Na John Nditi, Morogoro
WIZARA ya Mifugo na Uvuvi imekitaka Chama cha Wafugaji Tanzania kujishughulisha zaidi katika maendeleo na mafaniko ya biashara ya mifugo kwa wafugaji wote bila kubagua kwa vile si chama cha kisiasa wala cha kiharakati.

Katibu mkuu Mifugo , Profesa Elisante Ole Gabriel alisema hayo mjini Morogoro kwenye hotuba yake kufugua kikao kazi cha kupitia na kujadili rasimu ya mwongozo wa kupatikanaji , upimaji, uendelezaji na usimamizi wa maeneo ya malisho na maji kwa mifugo nchini.

Katibu mkuu Mifugo alisema , kutokana na kuwepo kwa mifugo ya aina tofauti , kinapaswa kuwa cha wafugaji wote si wa ng’ombe pekee , kwa kuanza kutoa huduma za kuwasaidia kuinua uchumi wao wafugaji wengi wakiwemo wanaofunga hata kuku ili kijijengee uhalali wa kuitwa jina hilo.

Profesa Ole Gabriel alisema , wizara kupitia waziri inatamani kusiwepo na migogoro ya aina yoyote baina ya wafugaji na watumiaji wengine wa ardhi.

Alisema , jambo hilo linaweza kufanikiwa endapo Chama cha Wafugaji kwa kushirikiana na wataalamu kuendesha zoezi la kuwaelewesha wafugaji kuhusu uchumi wa sekta ya malisho kwa ajili ya kuimalisha mifugo yao.

“ Hatupendi kuwa na uchungaji bali ni ufugaji na hilo linawezekana endapo wafugaji wanaeleweshwa umuhimu wa kuunganishwa na minyororo mitano ya biashara itakayozingatiwa ikiwemo mnyororo wa thamani ya mifugo , gharama za ufugaji ,kuingiza mapato nje ya ufugaji na kuangalia mtaji wake “ alisema Profesa Ole Gabriel.

Pamoja na hayo alisema ,ongezeko la idadi ya watu na mifugo iliyopo linasababisha uhitaji mkubwa wa maeneo ya malisho na uhitaji wa nyama na maziwa kama lishe .

Kwa mujibu wa Katibu mkuu Mifugo , takwimu za sasa zinaonesha kwamba idadi ya mifugo iliyopo nchini ni takribani ng’ombe milioni 33.4 , mbuzi milioni 21.29 , kondoo milioni 5.65 na punda wapatao 657,389 .

Hata hivyo alisema , vijiji vingi bado havijaanda mipango ya matumizi ya ardhi , na takwimu za Tume ya Mipango na Matumizi ya Ardhi zinaonesha kuwa idadi ni ndogo kwa vijiji vilivyoandaa mipango hiyo ambapo ni takribani asilimia 13.4 ya vijiji vyoye nchini.

“ Nimatumaini yangu kwamba iwapo vijiji vyote vilivyopo hapa nchini vingeandaa mipango ya matumizi ya ardhi maeneo mengi zaidi ya ufugaji yangeweza kupatikana “ alisema Profesa Ole Gabriel .

Katibu mkuu Mifugo alitumia fursa hiyo kuelekeza vijiji visivyokuwa na mpango wa matumizi kupanga mpango huo, na kutenga maeneo ya malisho kwenye vijiji vyao ili kuhakikisha tunafikia lengo la hekta milioni sita za maeneo ya malisho ifikapo mwaka 2025.

Alisema , kwa vile utengaji wa maeneo ya malisho unahusisha Mamlaka mbalimbali na wadau tofauti , ni vyema kupitia majukumu yaliyoainishwa kwenye mwongozo huo ni kuhakikisha kuwa kila mmoja wetu anatekeleza majukumu yake.

Profesa Ole Gabriel alisema lengo ni kuleta tija kwa uzalishaji wa mifugo na kuleta mabadiliko ya maisha ya wafugaji na mifugo yao nchini.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Idara ya Uendelezaji wa Maeneo ya Malisho na Rasilimali za Vyakula vya Mifugo , Dk Asimwe Rwiguza, kabla ya kumkaribisha Katibu mkuu , alisema licha ya kuwepo ngo’ombe zaidi ya milioni 33 .4 bado eneo la malisho ni madogo .

Dk Rwiguza alisema,katika mwaka unaomalizika eneo la malisho ni hekta milioni 2.8 zilizotajwa na Tume ya Mipango na Matumizi ya Ardhi, na hata hivyo licha ya kutokabidhiwa rasmi baadhi yamevamiwa kwa shughuli zingine tofauti na ufugaji na itaathitri uboreshaji wa mifugo na mazao yake.

Naye Mfugaji na Msimamizi wa Mradi wa Ujamaa Community Resource Team (UCRT),kutoka Simanjiro, Edward Loure aliipongeza wizara na Idara hiyo kwa kuamua kuwashirikisha kujadili na kuboresha mwongozo huo ambao baada ya kupitishwa utasimamiwa na kutekelezeka na wafugaji kutokana wao kuwa ni miongoni mwa washiriki.

Loure kwa niaba ya wezake ,alitumia fursa kumpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuunga mkono kwa kauli yake aliyowataka wafanye ufugaji wenye kuleta tija wao wenyewe na taifa kwa ili kukuza uchumi kupitia sekta ya mifugo.

Katibu mkuu wa wizara ya Mifugo na Uvuvi , Profesa Elisante Ole Gabriel anayesimamia Mifugo (aliyeketi kati kati ) akiwa kwenye picha ya pamoja na wadau wa kikao kazi cha kupitia na kujadili rasimu ya mwongozo wa upatikanaji , upimaji, uendelezaji na usimamizi wa maeneo ya malisho na maji kwa mifugo nchini baada ya kufugua kikao hicho mjini Morogoro.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...