Na Karama Kenyunko, Michuzi TV
KAIMU Meneja Uingizaji na Usafirishaji wa Mbolea Nje ya Nchi.(TFRA), Mselem Seleman amesema Tanzania inazaidi ya tani laki 1.5 za mbolea ambazo tayari zimeshatolewa kibali kusafirishwa kwenda nje ya nchi hivyo kuna umuhimu wa wafanyabiashara kuongeza uzalishaji wa mbolea ili kuongeza soko hilo.
Akizungumza katika Maonesho ya Biashara ya Kimataifa (Sabasaba),yanayoendelea Jijini Dar es Salaam, Seleman amesema zipo nchi nyingi zinazotumia mbolea na kwamba zinapitia Tanzania.
Moja wapo ya nchi hizo ni Rwanda, Burundi,Congo,Zambia, Malawi na nyingine Kenya.
"Tunawaomba wazalishaji wa mbolea kuongeza uzalishaji ili kuweza kukuza soko la mbolea ndani na nje ya nchi na kuwezesha nchi kuwa kitovu cha biashara hiyo kwa nchi ambazo zinaizunguka," amesema
Pia amesema kuwa mfanyabiashara ambaye atatakiwa kusafirisha mbolea nje ya nchi anapaswa kuomba kibali kwa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) kwa kupitia mtandao.
Kwa upande wake, Afisa Ubora wa Mbolea (TFRA), Raymond Konga amesema kila mbolea au kisaidizi cha mbolea lazima isajiliwe na Mamlaka hiyo kabla haijaanza kutumika nchini kwa mujibu wa kifungu namba 8 cha sheria ya mbolea.
Amesema hairuhusiwi kwa mtu yeyote kuingiza mbolea nchini isipokuwa awe amepata kibali kutoka katika mamlaka kwa mujibu wa kifungu na.21.
“Uingizaji wa mbolea nchini unafanyika kwa njia mbili ambapo ya kwanza ni kwa kutumia mfumo wa ununuzi wa mbolea kwa pamoja.Mfumo huu unasimamiwa na kanuni za ununuzi wa mbolea kwa pamoja, njia ya pili ni uingizaji wa mbolea kwa mfumo huria.Katika mfumo huu kila mtu anaruhusiwa kuingiza mbolea ilimradi amefuata sheria na taratibu za uingizaji wa mbolea”. Amesema Konga.
Sanjari na hayo TFRA inawakaribisha wadau na wananchi kwa ujumla kutembelea banda lao katika maonesho ya Biashara yanayoendelea katika viwanja vya Mwalimu Nyerere Sabasaba Jijini Dar es Salaam.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...