Charles James, Michuzi TV
KATIKA kuimarisha mfumo wa elimu nchini, Serikali imesema itaendelea kushirikiana na wadau wa sekta ya elimu katika kuboresha mfumo huo ikiwemo mitaala lengo likiwa ni kuzalisha vijana wenye ubora katika kujiletea maendeleo na Taifa kwa ujumla.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kongamano la elimu lililoandaliwa na Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia kupitia Taasisi yake ya Elimu, Naibu Waziri wa Elimu, Omary Kipanga amesema serikali imelenga kuhakikisha vijana nchini wanakua ni wenye maarifa, ujuzi na stadi.
Kongamano hilo limefanyika leo jijini Dodoma ukiwa ni mkutano wa pili wa wadau wa elimu wenye lengo la kukusanya maoni kuhusu uboreshaji wa mitaala ya elimu ngazi ya awali, msingi na sekondari.
Naibu Waziri Kipanga ameiagiza Bodi ya Taasisi ya Elimu Tanzania kufuatilia kwa karibu na kuyafanyia kazi maoni yote yatakayotolewa na wadau hao kwa lengo la kujenga na kuboresha zaidi mitaala hiyo.
" Niwahakikishia wadau wa elimu kuwa Serikali itaendelea kufanya kazi nanyi kwa karibu ili kuzidi kuimarisha mfumo wa elimu yetu na kuhakikisha vijana wa Kitanzania wanapata maarifa, ujuzi na stadi za kazi stahiki.
Nimtumie fursa hii kuwahimiza Bodi ya Elimu Tanzania kuhakikisha inafuatilia kwa karibu maoni ya wadau na kuyafanyia kazi kikamilifu na kwa umakini mkubwa ili tuweze kufanikiwa katika uboreshaji mitaala hii,” Amesema Naibu Waziri Kipanga.
Ametoa wito kwa washiriki wote wa kongamano hilo kutumia taaluma na nafasi zao kutoa maoni yao ili kuijenga sekta ya elimu ambayo kimsingi ndio uti wa mgongo wa maendeleo yoyote katika Nchi.
Akizungumzia kongamano hilo, Katibu Mkuu Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia, Dk Leonard Akwilapo amewapongeza wadau wote walioitikia wito wa kushiriki mkutano huo ambapo anaamini maoni ya kila mmoja yatakua sehemu ya uboreshaji wa mitaala hiyo.
Dk Akwilapo amesema kwa wadau ambao wameshindwa kufika Dodoma kushiriki mkutano huo bado wana fursa ya kushiriki kutoa maoni yao kupitia fomu zinazopatikana kwenye tovuti ya Taasisi ya Elimu Tanzania (www.tie.go.tz) au namba ya simu 0735041169.
Nae Mkurugenzi Mkuu wa TET, Dk. Aneth Komba amesema wanatarajia kuwa wadau watapata uelewa wa pamoja kuhusu maboresho ya mitaala hiyo ili watoe maoni yenye tija kwa elimu yetu nchini.
“Na imani kuwa tutapata maoni mengi yatakayoboresha Elimu yetu nchini,hivyo tushirikiane kuhakikisha tunafanikisha ubora wa elimu yetu kwa watoto ambao ni viongozi wajao wa taifa hili,” Amesema Dk Komba.
Naibu Waziri Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia, Omary Kipanga akihutubia mamia ya wadau wa elimu waliohudhuria mkutano wa pili wa kujadili uboreshaji wa mitaala ngazi ya awali, msingi na sekondari.
Katibu Mkuu Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia, Dk Leonard Akwilapo akizungumza wakati wa mkutano wa pili wa wadau wa elimu kujadili uboreshaji wa mitaala ngazi ya awali, msingi na sekondari.
Wadau mbalimbali wa elimu wakifuatilia mkutano wa pili wa wadau wa elimu jijini Dodoma wenye lengo la kujadili uboreshaji wa mitaala ya elimu kuanzia ngazi ya awali, msingi na sekondari.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...