WAKATI huu ambapo dunia inakabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi, ipo haja dhana ya utunzaji shirikishi wa vyanzo vya maji ikapewa kipaumbele ili kuokoa rasilimali hiyo muhimu kwa maisha ya binadamu.
Kauli hiyo imetolewa hivi karibuni na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji Wilaya ya Kilosa, Cheyo Nkelege wakati wa uzinduzi wa Ofisi ya Jumuiya ya Watumia Maji katika Kijiji cha Msowero, ambapo ujenzi wake umesimamiwa na Bodi ya Maji Bonde la Wami Ruvu.
Aidha, sambamba na mabadiliko ya tabianchi yanayotajwa kuhatarisha uhai wa rasilimali maji, changamoto nyingine inayotajwa ni ongezeko la shughuli za kibinadamu kwenye vyanzo hivyo, zinazosababisha hali ya uchafuzi wa mazingira.
Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti Bodi ya Maji Bonde la Wami Ruvu, Norah Mambya ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Maji Bonde la Wami Ruvi, alisema dhamira ya ujenzi wa ofisi ya Jumuiya ya watumaji maji katika eneo hilo utasidia ulinzi na uhifadhi endelevu wa rasilimali maji.
Kwa upande wao baadhi ya wananchi wa Kijiji cha Msowero, wameelezea namna Jumuiya za Watumia maji zinavyosaidia kutunza na kulinda vyanzo vya maji katika eneo hilo.
Katika hatua nyingine, imeelezwa kuwa mradi wa ujenzi wa Ofisi ya Jumuiya ya Watumia Maji Katika Bonde Dogo la TAMI/MSOWERO wilayani Kilosa hadi kukamilika umegharimu kiasi cha Shilingi Milioni 72.
Wana Jumuiya ya Watumia maji katika Bonde dogo la Tami/Msowero wakiwa katika picha ya pamoja na Viongozi wa Bodi ya Maji Bonde la Wami Ruvu,mara Baada ya kukamilika kwa hafla ya Uzinduzi wa Ofisi za Jumuiya hiyo katika Kijiji cha Msowero Wilayani Kilosa.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...