Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Dkt. Faustine Ndugulile akiongoza majadiliano katika kikao kazi kilichojadili utekelezaji wa mgao wa mrabaha kwa kazi za wasanii wa muziki pamoja na marekebisho ya Kanuni za Maudhui (pembeni yake ni Waziri wa Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo Mhe. Innocent Bashungwa.
Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Dkt. Faustine Ndugulile pamoja na Waziri wa Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo Mhe. Innocent Bashungwa, wakiwa katika kikao kazi kilichojadili utekelezaji wa mgao wa mrabaha kwa kazi za wasanii wa muziki pamoja na marekebisho ya Kanuni za Maudhui.

Na Mwandishi wetu
WAZIRI wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Dkt . Faustine Ndugulile MB, pamoja na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Innocent Bashungwa wamekutana katika kikao cha pamoja kujadili namna Wizara wanazozisimamia zitakavyotekeleza suala la mgao wa mrabaha kwa kazi za wasanii wa muziki zinazochezwa kwenye vyombo mbalimbali vya Habari.

Katika kikao hicho kilichofanyika jijini Dar es Salaam, Mawaziri hao wawili wamekutana na Wakurugenzi wakuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Chama cha Hatimiliki Tanzania (COSOTA), Makatibu Wakuu wa Wizara zote mbili pamoja na wataalaam kutoka Kituo cha data cha Taifa,TCRA na wizara.

Kikao kazi hicho kimejadili na kuweka mikakati ya pamoja juu ya utekelezaji wa zoezi la kuanza rasmi kwa mgao wa mrabaha kwa wasanii, pia wamejadili na kupitia mapendekezo ya marejeo ya Kanuni za Maudhui Mtandaoni ili kuona uwezekano wa kupunguza au kufuta baadhi ya tozo za leseni za maudhui mtandaoni.

Wamekubaliana kuhakikisha miundombinu itakayowezesha ukusanyaji wa mirabaha inawekwa katika hali ya utayari huku Mawaziri wakiziagiza taasisi za TCRA, Kituo cha Data na COSOTA kuhakikisha mifumo husika itakayohusika kukokotoa mirabaha inakamilika na kufanya kazi kwa wakati kama ilivyokusudiwa.

Katika kikao hicho Mawaziri walipokea na kujadili taarifa za maandalizi ya ufuatiliaji maudhui na namna maudhui ya kazi za muziki za wasanii zitakavyokokotolewa ili kuhakikisha wasanii wa muziki wanapata haki yao ya mapato yatokanayo na kazi zao za sanaa ya muziki.

Pia walijadili mapendekezo ya marekebisho ya kanuni za utangazaji na mfumo wa leseni unaopendekeza maboresho katika mfumo wa upatikanaji wa maudhui ya bila kulipia na ya kulipia, kanuni zinazotarajiwa kuanza kutumika hivi karibuni baada ya taratibu bayana kukamilika.

Awali Mkuu wa COSOTA akitoa taarifa mbele ya waheshimiwa Mawaziri alibainisha kuwa mara zoezi la ulipaji mirabaha litakapoanza watahakikisha kila aliechangia kufanikisha kazi ya msanii husika kukamilika hadi kurushwa anapokea stahiki yake, aliwataja baadhi ya wahusika hao kuwa ni pamoja na watayarishaji wa muziki, waandishi wa mashairi na lebo za muziki.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...