Waziri wa Nishati Mhe. Dkt. Medard Kalemani akikata utepe kuzindua Mradi Kabambe wa Kusambaza Umeme vijijini Awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili Katika mkoa wa Mtwara.



Waziri wa Nishati Mhe. Dkt. Medard Kalemani akifurahia pamoja na viongozi mbalimbali wa Chama na Serikali pamoja na viongozi kutoka Wizara ya Nishati, REA naTANESCO. mara baada ya kukata utepe ikiwa ni ishara ya kuzindua Mradi Kabambe wa Kusambaza Umeme vijijini Awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili Katika mkoa wa Mtwara.



Waziri Kalemani akiwatambulisha kwa wananchi na viongozi wa Mkoa wa Mtwara, Wakandarasi watakaosambaza umeme katika vijiji vya Mkoa wa Mtwara vilivyosalia kuunganishiwa umeme ambao ni Namis Corporate Engineers and Contractors ambaye atatekeleza Mradi katika Wilaya za Masasi na Nanyumbu wakati Central Electricals International atatekeleza Mradi katika wilaya za Mtwara, Newala na Tandahimba na kuwataka Wakandarasi hao, TANESCO na REA kufungua ofisi kijijini Namtumbuka ili kuwapatia huduma za umeme wanakijiji hao kwa urahisi.



Waziri wa Nishati Mhe. Dkt. Medard Kalemani akionesha kifaa cha UMETA kwa wanakijiji cha Namtumbuka, kata ya Namtumbuka, Halmashauri ya mji wa Nanyamba, Wilaya ya Mtwara, mkoani Mtwara ambapo uzinduzi wa Mradi Kabambe wa Kusambaza Umeme vijijini Awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili Katika mkoa wa Mtwara. tarehe 19 Juni, 2021.

……………………………………………………………..

Na Dorina G. Makaya – MTWARA

Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Medard Kalemani amesema, Serikali imetenga shilingi bilioni 62.146 kuvipelekea umeme vijiji 384 vilivyosalia kuunganishiwa umeme mkoani Mtwara ndani ya miezi 18 kuanzia tarehe 20 Juni, 2021.

Waziri Kalemani ameyasema hayo leo tarehe 19 Juni, 2021 alipokuwa akifanya uzinduzi wa Mradi Kabambe wa Kusambaza Umeme vijijini Awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili Katika mkoa wa Mtwara uliofanyika katika kijiji cha Namtumbuka, kilichopo kata ya Namtumbuka, Halmashauri ya mji wa Nanyamba, Wilaya ya Mtwara, mkoani Mtwara.

Dkt. Kalemani amesema, kati ya vijiji 797 vilivyopo mkoani Mtwara, vijiji 413 tayari vimepatiwa umeme na vijiji vilivyosalia 384 vitapatiwa umeme katika Mradi huu ndani ya miezi 18 na hivyo kuweka historia ya mafanikio katika kutekeleza Miradi ya kusambaza Umeme Vijijini.

Amesema, Itakapofika Disemba 2022, Tanzania itaandika historia katika vitabu vyake kuwa vijiji vyote vya Tanzania Bara vimepata umeme na kuungana na mataifa mengine duniani yaliyoendelea ambayo yameshaandika historia hii.

Waziri Kalemani amesema, hadi sasa, zaidi ya vijiji 10,312 vimeshapelekewa umeme na vilivyobakia takribani vijiji 1,956 ndivyo vinapelekewa umeme katika mradi huu.

Amesema Serikali imetenga takribani shilingi bilioni 10.3 kwa ajili ya kuvifikishia umeme vijiji vyote 58 vilivyosalia katika Wilaya ya Mtwara, kikiwemo kijiji cha Namtumbuka.

Dkt. Kalemani amewaasa wananchi wa Mtwara watandaze nyaya kwenye nyumba zao na kulipia shilingi 27,000/= tu ili waweze kuunganishiwa umeme na kwa wale wenye nyumba ndogo zisizozidi vyumba vitatu, wanaweza kutumia kifaa cha UMETA ambacho hakihitaji kutandaza nyaya katika nyumba.

Aidha Waziri Kalemani amesisitiza kuwa, kwa wananchi ambao watakuwa na upungufu wa fedha za kulipia kwa mkupuo, wanaweza kulipia kidogo kidogo na watakapokamilisha malipo yao wanaweza kuunganishiwa umeme katika kipindi ambacho Mkandarasi yupo katika eneo la Mradi.

