Charles James, Michuzi TV
KATIKA kuhakikisha kuwa inaboresha sekta ya afya nchini, Serikali imetenga kiasi cha Sh Bilioni 149 kwa ajili ya kugharamia bima za afya kwa wananchi wasio na uwezo wa kugharamia matibabu.
Hayo yamesemwa leo jijini Dodoma na Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto, Dk Dorothy Gwajima wakati akizindua Bodi mpya ya Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya na Maadhimisho ya miaka 20 ya NHIF.
Waziri Dk Gwajima amesema serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan imepanga kutekeleza sheria ya bima ya afya kwa wote na kuwahakikishia wananchi wote huduza za afya wakiwemo wasio na uwezo wa kugharamia matibabu.
Dk Gwajima amesema sheria hiyo inalenga kuhakikisha kila mtanzania anakuwa na bima ya afya na kwamba kutokuwa na fedha au uwezo wa kuchangia huduma za matibabu isiwe kikwazo cha mwanannchi kupata huduma za afya.
Amesema katika bajeti hiyo mpya ambayo utekelezaji wake umeanza leo Julai 1, Serikali ya Rais Samia itaendelea kuboresha sekta hiyo muhimu kwa mustakabali wa maisha ya Watanzania.
“ Utekelezaji wa jambo hili unaenda vizuri na kama mlivyomsikia Waziri Mkuu alipokuwa akisoma hotuba ya kuwasilisha hoja ya kuhitimisha bunge alisema serikali imejipanga kuwasilisha muswada wa sheria ya bima ya afya kwa wote kwenye bunge la Septemba mwaka huu.
Kwahiyo dhamira ya Serikali yenu hii ni njema ndani ya siku 100 za uongozi wa Rais Samia tayari ajenda hii imekimbia mbio kubwa na kufikia kwenye hatua ambayo tunamalizia na kuingia kwenye utekelezaji,” Amesema Dk Gwajima.
Waziri Dk Gwajima amesema katika kusherekea miaka 20 ya kuanzishwa kwa NHIF kunatoa nuru kuanza kujipanga zaidi kuwafikia wanachama na kuwasikiliza mahitaji yao kwani itasaidia kuboresha zaidi na kuufanya mfuko kuwa bora zaidi.
“ Wekeni mipango madhubuti ya kushughulikia changamoto ambazo mmekabiliana nazo katika kipindi hiki ili ziwe chachu ya kufikia mafanikio na lengo la serikali ya kila mtanzania kuwa ndani ya mfumo wa bima ya afya," Amesema Dk Gwajima
Ameutaka NHIF kuhakikisha inatumia kipindi hiki cha siku 90 za maadhimisho kutoa elimu zaidi na kuhamasisha wananchi hususani wa Vijijini ili waweze kuona umuhimu wa bima ya afya na kujiunga nayo.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Bernad Konga amesema kwa kipindi cha miaka 20 ya utoaji huduma NHIF imeongeza wigo wa kutoa huduma kwa kuendelea kusajili vituo vya kutolea huduma za afya kutoka vituo 3,198 wakati inaanzishwa hadi vituo 8970 juni 2020.
Konga amesema katika kupanua wigo wa wanachama mfuko umejumuisha makundi mbalimbali ikiwa ni pamoja na Wabunge, Wajumbe wa baraza la wawakilishi, Wajasiriamali, Wafanyakazi wa Kampuni Binafsi na Wanafunzi wa vyuo.
“Idadi ya wanachamna na wachangiaji imeongezeka kutoka wanufaika 691,774 mwaka 2001 hadi kufikia wanufaika milioni 4.3 mwezi Machi 2021 sawa na asilimia nane ya watanzania wote,”Amesema Konga.
Naye Mwenyekiti Mpya wa Bodi ya NHIF Juma Muhimbi amesema katika kuhakikisha mfuko unaendelea mbele zaidi wamejipanga kuhakikisha wanawasikiliza wanachama kero zao na kuzipatia ufumbuzi.
Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto, Dk Dorothy Gwajima akimkabidhi vitendea kazi Mwenyekiti mpya wa Bodi ya Wakurugenzi ya Mfuko wa Taifa wa Bima (NHIF), Juma Muhimbi baada ya kuzindua Bodi hiyo leo jijini Dodoma.
Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto, Dk Dorothy Gwajima akizungumza wakati wa uzinduzi wa Bodi mpya ya Mfuko wa Taifa wa Bima NHIF na maadhimisho ya miaka 20 ya Mfuko huo leo jijini Dodoma.
Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Benard Konga akizungumza wakati wa uzinduzi wa Bodi ya Mfuko wa Taifa wa Bima NHIF leo jijini Dodoma.
Mwenyekiti mpya wa Bodi ya Mfuko wa Taifa wa Bima NHIF, Juma Muhimbi akizungumza wakati wa uzinduzi wa bodi hiyo uliofanywa na Waziri wa Afya, Dk Dorothy Gwajima leo jijini Dodoma.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...