Na WAMJW-Dodoma

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Dorothy Gwajima amewataka watumishi wa Wizara hiyo pamoja na Sekta ya Afya kwa ujumla kukubali mabadiliko ya uongozi na kuangalia namna ya uendeshaji ili kuzidisha uweledi katika maeneo yao ya kazi.

Waziri Gwajima amesema hayo leo wakati wa hafla fupi ya kuwapokea viongozi wapya walioteuliwa na  Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan na kuapishwa mapema wiki hii.

Viongozi hao ni Katibu Mkuu Prof. Abel Makubi pamoja na Mganga Mkuu wa Serikali Dkt. Aifello Sichwale ambao leo wameripoti rasmi ofisi za  Wizara  jijini Dodoma.

"Tuimalishe mifumo ya kufanya kazi pamoja kama tulivyoimarisha mifumo ya kufanya na mataifa mengine, tuna makubaliano ya kufanya kazi pamoja katika kutekeleza dira ya afya duniani. Tunashindwaje kuwa na makubaliano ya kufanya kazi pamoja katika kutekeleza sera yetu?". amehoji Waziri Gwajima.

Waziri Gwajima ameongeza kuwa kuna watu huwa wanaanzisha ajenda ambazo kimsingi Wizara inakua haina haja nazo huku akitoa onyo kwa watumishi wa Wizara ya Afya kutoandaa vikao ambavyo ajenda zake zinakua siyo za kueleweka kimkakati na kisera.

Aidha, Waziri Gwajima pamoja na kuahidi ushirikiano wa kutosha kwa Katibu Mkuu na Mganga Mkuu wa Serikali mteule, ameagiza wakurugenzi wa idara zilizopo Wizarani kutengeneza vikao vya mashirikiano ili kuwezesha mnyororo wa kutoa huduma za afya kufanyika kwa uweledi na kuepusha malalamiko kutoka kwa wananchi.

Naye Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel amesema ushirikiano baina ya viongozi mbalimbali wa Wizara pamoja na taasisi zake ni chachu kubwa ya kuleta mabadiliko ya kiutendaji na kuongeza kuwa viongozi hao wote ni washauri wa Mhe. Waziri wakiwa na lengo la kuboresha huduma za afya nchini.

Kwa upande wake Katibu Mkuu Prof. Abel Makubi amesema ana imani kubwa kuwa wataalamu waliopo katika Sekta ya Afya wanaweza kufanya kazi nzuri katika kusimamia afya za Watanzania na kuweza kutimiza matarajio ya Rais. Lakini pia Prof. Makubi amewashukuru watumishi wa afya kwa kazi kubwa na hakusita kuomba ushirikiano kutoka kwao ili kuweza kuitekeleza sera ya afya ambayo iliandaliwa na Wizara.

Vilevile Mganga Mkuu wa Serikali Dkt. Aifello Sichwale akitoa shukrani zake mbele ya Waziri Gwajima amebainisha maeneo yake kadhaa ya utendaji ili kuboresha sekta ya afya.

Ametaja  maeneo hayo ni Uongozi, Uwajibikaji na Utawala bora. Eneo la pili ni kuhusu masuala ya fedha, eneo la tatu ni kuhusu bidhaa za afya, nne ni Rasilimali Watu, tano ni Masuala ya TEHAMA, sita ni Huduma kwa Mteja, saba ni kuhusu masuala ya utafiti na la nane ni kuhusu ushirikiano na Sekta Binafsi.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Dorothy Gwajima akiongea na kutoa maelekezo kadhaa kwa watumishi wa Wizara hiyo wakati wa hafla ya kuwapokea viongozi wapya jijini Dodoma.
 

Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Prof. Abel Makubi akitoa neno la shukrani kwa watumishi wa Wizara ya Afya (Hawapo pichani) wakati akipokelewa katika Wizara hiyo Jijini Dodoma.

Mganga Mkuu wa Serikali Dkt. Aifello Sichalwe akiongea mbele ya Watumishi wa Wizara ya Afya katika ukumbi mdogo wa Wizara uliopo Area D jijini Dodoma.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Dkt. Abel Makubi akipokea kadi ya kumtakia heri katika majukumu yake mapya kutoka kwa Waziri Dkt. Gwajima na Naibu Waziri Dkt. Mollel katika hafla ya mapokezi jijini Dodoma.
 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...