Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Dkt.Samuel Gwamaka, amepiga marufuku uanzishwaji wa madampo kiholela katika makorongo bila ya kufanyiwa Tathmini ya Athari kwa Mazingira.
Ameyasema hayo alipofanya ziara ya kushtukizia katika dampo lisilo rasmi lililopo maeneo ya Goba, Mtaa wa Amani, kata ya Mbezi juu, Manispaa ya Kinondoni Jijini Dar es Salaam, dampo hilo linatumika kutupwa taka kutoka maeneo mbalimbali ya Manispaa za Kinondoni na Ubungo na kupelekea malalamiko mengi kutoka kwa wakazi walio karibu na eneo hilo kwani dampo hilo lipo Katika mpaka wa Manispaa ya Ubungo na Manispaa ya Kinondoni.
Aidha Dkt. Gwamaka amesema kuwa kwa kawaida unapotaka kuanzisha dampo liwe dogo au kubwa Manispaa husika inatakiwa kufanya Tathmini ya Athari kwa mazingira kwa kuwashirikisha wadau wote wataalam kutoka Wizara mbalimbali pamoja na wakazi walio karibu na eneo hilo ili kuepusha migogoro isiyo ya lazaima
"Dampo hili limeridhiwa na Manispaa ya Kinondoni lakini kwa mujibu wa sheria ya Mazingira ya 2004, inasema unapotaka kuanzisha dampo sehemu yoyote ni lazima ifanyikeTathimini ya Athari kwa Mazingira lakini Manispaa ya Kinondoni hawakufanya hivyo ambayo ni kosa kisheria na napiga faini ya shilingi million tano kwa Manispaa hii kutokana na kuvunja sheria" alisema Dkt. Gwamaka
Ameendelea kusema kuwa hii iwe fundisho kwa Manispaa zote Nchini kuacha mara moja kuanzisha madampo kiholela hasa kwenye makorongo bila ya kufanya Tathmini ya Athari kwa Mazingira kujua kama eneo hilo ni rafiki kwa kufanya shughuli hizo bila ya kuathiri mazingira yetu
Kwa upande wake Esther Green mkazi wa eneo hilo, amesema kuwa kwa upande wake kutupwa taka katika korongo hilo linafaida kubwa kwani taka hizo zinasaidia kuzuia mmomonyoko na nyumba zao kutoathirika.
Ameendelea kusema kuwa japo kwake anaona faida lakini bado kuna baadhi ya wakazi hasa upande wa wakazi waliopo Manispaa ya Ubungo hawakubaliani na utupwaji wa taka hizo kwani zinaleta nzi na harufu mbaya hivyo kusababisha migogoro baina yao
Aidha Dkt. Gwamaka amemalizia kwa kusema kuwa migogoro hiyo isingetokea kama manispaa husika ingeweza kufanya Tathmini ya Athari kwa Mazingira kwani ingefanyika ingeweza kubaini changamoto zote kabla ya utupaji taka kuanzishwa katika eneo hilo. Ameendelea kusema kuwa kufanya Tathmini sio kwa ajili ya kuepusha migogoro tu bali hata kuzingatia usalama wa viumbe hai , binadamu, mimea na wanyama ambao wanahitaji kuishi. Dkt Gwamaka amesema hayupo tayari kuona mtu yeyote anavunja sheria na kuona maisha ya watu kuwa hatarini kwa uzembe wa watu wachache.
1. Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Muhandisi Dkt. Samuel Gwamaka, akiwa katika dampo lisilo rasmi maeneo ya Goba wilaya ya Kinondoni Jijini Dar es Salaam kujionea hali halisi katika eneo hilo ambalo linalalamikiwa na baadhi ya Wananchi
Mkurugenzi
Mkuu wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Muhandisi
Dkt. Samuel Gwamaka, akitoa ufafanuzi juu ya ziara yake katika dampo hilo
lisilo rasmi lililopo maeneo ya Goba kata ya Mbezi Juu jijini Dar es Salaam.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...