Charles James, Michuzi TV

WIZARA ya Elimu Sayansi na Teknolojia imewataka watumishi wake wote nchini kuzingatia nidhamu, ubunifu, maadili na weledi katika kazi zao ili kukuza kiwango cha elimu nchini.

Kauli hiyo imetolewa leo jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia, Omary Kipanga wakati akifunga mkutano wa 28 wa Baraza la 10 la Wafanyakazi wa Wizara hiyo.

Akizungumza na watumishi hao, Naibu Waziri Kipanga amewataka watumishi hao kuzingatia yale yote waliyoelekezwa na Waziri wa wizara hiyo, Prof Joyce Ndalichako jana wakati akifungua baraza hilo ambapo alisisitiza nidhamu kazini na kuacha kutumia lugha za ubabe kwa wateja ambao ni wananchi.

Ametoa rai kwa vyama vya wafanyakazi kama Tughe na Chama cha Walimu Tanzania CWT kushirikiana na Menejimenti ya Wizara kuhakikisha wanasimamia ipasavyo nidhamu na kukuza ubunifu kwa wafanyakazi lengo likiwa ni kuifanya wizara izidi kufanya vizuri kama ambavyo ilisifiwa na Rais Samia Suluhu Hassan.

" Nasisitiza mshikamano baina yetu watumishi, ili tuzidi kupongezwa kwa kufanya kazi vema ni lazima tushikamane tukiwa wamoja na wenye upendo, niombe kwa pamoja tuwe mabalozi wazuri wa kusimamia nidhamu na uwajibikaji kwenye vituo vyetu vya kazi.

Wizara yetu ndio uti wa mgongo wa Taifa letu, bila kukuza kiwango cha elimu na kuzalisha watalaamu wengi nchini ni vigumu kama Taifa kupata maendeleo, ni vema tukatoka na mkakati wa kuhakikisha tunazalisha vijana wasomi wenye tija kwa Taifa letu katika kuajiriwa na kujiajiri wenyewe," Amesema Kipanga.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara hiyo ambaye pia ndiye Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi, Dk Leonard Akwilapo ameahidi kuwa watayafanyia kazi maelekezo yote yaliyotolewa kwao na Waziri Prof Ndalichako na kwamba watatekeleza yale yote yaliyokusudiwa na baraza hilo katika kukuza kiwango bora cha elimu nchini.

Nae Mwenyekiti wa Tughe, Archie Mntambo amesema wataendelea kufanya kazi kwa bidii na ufanisi mkubwa ili kulinda sifa ya wizara hiyo ambayo imekuepo kiasi cha kupokea sifa kutoka kwa Rais Samia.

" Nikuhakikishie Naibu Waziri yale yote mliyotuelekeza tutayafanyia kazi kuhakikisha tunakua wabunifu, wenye weledi na nidhamu katika kazi lengo likiwa ni kuzalisha kundi kubwa la vijana wasomi wenye tija kwa Taifa letu," Amesema Mntambo.

Naibu Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia, Omary Kipanga akizungumza na wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi wa Wizara hiyo katika mkutano wa 28 wa baraza hilo jijini Dodoma.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi wa Wizara hiyo akizungumza katika mkutano wa Baraza hilo jijini Dodoma leo.
Mwenyekiti wa TUGHE Taifa, Archie Mntambo akitoa shukrani zake kwa mgeni rasmi Naibu Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia, Omary Kipanga wakati wa kufunga mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa Wizara hiyo ya Elimu.
Wajumbe wa mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia wakiwa kwenye mkutano wao wa pamoja uliofanyika jijini Dodoma kwa siku mbili jana na leo.
 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...