MKUU wa Mkoa wa Ruvuma
Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge ameanza kukutana na makundi mbalimbali,kundi la
kwanza kupata fursa hiyo ni wazee wa Mji wa Songea ambao wamewawakilisha wazee
wa Mkoa wa Ruvuma.
RC Ibuge amezungumza na
kusikiliza kero mbalimbali za wazee katika kikao kilichofanyika Ikulu Ndogo
mjini Songea kikihusisha wazee wa makundi yote wakiwemo wazee wa Baraza la
Makumbusho ya Majimaji,viongozi wa madhehebu mbalimbali ya dini na Kamati ya
Ulinzi na Usalama Mkoa wa Ruvuma.
Kabla ya kufanya
majumuisho,Mkuu wa Mkoa alitoa fursa kwa wazee kutoa maoni yao na kueleza
changamoto mbalimbali zinazowakabili wazee na wananchi wa Mkoa wa Ruvuma kwa
jumla.
Mzee Ismail Nyingo ambaye ni Mjumbe wa Baraza la Wazee wa Makumbusho
ya Majimaji,Mchungaji Adimu Mwezegule wa makanisa ya Pentekoste na Tito
Mbilinyi, Mwenyekiti wa wafanyabiashara Mkoa wa Ruvuma walizungumzia changamoto
ya Kituo Kikuu cha mabasi cha Songea kilichopo Kata ya Tanga.
Walisema licha ya
kwamba Kituo hicho ni cha kisasa,changamoto kubwa ni abiria wanapofika kutoka
nje ya Songea wanapata kero ya mawasiliano ya simu na daladala majira ya usiku
hivyo kuingia gharama kubwa ya kukodi taksi hadi mjini Songea.
“Tunaomba kwa usiku
mabasi yanapofika stendi ya Tanga kuruhusu kubeba abiria hadi mjini kwa sababu wananchi wanaangaika
sana’’,alisema Mchungaji Mwezegule.
Mzee John Nyoni
Mwenyekiti wa Baraza Huru la Wazee Manispaa ya Songea alimwomba Mkuu wa Mkoa
kusaidia kutatua changamoto zinazowakabili wazee zikiwemo Bima ya afya kwa
wazee,pensheni na kuomba Sera ya wazee itungiwe Sheria kwa sababu ipo muda
mrefu.
Mayasa Mfaume ni Katibu
wa Waganga wa Jadi aliomba kutatuliwa changamoto zinazowakabili waganga wa jadi
alidai kwamba hivi sasa hakuna mfumo kamili wa kuwatambua waganga wa jadi na
kuwapatia vibali.
Sponsioza Katambala
amemuomba Mkuu wa Mkoa kukutana na mabaraza ya wazee mara kwa mara ili wazee
hao waweze kuibua mambo mengi yanayohusu wazee na wananchi kwa ujumla.
Mzee Gerold Haule
amemuomba Mkuu wa Mkoa kushughulikia pembejeo kwa wakulima ambapo amesema Mkoa
umekuwa unazalisha kwa wingi mazao ya chakula kwa kutumia mbolea hivyo
upatikanaji ukiwa rahisi uzalishaji unaweza kuongezeka zaidi.
Mzee Adolf Kumbukuru
amezungumzia changamoto ya uharibifu wa mazingira katika Mto Ruvuma ambao upo
kwenye tishio kubwa kukauka kutokana na shughuli za kibinadamu.Ameomba Mto huo kuhifadhiwa ili kuulinda.
Akizungumza baada ya
kusikiliza changamoto za wazee,Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma amesema wazee ni hazina
kubwa ndiyo maana ameamua kuwa kundi la kwanza kuzungumza nao baada ya
kuteuliwa na Rais Samia Suluhu Hassan kuwa Mkuu wa mkoa.
RC Ibuge ameahidi
atazifanyia kazi changamoto hizo,ikiwemo stendi ya mabasi ya Tanga ambayo
amesema atafuatilia kwa sababu serikali imetumia zaidi ya shilingi bilioni sita
kuwekeza na kwamba ataangalia namna bora ya kukabiliana na changamoto za stendi
hiyo bila kuathiri stendi.
Amesema changamoto zote
atazifuatilia na kuzitolea majibu katika kikao kingine ambacho atapanga tena
kukutana na wazee ambapo ametoa rai kwa wazee kuendelea kushirikiana na
serikali ili kuwaletea maendeleo wananchi wa Mkoa wa Ruvuma.
Akizungumzia mfumo wa
stakabadhi ghalani katika mazao ya ufuta na soya,Mkuu wa Mkoa amesema mahitaji
ya soko kupitia mfumo huo ni makubwa hasa nje ya nchi na kwamba changamoto za mfumo
huo ni ndogo kwa kuwa mkulima anapata faida kubwa zaidi.
“Kinachofanya maendeleo
yasitokee popote ni watu wachache wenye maslahi binafsi ambao wanapotosha,mfumo
wa stakabadhi ghalani tangu umeanza kutumika mkoani Ruvuma mwaka 2018,umekuwa
na manufaa makubwa kwa wakulima’’,alisisitiza RC Ibuge.
Mkuu wa Mkoa pia
amesisitiza suala la amani kuwa ni moja ya vipaumbele vyake,ambapo amesema anataka
kuona katika Mkoa wa Ruvuma,kila mtanzania anakuwa salama na kushiriki ipasavyo
bila woga katika uzalishaji mali.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...