KATIBU Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Daniel Chongolo ameagiza kuanzia sasa Baraza Kuu la Umoja wa Wanawake wa Chama cha Mapinduzi (UWT) liwe na agenda ya kudumu ya matumizi ya fedha asilimia 4 za wanawake zinazotolewa katika Halmashauri.

Ametaka Baraza hilo lijue Nchi nzima fedha kiasi gani zimetengwa, zimetolewa kwa kina mama wangapi kwani anazotaarifa  kuna baadhi ya viongozi wamekuwa wakijinufaisha na fedha hizo.

Akizungumza  leo June 26,2021 wakati akifungua Baraza Kuu la UWT Taifa,Katibu Mkuu huyo amesema matarajio ya chama ni kuona viongozi wanakuwa na agenda zenye mashiko katika jamii huku akihoji ni kwanini Baraza la mwaka huu halina agenda ya matumizi ya fedha asilimia 4 zinazotolewa katika Halmashauri.

“Kuanzia sasa agenda ya kudumu ya Baraza kuu la Jumuiya  iwe matumizi ya fedha asilimia 4 za wanawake zinazotolewa katika halmashauri.Tujue nchi nzima fedha kiasi gani zimetengwa,zimetolewa kwa  akina mama wangapi na kina mama wangapi  wamenufaika sababu kina mama wengine ndio kina sie wengine wanatengeneza miradi ya kuwanufaisha ninyi,sisi kama chama hatupo tayari hili litokee,”amesema.

Amesema Baraza hilo ndio furum ya kuwazungumzia wanawake kuhusiana na fedha hizo ambapo amedai Halmashauri ya Kinondoni pekee imetenga shilingi bilioni 4 ambapo amehoji ni kwanini mwanamke alalamike suala la mtaji.

“Kwa sababu hii ndio forum ya kutengeneza mfumo sahihi msiwaache kina mama wenzetu mimi nimetoka Kinondoni mwaka huu wametenga bilioni 4 kwanini wanawake walalamike changamoto ya mitaji,”amesema.

Vilevile,amewataka Wabunge wanaotokana na UWT kuzisimamia na kuwa na taarifa ya asilimia 4 ya fedha zinazotolewa katika Halmashauri kwamba  zinawanufaisha wanawake.

VIKAO

Aidha,Katibu Mkuu huyo ameitaka UWT  kutumia vikao kuwasaidia wanawake na sio kuvitumia kusengenyana na mambo  yao binafsi.

Amesema kwa sasa ukiona idadi ya wajumbe kwenye vikao imekamilika ujue kuna mtu anataka kushughulikiwa ambapo amedai jambo hilo sio zuri.

“Uhai wa chama ni vikao ni muhimu kwani ndio sehemu ya kujadili mambo yetu na uzoefu unaonesha vikao vyetu vingi vinakosa tija.Nasema kwa sababu tumekuwa na vikao kuanzia kamati ya utekelezaji,baraza kuu na vikao vingine  vya juu muda mwingi sana katika vikao hivi ukiona ‘Colum’ imetimia  na wajumbe wamefika ujue kuna mtu wanataka kumshughulikia.

“Vikao hivi vinafanyika ndani ya Jumuiya katika chama ambacho kimepewa nafasi ya kuongoza Nchi na kazi ya kuongoza Nchi sio kazi ya lelemama alisema Mwalimu Nyerere(Rais wa kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania) na sisi ndio tunatoa kazi ya uongozi sisi ni lazima tuwe mwarobaini wa kule tunapotoka.

“Kuna kina mama kila eneo sasa wanatakiwa wakuone wewe kama daraja vikao ndio vinatakiwa kuwa sehemu mahasusi sisi tumebahatika kuwemo katika vikao.Sisi tunawajibu wa kuheshimu msihangaike na mambo ya watu hangaikeni na mambo ya maendeleo UWT isiwe kwenda kujadili huyu mrefu ama mfupi jadilini mambo ya maendeleo tuwe ni viongozi ambao tunajitengenezea daraja uongozi usiwe ni kujadili sisi kwa sisi tujadili inshu,”amesema.

