chekechea, makanisa na masoko.
Katika hatua nyingine Mhe. Lukuvi ameruhusu Manispaa ya Kinondoni kupeleka huduma muhimu za Jamii Kama vile shule, zahanati, vituo vya afya pamoja na kuboresha mtandao wa barabara utakaowarahisishia wananchi hao katika shughuli zao za kila siku.
Mkutano huo umehudhuriwa pia na viongozi mbalimbali wakiwemo wa vyama na Serikali kwa lengo la kuongeza nguvu ya pamoja Katika kuhakikisha Sera ya Serikali ya awamu ya tano ya kutetea wanyonge inatekelezwa.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...