Charles James, Michuzi TV
MSIWE LIMBUKENI! Ni kauli ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Anthony Mtaka hii leo alipokua akiwaapisha Wakuu wapya wa Wilaya za Kongwa na Kondoa, ambapo amewataka kuepuka Balehe za Madaraka ili waweze kutekeleza majukumu yao kikatiba na kisheria.
RC Mtaka amesema kama zilivyo hatua za ukuaji wa binadamu hata kwenye uongozi pia zipo hivyo ni vyema kama viongozi walioaminiwa na Rais kuepuka kunyanyua mabega na kuwa limbukeni wa madaraka kwani kufanya hivyo ni kujichimbia wenyewe kaburi lao la uongozi.
Wakuu wapya waliopisha ni Remedius Emmanuel ambaye ameteuliwa kuwa DC wa Wilaya ya Kongwa na Dk Khamis Mkanachi ambaye yeye ameteuliwa kuwa DC wa Wilaya ya Kondoa.
Akizungumza baada ya kuwaapisha Wakuu hao, RC Mtaka amewaasa kufanya kazi zenye matokeo chanya kwa wananchi na Taifa kwa ujumla ili Viongozi Wakuu wa Nchi watakapoenda kwenye Wilaya zao wapongeze juhudi walizozionesha na siyo wanakua viongozi ambao wakiondoka kwenye maeneo yao ya kazi wanakua hawajaacha alama.
" Mnapaswa kujua nyie ni Wakuu wa Wilaya na siyo wasaidizi wa Mkuu wa Mkoa, Rais Samia amewaahidi kwenye nafasi zenu, nendeni mkafanye kazi kwa kubeba matarajio aliyonayo kwenu lakini pia mkatimize azma yake ya kuwaletea watanzania maendeleo.
Kuna kasumba ya viongozi wengi kuathiriwa na Balehe ya Madaraka, kama zilivyo hatua za ukuaji wa binadamu hata kwenye uongozi ipo, epukeni Balehe za uongozi ili muweze kuwatumikia watanzania kwenye maeneo yenu kwa haki," Amesema RC Mtaka.
Amewataka kufanya kazi kwa bidii wakiinua elimu kwenye maeneo yao ili kuzalisha Vijana wengi wa Makao Makuu ya Nchi wenye uwezo wa kushindana kwenye soko la ajira na biashara kwa kuwa wamepatiwa elimu bora.
" Nitajisikia faraja kuona wakuu wangu wa Wilaya akili yao inatumika kwa maslahi ya Taifa letu na inaleta matokeo chanya, siyo muwe vituko hadi mtu aone kusema huyu ni DC wangu au huyu DC ni rafiki yangu," Amesema Mtaka.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kongwa, Remedius Emmanuel amemhakikishia RC Mtaka kufanya kazi kwa ushirikiano huku akiziishi ndoto za Rais Samia Suluhu Hassan za kuwaletea maendeleo wananchi wa Kongwa.
" Namshukuru Mungu kwa siku ya leo, namshukuru pia Rais Samia kwa kuniamini katika uteuzi huu na kuwa miongoni mwa Vijana wachache wanaomsaidia kazi katika Serikali yake, niahidi ushirikiano, utii na uadilifu katika kazi yangu hii ya Ukuu wa Wilaya.
Ninajua vipaumbele vya Mkoa wetu na kwa kupitia Ilani ya Uchaguzi ya CCM nitakwenda kusimamia utekelezaji wake ili kuona azma ya Serikali ya kuwaletea maendeleo watanzania na zaidi wananchi wa Kongwa inatimia," Amesema DC Remedius.
Kwa upande wake DC Mkanachi ameahidi kusimamia vipaumbele vya Mkoa wa Dodoma kwenye elimu, kilimo kwa nguvu ambapo pia ameahidi ushirikiano kwa Viongozi wa ngazi zote, makundi ya kijamii na viongozi wa Dini pamoja na wananchi wote.
Uapisho huo pia umehudhuriwa na Wakuu wengine wa Wilaya za Dodoma ambao tayari walikuepo kwenye nafasi zao lakini wakahamishwa vituo vya Kazi na wengine wakibaki katika vituo vyao vile vile vya kazi.
Mkuu wa Wilaya ya Kondoa, Khamis Mkanachi akila kiapo cha kutumikia nafasi yake mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Anthony Mtaka.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Anthony Mtaka akizungumza baada ya kuwaapisha Wakuu wa Wilaya za Kongwa na Kondoa Leo jijini Dodoma.
Mkuu wa Wilaya ya Kongwa Mpya, Remedius Emmanuel akizungumza mara baada ya kuapishwa leo jijini Dodoma na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Anthony Mtaka.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...