WADAU mbalimbali kutoka sekta ya fedha nchini wameshiriki tukio la kuorodheshwa kwa toleo la tatu la hatifungani za Kampuni ya utoaji Mikopo kwa Mabenki na Taasisi za Fedha kwa ajili ya Mikopo wa nyumba Tanzania (TMRC), katika Soko la Hisa Dar es Salaam ambalo lengo lake ni kuhakikisha Watanzania wanapata fursa ya kupata fedha kwa ajili ya mkopo wa nyumba.

Akisoma hotuba  katika tukio hilo, Kamishna wa Idara ya Maendeleo Sekta  ya Fedha ndani ya Wizara ya fedha na Mipango,Dkt Charles Mwamwaja amesema tukio hilo la kuorodhesha toleo la tatu la hatifungani za TMRC kwenye Soko la Hisa Dar es Salaam linakuja baada ya miaka miwili tangu kutolewa kwa toleo la pili la hatifungani Julai 1 mwaka 2018 .

"Ninayo furaha ya kipekee kushiriki leo kwenye uorodheshaji wa toleo la tatu la hatifungani za TMRC ya miaka mitano kwa wakati huu ambao TMRC imeanza kutafuta fedha za kukopesha kwenye mabenki kwa ajili ya mikopo ya nyumba kwenye soko la fedha, 

"Shughuli hii ya leo inachangia kwa kiasi kikubwa katika kukua kwa masoko ya mitaji hapa nchini Tanzania, hatifungani za TMRC ya miaka mitano ni matokeo ya mpango wa Serikali ya Tanzania ya kuongeza upatikanaji wa fedha za muda mrefu chini ya marekebisho ya sekta ya fedha.

"Yakiwa na malengo ya kuhakikisha kunakuwa na mfumo wa upatikanaji wa fedha za muda mrefu zitakazoendana na mahitaji ya soko kwa ajili ya maendeleo ya uchumi wa nchi yetu.Mikopo ya nyumba kama mnavyofahamu ni eneo muhimu na ndilo hasa linalolengwa zaidi kupitia hatifungani hizi ambazo tumezizindua,"amesema.

Aidha amesema utekelezaji huo unaendana na mpango mkuu wa maendeleo ya sekta ya fedha 2021 hadi 2030 unaohimiza na kusisitiza upatikanaji wa fedha za muda mrefu."Nikiri TMRC imefanikiwa kutoa toleo la tatu kwa mafanikio makubwa."

Ameongeza TMRC wamewezesha kuendelea kukuza imani ya uwekezaji wa TMRC kwa kuwa toleo la tatu makusanyo yamezidi matarajio kwa asilimia 26,na wameshuhudia mabenki mengi yakijihusisha na mikopo ya nyumba na yamekuwa yakiongozeka kutoka benki tatu mwaka 2010 hadi benki 32 mwaka 202.

"Tumeshuhudia kuongeza kwa muda wa mikopo ya nyumba kutoka miaka mitano mpaka saba lakini mingine kutoka miaka 15 mpaka miaka 25 ,uwepo wa TMRC umewezesha mabenki kutoa mikopo ya nyumba,pia idadi ya benki zinazoshiriki katika utaratibu huu zimeongezeka kwa kiasi kikubwa,"amesema.

Ameongeza mfumo wa mkopo wa nyumba una mchango katika uchumi wa nchi na hilo linaonekana katika nchi mbalimbali duniani ambazo zina mfumo huo wa muda mrefu na wenye kushirikisha wadau mbalimbali .

"Mojawapo ya faida ya mfumo huu wa kutoa nafasi ya kuwekeza kwenye nyumba kama sehemu ya mtaji ambayo inaweza kumsaidia mmiliki kuwa na mapato ya ziada,pia kuchangia kodi za Serikali kupitia makato ya kodi ya mwenye nyumba.

"Kuinua uchumi wa mmiliki wa nyumba, kuongeza matumizi kutokana na ongezeko la kipato na kufanya watengenezaji wa mali na bidhaa na kufanya uzalishaji kuongeza uzalishaji ndani ya nchi.Miliki pia ni sehemu ya mali zisizohamishika ambazo hutumika kama dhamana kwa ajili ya kupata mitaji kutoka kwenye taasisi za fedha,"amesema.Ametoa mwito kwa wananchi na Watanzania kwa ujumla kufaidika na huduma ya utoaji wa mikopo ya nyumba, lakini vilevile.

Kwa upande wake Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA),CPA Nicodemus Mkama amesema Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana iliidhinisha maombi ya Kampuni ya TMRC kuuza toleo la tatu la hatifungani lenye thamani ya Sh.bilioni saba ikiwa ni sehemu ya mpango wa kutoa hatifungani yenye thamani ya Sh.bilioni 120.

Amesema na hiyo imefanyika kwa mujibu wa Sheria ya masoko ya mitaji na dhamana pamoja na kanuni za masomo ya mitaji na dhmana na mauzo hayo yalifunguliwa Aprili na kufungwa Julai ambapo TMRC imefanikiwa kukusanya kiasi bilioni 8.9 ikilinganishwa na lengo la kukusanya sh.bilioni saba , sawa na mafanikio ya asilimia 127.

"Haya ni mafanikio makubwa, ni dhahiri mafanikio haya yametokana na ushiriki zaidi kwenye hii hatifungani ya uwekezaji ukilinganisha na ule mpango uliokuwepo na hii imetokana na juhudi zinazofanyika kwa kushirikiana na wadau wa sekta ya fedha kwa kutoa elimu kwa umma.

