Na Mwandishi Wetu
MAELFU ya wananchi waliohudumiwa katika banda la Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) kwenye Maonesho ya Sabasaba yanayofanyika katika viwanja vya Mwalimu Nyerere, Dar es Salaam wameupongeza Mfuko kwa kazi kubwa na nzuri ambayo imefanyika katika maonesho hayo.
Huduma zinazotolewa na Mfuko katika Maonesho hayo ambayo yalianza tangu Juni 28, mwaka huu ni pamoja na usajili wa wanachama wapya, elimu ya umuhimu wa bima ya afya, kupokea maoni ya wananchi juu ya uboreshaji na uimarishaji wa huduma pamoja na kutatua changamoto wanazokutana nazo wanachama katika huduma.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti baada ya kupata huduma, walisema kuwa kusogeza huduma ya kusajili katika maonesho hayo imesaidia kwa kiasi kikubwa wananchi kujisajili bila usumbufu wowote.
“Binafsi nipongeze sana kwa huduma ambazo mmeziweka hapa bandani ambapo mtu anafika anapata elimu ya kitu gani atakipata baada ya kujiunga na huduma na anapoamua kujiunga anajaza fomu hapa hapa na kulipia bila usumbufu wowote, hii kazi ni nzuri,” alisema Bi. Mwajabu Ally wakati akitoa maoni yake juu ya huduma zinazotolewa.
Mwananchi mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Edward Komba alisema wazi kuwa anajivunia kuwa mwanachama wa NHIF kwa kuwa anaridhishwa na huduma zinazotolewa katika vituo vya kutolea huduma za matibabu.
“Pamoja na huduma nzuri ambazo tunazipata kwa sasa wanachama lakini ombi langu kwa Mfuko uendelee kuboresha huduma zikiwemo za kuwafikia wananchi katika maeneo ya vijijini ili ikiwezekana kila mwananchi aweze kuwa ndani ya bima ya afya,” alisema Bw. Komba.
Katika hatua nyingine walitoa wito kwa wananchi ambao bado hawajajiunga na huduma za NHIF kujiunga mara moja ili kujihakikishia upatikanaji wa huduma za matibabu wakati wowote.
Akizungumzia huduma mwitiko wa wananchi katika kupata huduma bandani hapo, Meneja Uhusiano wa NHIF, Bi. Anjela Mziray alisema jumla ya wananchi 3,724 wamefika n kupata huduma na kati ya hao 1,407 wakiunga na huduma za Mfuko.
Bi. Mziray aliwaomba wananchi kuitikia wito wa kijiunga na huduma za Mfuko ili kuondokana na usumbufu wa kupata huduma za matibabu wakati wanapopatwa na magonjwa.
Alisema kuwa Mfuko umesogeza zaidi huduma kwa wananchi wake kwa kuwa na Ofisi kila Mkoa ili kurahisisha uptikanaji wa huduma za kujiunga lakini pia kutatuliwa changamoto wakati wowote zinapojitokeza.
Maafisa wa Mfuko wa Taifa ya Bima ya Afya (NHIF) wakiendelea na kazi ya kusajili wananchi wanaojitokeza kupata huduma ya bima ya Afya katika maonesho ya 45 ya Biashara ya Kimataifa ya Sabasaba yanayofanyika kwenye viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere Barabara ya Kilwa mkoa wa Dar es Salaam.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...