Charles James, Michuzi TV
ELIMU ELIMU ELIMU! Hiki ndicho kipaumbele cha Mkuu wa Mkoa mpya wa Dodoma, Anthony Mtaka ambapo amesema iwe kwa kupenda au kutopenda lazima watoto wa Mkoa wa Dodoma wasome.
Mtaka ameitoa kauli hiyo leo jijini Dodoma wakati akikabidhiwa ofisi na aliyekua Mkuu wa Mkoa huo, Dk Binilith Mahenge.
Akizungumza na Viongozi mbalimbali wa Mkoa wa Dodoma, RC Mtaka amesema ni jambo la aibu kuona Shule ya Kwanza kwenye Mkoa huo inakua ya 101.
" Haiwezekani Shule ya Kwanza Simiyu inaingia 20 bora kitaifa halafu ya Kwanza hapa Dodoma inakua ya 101, ni lazima Wakurugenzi wa Halmashauri zote na Maafisa Elimu mtambue kipaumbele changu ni elimu, naamini katika Taifa lenye wasomi wengi katika kufikia mafanikio na ili Taifa lifanikiwe inabidi sisi huku chini tuanze.
Inatupasa kuandaa kizazi kipya cha Makao Makuu, kizazi chenye wasomi watakaoendana na hadhi ya Mkoa, wananchi watake wasitake watoto watasoma tu," Amesema Mtaka.
Ametoa wito kwa viongozi wote kuanzia Mkoani, Wilayani na Halmashauri kuwa wanyenyekevu na siyo kutumia nafasi na vyeo walivyonavyo kuumiza wengine.
" Mimi naamini katika 'team work' siyo jeshi la mtu mmoja hivyo kwa pamoja tukishirikiana tunaweza kuifanya Dodoma kuwa Mkoa wenye mafanikio makubwa kulingana na hadhi yake.
Tusifanye kazi kwa mihemko siyo mtu DC unanyanyua mabega kijana wa Chuo anakuletea wazo la kimaendeleo hata humsikilizi, unakuta mtu DC anatembea na walinzi kibao wa kazi gani Sasa? Mimi nshamwambia msaidizi wangu kibao cha namba za RC au bendera kupepea kwenye gari yangu sitaki, nataka niwe kama nilivyo," Amesema Mtaka.
Amemuomba Mkuu wa Mkoa mpya wa Singida, Dk Binilith Mahenge kushirikiana katika mazao ya kimkakati kwa mikoa hiyo miwili ikiwemo Alizeti na Zabibu.
Amesema watahakikisha wanapambana kulifanya zao la Alizeti kuwa zao la kibiashara ili kufanya lilimwe kwa wingi na kuondoa changamoto ya mafuta nchini ambayo imekua ikijitokeza.
Ametoa wito kwa kila kiongozi kwenye Mkoa kufanya kazi kwa kuzingatia kanuni na sheria za kazi huku akiwasihi kuwa wabunifu na wenye fikra chanya kulingana na mabadiliko ya kiteknolojia duniani.
Aliyekua Mkuu wa Mkoa wa Dodoma ambaye amehamishiwa Singida, Dk Binilith Mahenge akizungumza wakati wa kumkabidhi ofisi Mkuu mpya wa Mkoa wa Dodoma, Anthony Mtaka.
Mkuu mpya wa Mkoa, Anthony Mtaka (mwenye shati jeupe) akiwa na aliyekua Mkuu wa Mkoa huo, Dk Binilith Mahenge ambaye amehamishia Singida wakiwa katika picha ya pamoja na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa pamoja na Wakuu wa Wilaya za Dodoma baada ya Wakuu hao kukabidhiana ofisi.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...