Na Mwandishi, Wetu
WAFANYAKAZI wa Benki ya I&M Tanzania wamejitolea msaada wa vitu mbalimbali vikiwemo vyakula, nguo, sabuni pamoja na vifaa vya shule katika moja ya kituo cha kulea watoto yatima kiitwacho ‘Lady Fatema’ kilichopo Mjimwema Mageti Saba wilayani Kigamboni jijini Dar es salaam.
Wametoa msaada huo chini ya mpango wao wa ‘IM FOR YOU’ katika jitihada za kurudisha kwa jamii kupitia mpango huo ambapo wafanyakazi hujitolea kwa jamii kwa njia mbalimbali kama vile kutoa elimu ya fedha na ujasiriamali kwa wanawake na vijana ili waweze kujiajiri pamoja na kusaidia vitu mbalimbali kwa wahitaji.
Msaada huo umekabidhiwa leo Mei 11 mwaka 2021 kwa Wasimaizi wa kituo hicho Mariam Ramadhan na mmewe Kalekela Omari Mahmood walianzisha kituo hicho mwaka 2011 wakiwa na lengo la kusaidia watoto yatima wanaoishi katika mazingira hatarishi wakiwapatia elimu, chakula na hifadhi ya kulala.
Mbali na misaada mbalimbali inayopelekwa na wafadhili, kituo hicho kina changamoto ya eneo la kutosha kwa ajili ya kuhifadhi watoto wengi na wa jinsia tofauti kwani kwa sasa imewalazimu kubaki na jinsia ya kiume tu kutokana na ukosefu wa vyumba vya kutosha kwaajili ya watoto hao.
Katika kuadhimisha mwezi mtukufu wa Ramadhani na ikiwa ni wiki ya kuelekea sikukuu ya Eid Al-Fitr, wafanyakazi wa benki ya I&M waliamua kujitolea vitu hivyo katika kituo cha kulea watoto yatima Mjimwema Kigamboni ili na wao waweze kusheherekea na kufurahia sikukuu ya EID inayotarajiwa kuwa mwishoni mwa wiki hii kutegemeana na kuandama kwa mwezi.
Pia wafanyakazi wa benki ya I&M wametoa elimu ya usimamizi wa fedha na ujasiriamali kwa vijana na wanawake waliokuwa katika kituo hicho ili iweze kuwasaidia katika usimamizi wa fedha za kituo hicho pamoja na kujiajiri wao wenyewe pindi watakapoanza kujitegemea.
Benki ya I&M kupitia wafanyakazi wake wameweza kufanya kampeni mbalimbali za kusaidia jamii kama vile kujitolea kwa kufundisha wanawake, vijana na wajasiriamali katika kikundi cha Wanawake wajasiriami kilichopo Yombo vituka, Temeke jijini Dar es salaam, vilevile wiki iliyopita wafanyakazi wa benki hiyo walijitolea damu ili kusaidia wagonjwa wenye uhitaji wa damu katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...