Eleuteri Mangi-Dodoma
Wakuu wa Vitengo vya Mawasiliano Serikalini katika Wizara, Taasisi, Wakala pamoja na Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa wametakiwa kuwa wabunifu na wepesi katika kutangaza kazi Serikali zinazotekelezwa katika Ofisi zao.
Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO) na Msemaji Mkuu wa Serikali, Ndugu Gerson Msigwa wakati wa kikao chake na Wakuu hao Julai 12, 2021 katika Ukumbi wa Kambarage Hazina Jijini Dodoma kuhusu utoaji wa taarifa za Utekelezaji wa Serikali kwa umma ikiwa ni pamoja na masuala yanayohusu tasnia ya Habari Serikalini.
“Tuwe na moyo wa kupenda kazi, fanyeni kazi kwa kuzingatia taaluma ya habari na tangazeni kazi zinazotekelezwa katika ofisi zenu na mjenge mahusiano mazuri ya kikazi na vyombo vya habari maana hivyo ndiyo vyombo vyetu vya kutangaza kazi za Serikali kwa umma” amesema Msigwa.
Mwanzoni mwa kikao kazi hicho, Wakurugenzi wasaidizi wa idara hiyo Rodney Thadeus pamoja na Zamaradi Kawawa walisisitiza wakuu hao wa vitengo serikalini kuendelea kushirikiana katika kuisemea Serikali kwenye maeneo yao ili kuwapa wananchi taarifa za maendeleo katika sekta mbalimbali ambazo zina tija kwa wananchi na taifa.
Akichangia katika kikao hicho Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini kutoka Sekta ya Uchukuzi Christopher Philemon amesema jukumu la Kitengo cha Mawasiliano Serikalini ni kuhabarisha umma kwa kufanya kazi zenye ubora unaoendana na mabadiliko ya teknolojia ili kuwafikia watu wote katika maeneo mbalimbali mjini na vijijini ndani na nje ya nchi yetu.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...