Na Bakari Madjeshi, Michuzi TV

TIMU ya Wataalam wa Jiosayansi kutoka Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) imetoa matokeo ya uchunguzi wa athari ya Volcano tope iliyotokea katika Mtaa wa Makoka, Kata ya Makuburi Wilayani Ubungo, mkoani Dar es Salaam baada ya eneo hilo kukumbwa na athari hiyo ya tope linalotoka ardhini.

Wataalamu hao wa Jiosayansi kutoka GST walianza uchunguzi huo jana June 4, 2021 baada ya Wananchi na Wakazi wa eneo hilo kubaini kuwepo athari hiyo ambayo ni tishio kwao na ingeweza kuleta madhara makubwa.

Akizungumza na Waandishi wa Habari katika eneo hilo, Mjiolojia Mwandamizi kutoka GST, Gabriel Mbogoni amesema baada ya uchunguzi huo timu hiyo imegundua kuwa ni majanga asili ambayo yanatokea kwenye matabaka ya miamba (liquefaction) hususani kwenye matabaka ya udongo.

“Kwenye tabaka la udongo, kuna chembechembe za udongo ambazo zinakuwa zimeshikana lakini katikati kuna nafasi kwa kawaida nafasi hiyo inakuwa na maji, maji na chembechembe za udongo huwa zinawiana, zile chembechembe zinakuwa zinagusana na kusigana hivyo kunakuwa na ukinzani, wakati mwingine shughuli mbalimbali za binadamu, milipuko husababisha kuleta athari hizo za Volcano tope.”Amesema Mbogoni.

Amesema kutokana na hali hiyo maeneo hayo hayawezi kuwa rafiki kwa binadamu, Wanyama kutokana na kuzama kwenye tope hilo na hata majengo kutitia, amewaasa Wananchi kuchukua tahadhari kutokana na majanga hayo ya asili kutotabirika mara kwa mara.

Naye, Mjumbe Msaidizi wa Mtaa huo, George Joseph amesema baada ya kuona tope hilo walichukua hatua kwa kutoa taarifa Ofisi za Serikali ya Mtaa kupitia kwa Mtendaji, amesema walishirikiana na Mtendaji huyo sambamba na DAWASCO ili kubaini kama kuna uvujifu wa bomba la maji katika eneo hilo.

“Eneo hili litaleta madhara mengi sio tu kuzama kwa watu lakini litakuwa tishio kwa wapita njia, kutokana na kuwa njia kubwa ya watu wa Makoka katika kufanya shughuli kama za mazishi kutokana na uwepo wa Makabari eneo la kule juu, pia italeta changamoto kwa wananchi wenyewe wanaotumia njia hiyo kwa shughuli za kawaida za kila siku.” Ameeleza Mjumbe Joseph.

Mkazi wa eneo hilo, ambaye Nyumba yake kwa kiasi kikubwa ipo eneo hilo la athari, Charles Mtweve amesema athari hiyo imeanza kuonekana mwaka mmoja uliopita yakiwemo madhara ya kuzama kwa watu wanaotumia njia hiyo, amesema mara nyingi athari hiyo inaonekana kipindi cha Mvua.

Athari kama hiyo ya Volcano tope imewahi kutokea katika Mikoa ya Dodoma eneo la Chemba,Manispaa ya Shinyanga, Wananchi wa maeneo mbalimbali wameaswa kuchukua tahadhari juu ya athari kama hizo, pindi inapotokea athari kama hiyo wameaswa kujaza mawe eneo husika sambamba na kutengeneza mifereji ili kuruhusu maji kuondoka.
Mmoja wa Wataalamu kutoka GST akipima urefu wa kina cha tope la Volcano lilitokea Mtaa wa Makoka, Kata ya Makuburi, Dar es Saalam.
Mjiolojia Mwandamizi kutoka GST, Gabriel Mbogoni akieleza chanzo cha athari ya Volcano tope ilitokea katika Mtaa wa Makoka, Kata ya Makuburi Wilayani Ubungo mkoani Dar es Saalam.

Tope

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...