Na Amiri Kilagalila,Njombe
Sekretarieti
ya Chama cha Mapinduzi CCM mkoa wa Njombe imewatahadharisha wanachama
wa Chama hicho pamoja na viongozi kwa kushindwa kulipa kadi zao za
uanachama kwa wakati huku wengine wakisubiri nyakati za uchaguzi na
kuanza kulipia.
Katibu wa
Chama cha mapinduzi (CCM) mkoa wa Njombe Bi,Amina Imbo amesema
wanachama wengi hususani wanaohitaji kugombea nafasi za uongozi ndani ya
Chama hicho wamekuwa wakijitokeza kulipia kadi zao hususani katika
wakati huo ili chama kiwape nafasi za kugombea nafasi.
Ameyasema
hayo wilayani Makete mkoani Njombe wakati akitoa semina ya uimarishaji
wa uchumi wa Chama na jumuiya zake katika ziara ya Sekretarieti ya Chama
mkoa inayozunguka halmashauri 6 za mkoa huo kwa ajili ya kukagua uhai
wa Chama na jumuiya zake,kukagua utekelezaji wa Ilani (miradi mbali
mbali ya Maendeleo) pamoja na utekekelezaji wa maagizo mbali mbali
kutoka ngazi ya juu ya Chama.
Bi
Amina amepiga marufuku utaratibu huo na kuagiza kila mwanachama kulipia
kadi yake ya shilingi 100 kwa mwezi na kwa wakati ili kuendelea
kuimarisha uhai wa Chama kwa kuwa pia uhai wa mwanachama hutegemea na
ulipiaji wa kadi kwa wakati kwa kuwa chama hicho kimekuwa na wanachama
wengi wasio hai.
"Tutaenda
kwenye kompyuta na kuangalia uhai wako kwa kulipa ada yako ya kila
mwezi bila limbikizo iwe kwa mwezi,miezi mitatu,mitano au hata mwaka na
ndio itakuwa sababu ya anayetaka kugombea uongozi kumpa kipaumbele
katika nafasi"alisema Amina Imbo
Aidha
ameagiza viongozi wote wa CCM kuweka mikakati mizuri ya uingizaji wa
wanachama wapya kwa kuwa chama hicho mkoa wa Njombe kina wanachama Laki
moja na stini pekee wakati taifa limeelekeza angalau mkoa kuwa na
wanachama zaidi ya laki tano hatua inayopelekea mkoa wa Njombe kuwa
katika nafasi mbaya kwenye takwimu za idadi ya wanachama.
Katibu
wa UWT mkoa wa Njombe Bi,Frola Kapalie ametoa rai kwa wanachama
kuongeza nguvu katika ulipiaji ada ya uanachama kwa kuwa mfumo wa sasa
umekuwa ukionyesha taarifa za kila mwanachama.
“Tujitafakari na kuhakikisha tumelipia kadi kwa kuwa viongozi wanatazama kwa karibu mwenendo wa uanachama wetu"alisema Frola
Kwa
upande wake Katibu wa siasa na uenezi mkoa wa Njombe Erasto Ngole
ameagiza viongozi kuandaa na kufanya vikao vya uongozi kila wakati ili
kujiimarisha na kupeleka ajenda za vikao na maendeleo ya Chama kwa
wanachama
"Mkikaa na
kukubaliana baadhi ya ajenda kwa utaratibu na makatibu kata wakaandika
vizuri taarifa za vikao tunaamini vikao hivyo vitakuwa halali na sio vya
majungu na Chama kitakuwa vizuri na kwa utaratibu"alisema Ngole
Wilbath Mwalyoyo na Matrida
Msigwa ni baadhi ya wanachama na viongozi wa CCM katika ngazi za kata
wilayani humo walioshiriki katika semina hiyo,wameshukuru kutembelewa na
viongozi hao na kukumbushwa namna ulipaji wa ada pamoja na uingizwaji
wa wanachama wapya ndani ya Chama hicho.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...