YEYE NI MKALI

Katibu huyo amesema yeye ni mgeni machoni mwa watu lakini anauzoefu wa zaidi ya miaka 20 na ameingia katika vikao muhimu vya chama hicho ambapo amedai yeye atasimamia taratibu ili kujenga maadili ndani ya chama.

“Niwaambie ninavyoongea nacheka hivi lakini mimi ni bingwa wa kusimamia taratibu ni lazima tujenge maadili kwenye chama chetu na lazima tusimamie hili na tuheshimu kwa dhati.

“Mimi ni Katibu Mkuu mpya ila mwenye kwao wanamjua niseme kweli mimi ni mgeni machoni mwa wengi lakini huu ukumbi nimeingia zaidi ya miaka 20 na nimebahatika kweli kuwa kijana mdogo ambaye nimeingia   katika vikao muhimu vya Sekretarieti,Kamati Kuu,Maadili Taifa wakati ule nilikuwa Afsa lakini nimekuja kuwa Mkuu wa Maafsa,”amesema.

KUONEKANA WAKATI WA UCHAGUZI TU

Katibu Mkuu huyo amesema wanawake ni jeshi kubwa lakini limekuwa likionekana wakati wa uchaguzi tu hivyo amelitaka kujitokeza wakati wote kukipambania chama.

“Wanawake ni Jeshi kubwa lakini halionekani katika shughuli za kawaida ninyi mmekuwa Jeshi kubwa wakati wa uchaguzi tu jambo hili sio sawa Jeshi  kubwa ni lile linalofanya kazi kubwa wakati wa Amani na kuongoza mapambano.

“Na sisi wakati wa kawaida ndio wakati wa kuimarika na kuhamasisha na kuusimamia na uhai ili wakati wa pambano Jeshi letu litusaidie.Mwakani kuanzia  Februari  tunaanza uchaguzi na hicho ndio kipimo cha kuona kwamba ninyi ni jeshi kubwa na maana nyingine,”amesema.

ASIKITISHWA NA MATENDO YAO

Amesema licha ya wanawake kuwa ni jeshi kubwa lakini baadhi wamekuwa wakifanya matendo ambayo sio mazuri.

“Wanawake ni Jeshi kubwa lakini baadhi yenu wanawaangusha Jeshi hili hasa kwa vitendo vyao na matendo yao na hivi karibuni tumeona mambo ya aibu yanafanyika ni maeneo mengi hayatujengei sura nzuri yanachafua sura yetu.

“Nikuhakikishie sisi ni wakali na tutaendelea kuwa wakali mtu yeyote akifikia kwamba anauwezo wa kufanya mambo yake ya hovyo na sisi tukamchekea na kumwangalia sio wakati huu.Ukiwa kiongozi lazima uwe unajiheshimu na unajua majukumu yako,”amesema.

WANAOJIPANGA

Katibu Mkuu huyo pia amesema wale wanaojipanga na kujipitisha kugombea nafasi mbalimbali wanatakiwa kuachwa kwani hakuna mahali panaporuhusu utaratibu huo mbovu.

“Mimi niwaombe mkisikia dalili watu wanaojipanga katika nafasi muwaache hata UWT hakuna mahali panaporuhusu utaratibu huu na utaratibu huu ni wa hovyo na hautusaidii kupata viongozi wazuri.

“Nimeona niliseme hilo kwa sababu moja ya sifa ya vikao vyetu mara nyingi hutumikia kupanga safu na hutumika kutengeneza makundi badala ya kutengeneza umoja hutumika kutengeneza miundombinu ya kujiwekaweka mahali fulani ili ukubalike badala ya kutengeneza miundombinu ya chama chetu kiheshimike,”amesema.

KWENDA KWENYE MASHINA

Amesema ndani ya chama wamefanya mapitio na kugundua wameteleza kwenye kusimamia misingi kuanzia ngazi ya shina.

Amesema wameanza kwenda katika mashina kuwahamasisha wananchi kwani ndiko wanakopatikana.

 



Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi CCM, Daniel Chongolo akihutubia Baraza Kuu la Umoja wa Wanawake wa CCM (UWT) Katika Ukumbi wa Makao Makuu ya Chama hicho jijini Dodoma leo.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...