Diwani wa kata ya Milo Robert Njavike akiongea na wananchi wa kata hiyo katika mkutano wa hadhara wa kusikiliza changamoto mbalimbali.
Viongozi pamoja na wananchi wa kata ya Milo wakiwa katika mkutano wa kujadili changamoto mbalimbali zinazoikabili kata hiyo.

Na Shukrani Kawogo, Njombe

WANANCHI wa kata ya Milo wilayani Ludewa mkoani Njombe wamewaomba viongozi wa kata hiyo kuwawekea chombo maalum kitakacho wasimamia na kuwatetea wakulima pindi wanapouza mazao yao.

Ombi hilo wamelitoa katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika kijiji cha  Mapogolo ulioandaliwa na diwani wa kata hiyo Robert Njavike sambamba na viongozi wa  vijiji na serikali wa kata hiyo kwa lengo la kusikiliza kero mbalimbali za wananchi hao.

Wananchi hao wamedai kuwa wafanyabiashara wamekuwa wanawanyonya wanapokuja kununua mazao yao na kufunga lumbesa kitu ambacho kinawapa hasara.

Enelly Haule ni miongoni mwa wananchi hao amesema kuwa wamekuwa wakitumia gharama nyingi katika kilimo lakini wanapokuja kuuza mazao hayo wafanyabiashara wamekuwa wakitaka kuuziwa mazao kwa ujazo wa lumbesa.

"Viongozi wetu wa kata tunaomba sana mtusaidie kutuundia chombo kitakachokuwa kinatusimamia katika kutenda haki katika uuzaji wa mazao yetu kwani wafanyabiashara wamekuwa wakitupangia ujazo wa mazao hasa viazi pasipo kujali gharama tulizotumia", Alisema Haule.

Sambamba na suala hilo la lumbesa pia wananchi hao wameomba kuondolewa kodi kwa wakulima wanaotumia maji ya bonde la ziwa nyasa kwenye mto kigina.

Akiwasilisha ombi hilo Jackson Mgimba amesema wanaimba wapewe uhuru wa kutumia maji hayo bila kuwepo kizuizi hicho cha kodi.

Aidha kwa upande wa mtendaji wa kata hiyo Kilian Mtitu amesema kuwa wakulima wenyewe wanapaswa kuwa na umoja katika kupinga kipimo hicho cha lumbesa kwani endapo watashirikiana wafanyabiashara watalazimika kununua kwa kipimo cha kawaida huku akiahidi kulifanyia kazi suala kuunda chombo hicho cha kuwasimamia.

Pia katika suala la Watumiaji wa vyanzo vya maji kwenye mto kigina amesema kuwa utaratibu wa mabonde yote tisa nchini likiwemo bonde la ziwa nyasa ambao unawataka watumiaji wa vyanzo hivyo kuwa na kibali maalum. 

Ameongeza kuwa sheria hiyo siyo katika mabonde tu bali hata katika maji ya mvua ambapo mtu anapokinga maji yanayozidi lita 20 anatakiwa awe na kibali maalum.

Katika mkutano huo ziliwasilishwa changamoto nyingi ikiwemo suala la umeme, maji, barabara na nyinginezo na kupatiwa majibu.

Naye diwani wa kata hiyo Robert Njavike amesema kuwa changamoto nyingi zinazowakabili wananchi wake anazifuatilia kwa karibu sana katika kuzitafutia ufumbuzi huku akimpongeza mbunge wa jimbo la Ludewa Joseph Kamonga kwa kuonyesha ushirikiano wa kutosha katika kuzisemea kero zao.

Amesema mbunge huyo amekuwa akiwakutanisha madiwani mbalimbali na wakuu wa idara husika ikiwemo mawaziri ili kuwasilisha kero mbalimbali zilizopo katika kata zao.

"Mbunge wetu alituandalia ziara ya kutembelea bungeni madiwani wote na akatukutanisha na mawaziri mbalimbali akiwemo waziri wa maji Juma Aweso na waziri wa nishati Bernard Kalemani", Alisema Njavike.

Aliongeza kuwa kutokana na changamoto ya umeme na maji Katika kata yake alitumia fursa hiyo kuwasilisha tatizo hilo ambapo kwa upande wa umeme aliambiwa mwaka huu kata yake itaingizwa katika gridi ya taifa na kwa upande wa maji nalo pia ameahidiwa kushughulikiwa.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...