"Kwa hiyo mafanikio makubwa kama haya ni matokeo chanya ya elimu kwa umma ambayo inafanywa na wadau wa sekta ya fedha ya kuhakikisha tunatoa elimu kwa umma kuhusu faida na fursa zinazopatikana katika masoko ya mitaji , fedha ambazo zimepatikana kupitia mauzo ya toleo hili la tatu tunatarajia.

. "Zitatumika kutekeleza mpango mkakati wa kutoa mikopo yenye riba nafuu kwa benki ambazo zinatoa mikopo ya nyumba kwa lengo la kuboresha makazi ya wananchi na kuongeza uwekezaji katika sekta ya fedha na kama mnavyohafamu dhamira ya Serikali ni kuona sekta ya fedha inawezesha upatikanaji wa fedha kwa ajili ya kutoa mikopo kwa gharama nafuu,"amesema.

Amesisitiza kwa hiyo hatua hiyo ni muhimu kwani ina matokeo nyanya katika ukuaji wa sekta binafsi, sekta ya umma na uchumi wa nchi kwa ujumla, hivyo utoaji wa hatifungani ya TMRC unachangia dhamira ya Rais pamoja na malengo ya serikali ya kujenga mazingira wezeshi kujenga uchumi shindani na viwanda kwa maendeleo ya watu.

Aidha amesema mauzo ya toleo la tatu la hatifungani za TMRC yamekuwa na matokeo chanya katika maendeleo ya masoko ya mitaji na sekta ya fedha kwa ujumla kwani asilimia 95 ya washiriki katika uwekezaji wamekuwa wa ndani na washiriki wa nje ni asilimia tatu.
Wakati huo huo ...amesema uwepo wa TMRC umekuwa na mafanikio mengi yakiwemo ya kujenga wanahisa wengi zaidi kwani walivyoanza walikuwa na wanahisa wanne tu lakini leo kuna wanahisa 17 na wengine wanatoka nje.

"Kwa hiyo ni jambo nzuri,na katika kipindi hicho tumeweza kukopesha mabenki kiasi cha Sh.bilioni 150 ingawaje zmepungua kidogo , mwishoni mwa Juni ilikuwa kiasi cha Sh.bilioni 134 kiasi ambacho kinakwenda kuhudumia wananchi kwa ajili ya mataji ya nyumba
"Pia tumesaidia kuongeza muda wa marejesho ya nyumba hadi kufikia miaka 25 , muda ambao upo kisheria, hii mikopo ya nyumba haiwezi kwenda kuwa zaidi ya miaka 25 lakini kwa kuwa benki zinajua namna ya kupata hizi fedha TMRC wanatoa mikopo ya miaka 15 hadi miaka 20.

"Kwa hiyo inatoa unafuu katika urejeshaji , aidha tumehamasisha mpaka leo hii kuna benki 32 zinazojihusisha na kutoa fedha za mikopo ya nyumba kati ya benki kama 50.Hii ni kitu cha kutia moyo kwani benki nyingi zinajua TMRC wapo,"amesema.

Pia amesema wanafahamu huduma hiyo imesambaa, takwimu zinaonesha katika mikopo iliyotolewa iko katika mikoa 23 tofauti na hiyo ni kwasababu mfumo wanaotumia wao kupitia mabenki unarahisisha kumfikia mteja au hizi fedha kumfikia mteja kokote aliko.

"Kwa hiyo mikopo ya nyumba kwa ujumla wake imeendelea kukua, bilioni 76 lakini hadi kufikia Sh. bilioni 465 .yote yasingewezekana kama isingekuwa juhudi za Serikali ya Tanzania kuanzisha mradi wa kukopesha nyumba kwa hiyo leo tunasimama kujivunia mafanikio.

"Ni kwasababu Serikali ilikuwa na maoni ya kuisaidia sekta ya mikopo ya nyumba na wakachukua huu mradi wa mikopo ya nyumba ambao walishirikiana na benki ya dunia na kuanda utaratibu huu wa mikopo ya muda mrefu.Tunajua Wizara ya Fedha imehusika katika kuweka utaratibu zile fedha kutumika, bado ni muhimu juhudi kama hizi ziendelee kufanywa na Serikali,"amefafanua.



Kamishna wa Idara ya Maendeleo Sekta ya Fedha ndani ya Wizara ya fedha na Mipango,Dkt Charles Mwamwaja akigonga Kengele kuashiria kuorodheshwa kwa toleo la tatu la Hatifungani ya Kampuni ya TMRC katika soko la Hisa la Dar es Salaam,Pichani kulia ni Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA),CPA Nicodemus Mkama na Mwenyekiti wa Bodi ya TMRC Ammish Owusu wakishuhudia tukio hilo kwa pamoja.

Kamishna wa Idara ya Maendeleo Sekta ya Fedha ndani ya Wizara ya fedha na Mipango,Dkt Charles Mwamwaja akizungumza wakati wa hafla ya kuorodheshwa kwa toleo la tatu la Hatifungani ya Kampuni ya TMRC katika soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) jijini Dar es Salaam.
Afisa Mtendaji Mkuu wa TMRC akizungumza jambo mbele ya Wanahabari na Wageni waalikwa mbalimbali (hawapo pichani) wakati wa hafla ya kuorodheshwa kwa toleo la tatu la Hatifungani ya Kampuni ya hiyi katika soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya Wadau mbalimbali wakishuhudia tukio hilo wakati likifanyika

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...