Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Sportpesa, Abbas Tarimba (katikati) akimkabidhi mfano wa hundi yenye thamani ya shilingi milioni 50, Afisa Mtendaji Mkuu wa Simba SC, Barbara Gonzalez huku wakishuhudiwa na Wachezaji wa Simba SC, David Kameta (Duchu), Gadiel Michael na Ame Ibrahim  zilizotolewa na Kampuni ya Michezo ya Kubahatisha ya Sportesa kama bonasi kwa Simba SC baada ya kufika Robo Fainali ya Michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu.

Na Bakari Madjeshi, Michuzi TV

Klabu ya Simba imekabidhiwa kitita cha Shilingi Milioni 50 (50,000,000/-) na Kampuni ya Michezo ya Kubahatisha ya Sportpesa kama bonasi baada ya Klabu hiyo kufika Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu wa 2020-2021, bonasi hilo ni makubaliano baina ya Simba SC na Kampuni hiyo pale timu inapofanya vizuri katika Mashindano mbalimbali.

Akizungumza na Waandishi wa Habari wakati wa makabidhiano ya mfano wa hundi jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Sportpesa, Abbas Tarimba amesema wanajivunia kwa Klabu ya Simba kufanya vizuri katika Soka la Tanzania na Kimataifa na kutambua mchango wao wa kuendeleza Soka nchini.

Tarimba amesema tangu kuingia mkataba na timu mbalimbali za Ligi Kuu Soka Tanzania Bara, Sportpesa imekuwa ikitoa bonasi hilo kwa Simba SC pekee ikiwa sambamba na kutoa Milioni 100 katika misimu mitatu ambayo Simba SC imetangazwa kuwa Mabingwa wa VPL.

“Tunawapa Simba SC kiasi cha Shilingi Milioni 50 baada ya kufika Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, isingekuwa kufungwa na Kaizer Chiefs basi leo tungekuwa tunazungumzia Simba SC kufika Nusu Fainali ya Michuano hiyo mikubwa barani Afrika ya CAF CL”, amesema Tarimba.

Pia, Tarimba amesema wapo kwenye mazungumzo ya kuongeza mkataba na Simba SC ili kuendelea kuidhamini Klabu hiyo kwa kipindi kingine.


Kwa upande wake, Afisa Mtendaji Mkuu wa Simba SC, Barbara Gonzalez amesema wanajivunia udhamini wa Sportpesa na kuwapa faraja kufanya vizuri zaidi katika Michuano ya ndani na Kimataifa pia kuwajenga zaidi kama Klabu.


Barbara amesema wapo kwenye mazungumzo na Kampuni hiyo ili kuongeza mkataba wa udhamini, amesema wangependa    kuongezeka zaidi bonasi zinazotolewa kutokana na thamani ya Klabu na Wachezaji kwa ujumla na hata kukua kwa Ligi ya Tanzania.


Naye, Mchezaji wa Simba SC, Gadiel Michael amezungumza kwa niaba ya Wachezaji wengine, amesema wanaona faraja kupata bonasi hilo la Milioni 50 za Kitanzania, Gadiel ameeleza kuwa inawapa hamasa kama Wachezaji wa Simba SC kuendelea kupambana na kufanya vizuri katika Michuano mbalimbali.
Afisa Mtendaji Mkuu wa Simba SC, Barbara Gonzalez akizungumza wakati Klabu hiyo ikikabidhiwa bonasi la Shilingi Milioni 50 kutoka Kampuni ya Michezo ya Kubahatisha ya Sportpesa.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Sportpesa, Abbas Tarimba (katikati) akizungumza na Waandishi wa Habari, kulia ni Afisa Mtendaji Mkuu wa Simba SC, Barbara Gonzalez na kushoto ni Mchezaji wa Simba SC, Gadiel Michael.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...