Charles James, Michuzi TV
KATIKA kuwajengea uwezo Maafisa Biashara, Wizara ya Uwekezaji imeendesha semina ya mafunzo kwa Maafisa Biashara wa Mikoa yote Nchini huku ikiwasisitiza kuepuka kufunga Biashara za watu kiholela.
Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Uwekezaji, Geofrey Mwambe wakati akifungua mafunzo hayo yaliyoandaliwa na Kituo cha Uwekezaji nchini TIC.
Waziri Mwambe pia amesema kuwa tayari wameshawasiliana na Wizara ya Viwanda na Biashara ili waweze kufungua Idara za Uwekezaji Biashara na Viwanda katika Halmashauri zote nchini.
Mwambe ametumia semina hiyo kuwaasa Maafisa Biashara hao kutumia taaluma na weledi wao katika kutafuta wawekezaji kwenye Mikoa yao lakini pia kuwa daraja la wawekezaji kuwekeza.
" Nyinyi mna nafasi kubwa ya kuchochea maendeleo kwenye Nchi yetu kama kila mmoja kwa nafasi yake ataamua kwa dhati kutumia weledi na taaluma yake kutafuta wawekezaji.
Nchi yetu ina utajiri sana hakuna sehemu yoyote kwenye Nchi yetu ambayo haina soko la kibiashara, kama siyo Madini basi ni Utalii, Kilimo au hata Viwanda, nyanyueni uwekezaji kwenye Mikoa yenu," Amesema Waziri Mwambe.
Amesema pia Wizara yake iko katika mpango wa kuwezesha Maafisa Biashara kuwa wasimamizi wa zile asilimia 10 wanazogaiwa makundi maalum ya Wanawake, Vijana na Wenye Ulemavu.
" Nafikiri kuna haja ya zile asilimia 10 za makundi maalum ziwe zinasimamiwa na Maafisa Biashara maana haiwezekani Maafisa Maendeleo ya Jamii ndio wasimamie watu biashara wakati siyo taaluma zao," Amesema Waziri Mwambe.
Kwa upande wake Afisa Biashara wa Mkoa wa Mbeya Stanley Kibakaya akizungumza kwa niaba ya Maafisa Biashara wenzake amemuahidi Waziri Mwambe kwamba wataenda kufanya kazi kwa bidii huku wakiwa sehemu ya watekelezaji wa mpango wa Tatu wa Taifa wa Maendeleo kwa bidii na weledi.
" Tunakushukuru Mhe Waziri kwa nafasi hii uliyotupatia, semina za mafunzo kama hizi zimekua zina manufaa makubwa na tunaomba ziendelee kuwepo mara kwa mara," Amesema Kibakaya.
Afisa Biashara wa Mkoa Mbeya, Stanley Kibakaya akitoa neno la shukrani kwa Waziri wa Uwekezaji, Geofrey Mwambe baada ya kufungua semina ya mafunzo jijini Dodoma leo.Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Uwekezaji, Geofrey Mwambe (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Maafisa Biashara wa Mikoa baada ya kumaliza kuzungumza nao jijini Dodoma.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...