Na Said Mwishehe, Michuzi TV
MAMLAKA ya Dawa na Vifaa Tiba(TMDA) imekutana na wahariri wa vyombo vya habari kwenye kikao kazi kilichofanyika Jijini Arusha.
Kikao hicho kimehusisha wahariri kutoka mikoa ya Dar es Salaam, Kilimanjaro, Arusha na Manyara na lengo kuu ni kubadilisha uwezo kuhusu majukumu , mikakati na malengo ya TMDA katika kutekeleza majukumu yake.
Sababu ya TMDA kukutana na wahariri hao kupitia kikao hicho imelenga kutumia wadau hao ambao wanatoka katika vyombo mbalimbali vya habari kufikisha elimu kwa umma kuhusu TMDA na majukumu yake.
Mada ambazo zimewasilishwa na TMDA kwa wahariri ni mada iliyokuwa inahusu Sheria, Kazi na majukumu ya TMDA.Mada ya pili ilihusu Udhibiti wa vifaa tiba, nyingine Udhibiti wa tumbaku na mazao yake.
Mada nyingine ni Mchango wa maabara ya TMDA katika kuhakikisha ubora,usalama na ufanisi wa dawa,vifaa tiba na vitendanishi, udhibiti wa bidhaa duni na bandia, changamoto za udhibiti wa bidhaa katika soko.Mada nyingine ilihusu wajibu wa wahariri katika kulinda afya ya jamii.
Pamoja na uwepo wa mada zote hizo, mada iliyohusu Udhibiti wa Tumbaku na mazao yake iliibua maswali mengi kwa washiriki wa kikao hicho na maswali yalikuwa mengi.
Baadhi ya maswali ya wahariri kwenda kwa TMDA na hasa aliyetoa mada hiyo, pamoja na mambo mengine imefafanua kwa kina madhara yanayopatikana kutokana na matumizi ya tumbaku.
SWALI:Kutokana na madhara yatokanayo na tumbaku , je Serikali haioni umuhimu wa kuvifungia viwanda vya tumbaku?
Jibu:Ni mapema mno kueleza kwamba tunaweza kufungia viwanda vya tumbaku, tunaamini hata hizi jitihada za kutunga sheria ya kudhibiti tumbaku pamoja na kuteua taasisi zinaonesha nia ya kupunguza matumizi ya tumbaku.
Tumbaku ni uchumi na unaposema unafunga viwanda maana yake kutaathiri wakulima na wadau wa tumbaku, kazi iliyopo ni kuwapa elimu wananchi kuhusu madhara ya tumbaku na kuja na kilimo mbadala.Pili ili watu wafike kuachana na matumizi ya tumbaku, kulima tumbaku lazima wapate kuelimishwa.
Tumezungumza madhara ya tumbaku lakini kuna watu wanavuta na baadhi yao hata ukiwaliuza wanakwambia hakuna madhara ambayo wameyapata , lakini binadamu anahitaji kukumbushwa kila siku hadi pale atakapobadilika.
SWALI:Je kuna tofauti gani kati ya tumbaku na Sigara.
JIBU:Tofauti ya tumbaku na sigara ni kwamba sigara inakuwa imepita kiwandani katika kuitengeneza kwake na tumbaku haijapita viwanda.
SWALI:Kuna madhara gani ya kuweka tumbaku sehemu za siri kama njia ya uzazi wa mpango na kuzuia hamu ya tendo la ndoa?
JIBU:Madhara yako pale pale, hata ukienda kwenye wagonjwa wa kansa baadhi yao unapofuatilia historia zao hasa wanaosumbuliwa na kansa ya kizazi utakuwa huko nyuma walikuwa wakiweka tumbaku sehemu zao za siri.
SWALI:Ni hatua gani zinachukuliwa kudhibiti wanaovuta sigara kwenye mikusanyiko ya watu?
JIBU:Hilo nalo ni tatizo, binafsi(mtoa mada) nachukia sana unakuta mtu anapuliza sigara bila kujali viumbe wengine na ndio maana katika kanuni ya mwaka 2003 ilitoa elekezo la udhibiti uvutaji sigara hadharani, mvutaji anatakiwa kuwa kwenye jengo maalum la kuvutia na sio kwenye mkusanyiko wa watu.
Hata hivyo TMDA kazi yetu ni kuendelea kutoa elimu na suala la kukamata wanaovunja kanuni za uvutaji sigara hiyo itakuwa kazi ya polisi.
SWALI: E -Cigarette ni nini?
JIBU: E-Cigarette ni mbaya sana kuliko ile sigara ambayo wengi wamezoea kuvuta.E-Cigarette inatengezwa kwa kuchukuliwa kwa kemikali mbalimbali na wanaweka kitu ambacho kinachoma hiyo kemikali na mvutaji anavuta hewa.
Hewa hiyo inayovutwa inaingia moja kwa moja kwenye mapafu ya mtumiaji.Hii E-Cigarette huwezi kuuona moshi, ndio maana TMDA tunasema tutadhibiti.
SWALI:Je kuna nchi zimeweza kuzalisha sigara zenye Nicotine ndogo?
JIBU:Bado TMDA hatujafanya utafiti lakini kisayansi inawezekana wala sio jambo gumu na wala sio jambo la kutoka mbinguni, unachokifanya ni kutengeneza Nicotine ya kiwango fulani.
SWALI:Je utafiti unaonesha kuna kemikali 40 zinazoweza kusababisha saratani, TMDA mmefanya utafiti lini?
JIBU:TMDA hatujafanya utafiti huo sisi lakini matokeo ya utafiti yanaonesha uwepo wa madhara hayo, na ndio maana tuko hapa kwa ajili ya kutoa elimu maana vyombo vya habari vinamsaada mkubwa.
Tuseme tu mbali ya tafiti huo na sisi kama taasisi kwa kushirikiana na taasisi nyingine kama NIMRI na vyuo vikuu tutafanya tafiti mbalimbali kuhusu madhara ya tumbaku katika kusababisha magonjwa mbalimbali.Jukumu hili la kudhibiti tumbaku na mazao yake kwetu ni jukumu jipya.
SWALI: Je TMDA inafanya nini katika kuangalia tumbaku kama uchumi?
JIBU:Ni kweli tunafahamu tumbaku ilivyokuwa na mchango mkubwa katika maisha ya jamii ya wanaojihusisha na kilimo cha zao hilo.Hivyo ukija leo na injili ya tumbaku mbaya hautaeleweka lakini kikubwa tunapaswa kuendelea kutoa elimu na kuhakikisha kunakuwa na njia mbadala ya uchumi.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...