Na Said Mwishehe,Michuzi TV
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika kufungua Maonesho ya 45 ya Biashara ya Kimataifa yanayofanyika kila mwaka katika viwanja vya Mwalimu Nyerere' Sabasaba wilayani ya Temeke mkoani Dar es Salaam.
Waziri wa Viwanda na Biashara Profesa Kitila Mkumbo amewaeleza waandishi wa habari kuwa Rais Samia atakuwa mgeni rasmi kwenye ufunguzi wa maonesho hayo Julai 5 mwaka huu."Ni heshima kubwa kwa Rais kukubali kuwa mgeni rasmi katika maonesho haya, hii itakuwa mara yake ya kwanza kuja kuyafungua tangu aliposhika wadhifa wa Urais wa nchi yetu".
Aidha Prof.Mkumbo aamewaomba wananchi wa kujitokeza kwa wingi ili kuja kumuunga mkono Rais Samia Suluhu Hassan kwa kupata fursa ya kutembelea Maonyesho haya ya 45 .Maonesho yameanza Juni 28 mwaka huu lakini Julai 5 ndio utakuwa ufunguzi rasmi, hivyo Rais atakuwa viwanja vya Sabasaba saa nane mchana.
Kuhusu maandalizi ya maonesho hayo Profesa Mkumbo amesema maandalizi yamekamilika na kila kitu kipo sawa, huku akieleza kila mwaka maonesho hayo yanakuwa na kauli mbiu yake na kauli mbiu ya mwaka huu inasema hivi " Uchumi wa viwanda kwa ajira na biashara endelevu".
Ameongeza kwamba jumla ya washiriki ni 3002 na wamethibitisha kushiriki.Kati ya hao nchi saba za kigeni,kutakuwa na kampuni 76 huku akifafanua ushiriki mwaka huu ni mkubwa ikilinganishwa na mwaka jana hasa katika ongzeko la kampuni za kigeni.
"Katika kuandaa maonyesho hayo kuna taasisi mbalimbali zimewezesha kuyafanikisha na kutakuwa na mikutano mbalimbali itakayoshirikisha kampuni za nje na ndani ili kutafuta fursa za biashara,"amesema Profesa Mkumbo.
Amesema kuwa mikutano hiyo itafanyika ana kwa ana na mingine kwa njia ya mitandao na kwamba kutakuwa na uzinduzi wa nembo maalumu ya viungo vya chakula ambavyo vinazalishwa nchini na utakaofanyika Julai 9,2021.
Profesa Mkumbo amesema kutakuwa na uzinduzi wa mfumo wa taarifa za biashara ambao utaongeza uwazi wa tatatibu za biashara kimataifa ambapo utaongeza wigo wa taarifa za biashara na kutakuwa na uzinduzi wa Duka la kimtandao kwa ushirikiano wa Tantrade na Shirika la Posta.(Mobile Shop) na mambo mengine.
Aidha kutakuwa na uzinduzi wa kutambua mabanda ya washiriki wa ndani ya uwanja kwa maonyesho hayo ambapo kumeandaliwa ramani."Pamoja na yote hayo tunaomba wananchi kuendelea kuchukua tahadhali za kujinga na janga la Corona.Viingilio kwa mtoto ni Sh.1000 na wakubwa Sh.3000 na siku yenyewe ya sabasaba kiingilio kitakuwa Sh.4000.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...