MENEJA Mkuu wa Kampuni za Ranchi za Taifa (NARCO), Prof Peter Msoffe ametaja mikakati itakayosaidia kampuni hiyo kuweza kujiendesha kibiashara Zaidi.

Prof Msoffe amebainisha mikakati hiyo leo  baada ya kumalizika kwa kikao cha makabidhiano ya ofisi na aliyekuwa Kaimu Meneja Mkuu wa NARCO, Masele Shilagi kilichofanyika kwenye ofisi hizo jijini Dodoma.

Akizungumzia mikakati hiyo, Prof Msoffe amesema kuwa serikali inataka kampuni hiyo iwe kitovu cha umahiri wa masuala yote yanayohusu ranchi.

" Katika kuhakikisha hilo linafanikiwa ni lazima kampuni ijipange katika uzalishaji wa nyama ya kutosha iliyo bora, uzalishaji wa mifugo iliyo bora, kutoa mafunzo kwa wataalam na wafugaji, kujiendesha kibiashara na kuweza kupeleka gawio serikalini," Amesema Prof Msoffe.

Amesema ana matarajio makubwa kuwa hayo yataweza kutekelezeka kwa kuwa yeye ameikuta kampuni ikiwa inaendelea kuimarika hivyo kwa kushirikiana na viongozi na watendaji wa kampuni wataweza kutekeleza mikakati hiyo ambayo itawasaidia kuweza kutimiza azma ya serikali kwa kampuni hiyo.

Naye Masele Shilagi ambaye alikuwa ni Kaimu Meneja Mkuu wa Kampuni ya Ranchi za Taifa amesema kuwa kampuni imekuwa ikiendelea kuimarika kimapato ambapo iliweza kujiendesha bila kutumia ruzuku kutoka serikalini lakini pia wameweza kusimamia mapato na matumizi ambapo kampuni imekuwa ikipata hati safi.

Amesema kampuni imeweza kupima baadhi ya ranchi zake na kushughulikia migogoro iliyokuwepo ikiwemo ya uvamizi wa wananchi kwenye maeneo ya ranchi. Aidha, Masele amewashukuru viongozi na watumishi wa NARCO kwa ushirikiano waliompatia kipindi cha uongozi wake na kuwaomba waendelee kutoa ushirikiano kwa Meneja Mkuu mpya.

Naye Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Uzalishaji na Masoko, Stephen Michael amesema kuwa viongozi na watendaji wanao wajibu wa kujipanga vizuri ili kuhakikisha malengo na matarajio ya serikali yanatimizwa. NARCO inazo fursa nyingi kwenye uzalishaji wa nyama bora, mifugo bora, malisho na utoaji wa elimu kwa wafugaji.

Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Uzalishaji na Masoko (WMUV), Stephen Michael (wa tatu kutoka kushoto) akiwa kwenye picha ya pamoja na viongozi na watumishi wa Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO) mara baada ya kukamilika kwa makabidhiano ya ofisi yaliyofanyika jijini Dodoma.
Meneja Mkuu wa Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO), Prof Peter Msoffe (kulia) akipeana mkono na aliyekuwa Kaimu Meneja Mkuu wa kampuni hiyo, Masele Shilagi baada ya kukabidhiana ofisi jijini Dodoma.
Meneja Mkuu wa Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO), Prof Peter Msoffe (kulia) akipokea taarifa ya makabidhiano kutoka kwa aliyekuwa Kaimu Meneja Mkuu wa Kampuni hiyo, Masele Shilagi (kushoto). Katikati ni Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Uzalishaji na Masoko (WMUV), Stephen Michael akishuhudia makabidhiano hayo yaliyofanyika kwenye Ofisi za NARCO jijini Dodoma.
 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...