Na Amiri Kilagalila, Njombe

Msongamano wa wafungwa kwenye gereza kuu la mkoa wa Njombe (mpechi) umekuwa kikwazo kikubwa katika utendaji kazi za kila siku katika gereza hilo.

Hayo yameelezwa leo na mkuu wa gereza hilo mkoa wa Njombe, Emmanuel Lwinga katika uzinduzi wa bodi ya Parole ya mkoa huo uliofanyika mkoani hapa.

Amesema gereza hilo lilipaswa kuwa na wafungwa wasiozidi 100 lakini kwasasa kuna wafungwa 300 hali inayosababisha gereza hilo kuwa na msongamano mkubwa.

Amesema  kutokana na wilaya ya Wanging'ombe kutokuwa na gereza hivyo wafungwa wote wa wilaya wanapelekwa katika gereza la mkoa na kusababisha wafungwa kujaa katika gereza hilo.

Amesema kupitia sheria ya Parole itasaidia kupunguza msongamano gerezani kwasababu sheria hiyo inaruhusu wale wenye vigezo ambao wamefungwa zaidi ya miaka minne kunufaika na sheria hiyo.

Amesema  mchako wake unaanzia gerezani kwa kupendekeza jina la mfungwa kisha kwenda katika kijiji anachotoka mfungwa huyo kwa ajili ya kuchunguza.

"Yule aliyefanyiwa kosa anahojiwa kama wanaweza kumpokea na akikubali mapendekezo yanapelekwa bodi ya mkoa na bodi hiyo inapeleka ngazi ya taifa na baadae kwa waziri," amesema   Lwinga.

Amesema wanufaika wa sheria hiyo ni wale wenye makosa madogo isipokuwa ya yanayohusiana na ubakaji na uhalifu wa kutumia silaha, hawahusiki na msamaha huo.

Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Mhandisi Marwa Rubirya ambaye alikuwa mgeni rasmi katika uzinduzi huo uliofanyika gerezani hapo amesema  malengo ya kuanzishwa bodi ya Parole ni kupunguza changamoto kubwa ya msongamano wa wafungwa katika magereza.

Amesema bodi hiyo itasaidia kupitia orodha ya baadhi ya majalada ili kuona uwezekano wa kupunguza msongamano kwa baadhi yao kuachiwa chini ya sheria hiyo.

"Lengo la pili ni kushirikisha jamii katika suala zima la urekebishaji wa tabia kwa wale wanaokutwa na hatia" amesema  Rubirya.

Baadhi ya wajumbe wa bodi hiyo akiwemo Sheikh wa Mkoa wa Njombe, Rajabu Msigwa na Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) dayosisi ya Kusini, George Fihavango wamesema jamii inapaswa kujifunza kusamehe kwakuwa kila mmoja ni mkosaji mbele ya mungu.

"Katika mazingira ya kidini hata sisi huwa tunamkosea muumba wetu na yeye huwa anatusamehe, anasema nipo tayari kuwasamehe waja wangu pindi wanaponiomba msamaha," amesema  Rajabu.

 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...