Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi) Dk Rashid Tamatamah (katikati) akionesha eneo ambalo yatajengwa mabwawa ya samaki wazazi kwenye kituo cha Ukuzaji Viumbe Maji kilichopo eneo la Rubambagwe, Chato mkoani Geita ambako alifika hapo kwa ajili ya kukagua hatua za ujenzi wake. wengine pichani ni Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara, Doto James (kushoto) na Mkuu wa Wilaya Chato, Charles Kabeho (kulia.)
Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Dkt. Rashid Tamatamah (kulia), Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara, Doto James (katikati) na Afisa Uvuvi Mfawidhi kanda ya Ziwa, Bilali Banali (kushoto) wakiwa kwenye ukaguzi wa hatua za ujenzi wa miundombinu mbalimbali iliyopo kwenye kituo cha Ukuzaji Viumbe Maji kilichopo eneo la Rubambagwe, Chato mkoani Geita.
Mshauri Elekezi wa mradi wa kituo cha Ukuzaji  Viumbe Maji uliopo eneo la Rubambagwe, Chato mkoani Geita kutoka Wakala ya Majengo nchini (TBA) Mhandisi Fredrick Jackson (kulia) akiwaonesha picha ya namna moja ya majengo katika eneo hilo litakavyokuwa katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi) Dk Rashid Tamatamah na Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara, Doto James wakati viongozi hao walipofika hapo kwa ajili ya kukagua hatua za ujenzi wake. Kushoto ni Afisa Uvuvi Mfawidhi kanda ya Ziwa, Bilali Banali.




SERIKALI kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi) imesema kuwa ifikapo mwezi Septemba mwaka huu itakuwa imekamilisha ujenzi wa kituo kikubwa cha ukuzaji viumbe maji kilichopo eneo la Rubambagwe, Chato mkoani Geita.

Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi) Dk Rashid Tamatamah mara baada ya kukagua  ujenzi wa kituo hicho uliofikia asilimia 50 hadi hivi sasa ambao utagharimu kiasi cha zaidi ya shilingi Bilioni 3 mpaka kukamilika kwake.

“Huu mradi wote unajumuisha ujenzi wa mabwawa 9 ambapo 6 yatakuwa ni kwa ajili ya samaki wazazi na 3 ya  kukuzia vifaranga hao lakini pia utakuwa na majengo 8 ambayo ni pamoja na jengo la kutotoleshea samaki, jengo la utawala ambalo ndani yake kutakuwa na mashamba darasa, nyumba za watumishi na jengo la elimu ya utengenezaji wa chakula cha samaki” Amesema Dk Tamatamah.

Dk Tamatamah amesema kuwa Kukamilika kwa kituo hicho kutaongeza uzalishaji wa vifaranga vya samaki hapa nchini ambapo kinatarajiwa kuzalisha  vifaranga zaidi ya milioni 20 kwa mwaka ikiwa ni ongezeko maradufu zaidi ya idadi inayozalishwa na vituo vinne vya Serikali vinavyojishughulisha na ukuzaji viumbe maji hivi sasa ambavyo kwa mujibu wa takwimu za hadi mwezi Aprili mwaka huu vimezalisha  jumla ya vifaranga milioni 3 pekee.

“Mradi huu ulianza wakati wa Serikali ya awamu ya tano hivyo nimshukuru Rais wetu Samia Suluhu Hassan kwa kuruhusu fedha iliyopangwa kwa ajili ya mradi huu iendelee kuukamilisha hadi mwisho, pia nawashukuru sana TBA kwa kuusimamia vizuri mradi huu na kuhakikisha unakuwa na viwango stahiki na mwisho nawashukuru viongozi wa Wilaya ya Chato na wananchi wote kwa namna wanavyoendelea kutoa ushirikiano wa karibu katika kuhakikishia mradi huu unakamilika kwa mafanikio” Amesema Dk Tamatamah.

Naye Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara, Doto James amesema kuwa mradi huo utakuwa na manufaa makubwa kwa wananchi wote kwa ujumla hasa kwa upande wa viwanda vya kuchakata samaki kwa sababu utasaidia ongezeko la uzalishaji wa samaki wa kutosha.

“Binafsi ninahusika moja kwa moja na matunda yatokanayo na mradi huu kwa sababu sisi upande wa viwanda tunahitaji samaki wa kutosha ili kuweza kuwa na uhakika wa kuchakata minofu ya samaki hasa hawa wanaotokana na tasnia ya ufugaji kwenye mabwawa lakini pia wingi wa samaki watakaozalishwa hapa  utachochea biashara ya bidhaa hii ndani na nje ya nchi” amesema James.

James amemuomba Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi) Dk  Rashid Tamatamah kuendelea kuanzisha miradi ya aina hiyo katika maeneo yote yenye uhitaji wa vituo vya kukuzia viumbe maji  kwa sababu mahitaji ya samaki na vifaranga wake yanaongezeka kadri siku zinavyozidi kwenda.

“Lakini pia namkaribisha Dk Tamatamah, Wizara ya Viwanda na Biashara kwa miradi mingine yote ambayo itazihusu sekta zetu na ile ya Uvuvi” Ameongeza James.

Akibainisha namna ambavyo Wilaya ya Chato itanufaika na mradi huo, Mkuu wa Wilaya hiyo Charles Kabeho amesema kuwa kituo hicho kitawapa fursa wananchi wake kujifunza teknolojia mbalimbali za ufugaji bora wa samaki na utengenezaji wa miundombinu ya ufugaji wa samaki.

“Lakini vile vile mradi huu utatengeneza ajira kwa wananchi wa Chato kwa sababu watatengeneza fursa mbalimbali za kiuchumi zitakazotokana na uwepo wa kituo hiki kikubwa kabisa ikiwa ni pamoja na kuwarahisishia upatikanaji wa vifaranga kwa wale ambalo watajikita kwenye shughuli za ufugaji wa samaki” Amesema kabeho.

Kabeho amemuahidi Dk Tamatamah kuendelea kutoa ushirikiano kwa Wizara yake mpaka mradi huo utakapokamilika.

Kwa upande wake Meneja wa Wakala ya Majengo nchini (TBA) mkoa wa Geita Gladys Jefta mbali na kuishukuru Wizara kwa kuwaamini na kuwapa kazi ya kusimamia mradi huo amemhakikishia Dkt. Tamatamah kuwa watausimamia mradi huo kwa ubunifu mkubwa ili uweze kukamilika ukiwa na viwango vinavyoendana na fedha itakayotumika.

“Ninapenda kutoa rai kwa mkandarasi wetu ambaye ni vikosi vya ujenzi kutoka Wizara ya Ujenzi kukamilisha mradi huu kwa muda ambao tumekubaliana ili kuipa fursa Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuanza kutekeleza malengo ya kituo hiki”  Amesema Jefta.

Mara baada ya kukamilika kwake, kituo hiki kikubwa zaidi hapa nchini kitajumuisha utoaji wa elimu ya ukuzaji viumbe maji kwa wananchi  wote hatua ambayo inatarajia kukuza zaidi tasnia hiyo na kuifanya nchi kuzalisha samaki kwa wingi kupitia ufugaji wa  kwenye mabwawa.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...