Charles James, Michuzi TV
WAZIRI wa Maji, Jumaa Aweso amemuagiza Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Mhandisi Anthony Sanga kuhakikisha anawalipa wachimbaji wote wa visima na watafiti ambao wanaidai Serikali.
Waziri Aweso ametoa agizo hilo jijini Dodoma leo wakati akizungumza na wachimbaji na watafiti wa maji katika warsha iliyoandaliwa baina ya Waziri wa Maji na wachimbaji hao kuhusu miongozo ya utafiti na uchimbaji visima.
Akizungumza katika warsha hiyo, Waziri Aweso amemtaka Katibu Mkuu Mhandisi Sanga kuwalipa wachimbaji hao fedha wanazodai huku akisisitiza pia wawe wanapewa fursa za kuchimba visima badala ya kuitumia Wakala wa Uchimbaji ambao kila mwaka wamekua wakishindwa kutimiza malengo ya visima ambavyo Wizara imekua ikipanga.
" Hawa wachimbaji na watafiti ni wadau wetu wakubwa wa katika Wizara yetu, haiwezekani Wizara mwaka jana ilikua na mpango wa kujenga visima 542 lakini vilivyochimbwa hata 150 havifiki, hii maana yake Wakala wa Uchimbaji hamuwezi kufanya peke yenu washirikisheni hawa wadau.
Mfano mwaka huu tuna Mpango wa kuchimba visima zaidi ya 1,000 niwaambie tu Wakala wa Uchimbaji toeni fursa kwa hawa wachimbaji, haiwezekani mnachimba kisima mwezi mzima bila sababu ya msingi, wapeni hawa wachimbaji muone kama hawatochimba kwa siku Moja," Amesema Waziri Aweso.
Amewaahidi wachimbaji hao kushughulikia changamoto zinazowakabili ikiwemo hiyo ya kuhakikisha wanalipwa madeni yao ya nyuma huku akiwataka kujenga umoja wao utakaowawezesha kuweza kuwasilisha changamoto zao Wizarani kwa haraka.
Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga amesema amepokea maelekezo ya Waziri juu ya kulipwa kwa wachimbaji hao ambapo amewataka kuwasilisha nyaraka zao ili waweze kulipwa.
" Niwaombe kabla hamjaondoka hapa Dodoma mlete nyaraka zenu ili tuweze kuwalipa stahiki zenu kabla ya kumalizika kwa mwezi Juni, niwaahidi ushirikiano wa hali na Mali na pamoja tuungane kumaliza changamoto ya Maji nchini," Amesema Mhandisi Sanga.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...