Dkt. Kalemani amewataka wananchi wa kijiji cha Namtumbuka na wananchi wote kiujumla ambapo Mradi wa kupeleka Umeme vijijini unafanyika, watumie fursa ya kupatikana kwa umeme katika kuendeleza na kukuza shughuli zao za kiuchumi ikiwemo kilimo, ufugaji na uvuvi.

Amewaasa wananchi wote kutunza nguzo na kuonya kuwa, hatua kali za kisheria zitachukuliwa kwa yeyote atakayebainika kuharibu miundombinu ya umeme.

Pia, Waziri Kalemani amewatambulisha kwa wananchi na viongozi wa Mkoa wa Mtwara, Wakandarasi watakaosambaza umeme katika vijiji vya Mkoa wa Mtwara vilivyosalia kuunganishiwa umeme ambao ni Namis Corporate Engineers and Contractors ambaye atatekeleza Mradi katika Wilaya za Masasi na Nanyumbu wakati Central Electricals International atatekeleza Mradi katika wilaya za Mtwara, Newala na Tandahimba na kuwataka Wakandarasi hao, TANESCO na REA kufungua ofisi kijijini Namtumbuka ili kuwapatia huduma za umeme wanakijiji hao kwa urahisi.

Aidha Dkt. Kalemani amemuagiza Mkandarasi atakayeunganisha umeme kijijini Namtumbuka, kukamilisha kazi hiyo ndani ya wiki tatu na kuahidi kurejea kijijini hapo kuwasha umeme ndani ya muda huo.

Vile vile, Waziri Kalemani amempongeza Kaimu Mkurugenzi Mkuu REA, Mha. Jones Olotu kwa kazi nzuri anayoifanya ambayo imepelekea mafanikio makubwa katika kazi ya kupeleka umeme vijijini hapa nchini.

Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mtwara wakati wa hafla hiyo ya uzinduzi wa Mradi Kabambe wa Kusambaza Umeme vijijini Awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili Katika mkoa wa Mtwara, Mkuu wa Wilaya ya Mtwara, Mhe. Dunstan Kyobya amesema, mbali ya kuwa umeme ni fursa nzuri katika kuleta maendeleo ya kiuchumi, lakini kwa mkoa wa Mtwara, umeme ni muhimu sana katika suala la ulinzi na usalama kwa maeneo mengi ya mipakani hususan kata za Namtumbuka, Mnongodi, Milangominne, Kitaya, Kiyanga, Kiromba, Mahurunga, Tangazo, Madimba, Msimbati na kwenye maeneo ya vyombo vya ulinzi na usalama.

Mhe. Kyobya Amesema, kupatikana kwa umeme katika vijiji vilivyobakia ambavyo vilikuwa bado havijaunganishiwa umeme, ni fursa kwa wanamtwara hasa wakulima wa zao la Korosho na ufuta, kuutumia umeme utakaopatikana katika kuongeza thamani kwenye mazao yao kwa kujenga viwanga vidogo vidogo.

Aidha Mkuu huyo wa Wilaya ya Mtwara ameongeza kuwa, kupatikana kwa umeme kutachochea upatikanaji wa mawasiliano ya simu na kuwa chanzo cha mapato kwa wananchi.

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini (REA) Wakili Julius Bundala Kalolo amesema, atahakikisha fedha iliyotengwa na Serikali inatumika ipasavyo kwa kuhakikisha Nishati ya umeme inasambazwa kwenye vijiji vyote vilivyosalia ambavyo bado havijaunganishiwa umeme.

Wakizungumza kwa nyakati mbalimbali, wakati wa hafla hiyo, mbunge wa Nanyamba Mhe. Abdallah Chikota, Mbunge wa Tandahimba Mhe. Katani Katani, Mbunge wa Mtwara mjini Mhe. Hassan Mtenga, Mbunge wa Ndanda Mhe. Cecil Mwambe, na Mbunge wa Lulindi Mhe. Issa Mchungahela wameipongeza na kuishukuru Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, kwa kutenga fedha na kupeleka umeme katika vijiji vilivyokuwa bado havijaunganishiwa umeme mkoani Mtwara, hatua itakayochochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii mkoani humo.

Katika ziara hiyo, Waziri wa Nishati Mhe. Dkt. Medard Kalemani, aliambatana na wataalamu kutoka Wizara ya Nishati, TANESCO na REA na ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Chama na Serikali wa Wilaya na Mkoa wa Mtwara.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...