Askari wa Uhifadhi wa Wanyamapori wametakiwa kujenga mahusiano mazuri na wananchi wanaozunguka Pori la Akiba Uwanda lililopo katika bonde la ziwa Rukwa ili kuondoa hofu kwa wananchi inayowafanya wajizamishe kwenye maji wanapotaka kukamatwa na askari hao baada ya kuvamia pori hilo kwa shughuli za uvuvi, kilimo na ufugaji.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe Mary Masanja (Mb) wakati wa ziara ya kikazi ya kusikiliza kero za wananchi wa vijiji cha Nankanga na Kilangawana Wilaya ya Sumbawanga Mkoani Rukwa .

“Jitahidini sana kujenga mahusiano mazuri na wananchi kwa sababu hatuwezi kurudisha uhai wa hawa wananchi wanaojizamisha kwenye maji kwa hofu ya kukamatwa na askari” amesema Mhe. Masanja.

Mhe. Masanja amewaagiza maaskari wanyamapori kuacha kujichukulia sheria mkononi kwa kuwapeleka kwenye vyombo vya sheria wananchi wanaovamia Pori la Akiba Uwanda.

Amewahamasisha wananchi wa eneo hilo kuondoa hofu zinazowapelekea kujizamisha ziwani.

“Msiishi kwa hofu kwa sababu Serikali hii inaongozwa kwa amani na utulivu, napenda kuwajulisha kuwa Serikali itaweka utaratibu wa vibali maalumu vya kuvua samaki ili mwananchi anapopita awe huru” amefafanua Mhe. Masanja.

Aidha, Mhe. Masanja amewaasa wananchi wa vijiji hivyo kufanya shughuli zao kwa kuzingatia sheria , kanuni na taratibu ili kuepuka adha ya kukamatwa ndani ya Pori la Akiba Uwanda ambalo liko ndani ya Ziwa Rukwa.

Kuhusu madai ya kila kijiji kutaka kujengewa forodha, Mhe. Mary Masanja amewataka wananchi hao kuwa wavumilivu wakati wataalamu wanafanya uchunguzi wa eneo linalofaa kwa ajili ya forodha.

Naye, Mwakilishi wa Vyama vya Wavuvi kutoka kijiji cha Nankanga, John Mwangilo amesema wananchi wa eneo hilo wamekuwa wakiwakimbia askari wa wanyamapori kwa kuhofia kukamatwa katika maeneo ya hifadhi.

“Tangu mwaka 2016 kumekuwa na vifo vingi ziwani ambavyo vyanzo vake ni hofu inayotokana na wavuvi kuhofia kukamatwa na askari wa wanyamapori na kuamua kujitosa ziwani kwa kuogopa vipigo vinavohatarisha maisha” amesema Bw. Mwangilo.

Mkazi mwingine wa Kijiji cha Kilangawana, Koritida Kalunde ameiomba Serikali kuangalia upya mipaka ya Pori la Akiba Uwanda ili wananchi wapate maeneo ya kulima na kufanya shughuli nyingine za maendeleo.

Kwa upande wake Meneja wa Pori la Akiba Uwanda, Kamishna Uhifadhi Mwandamizi Honest Njau amesema pori hilo lina manufaa makubwa kwa wananchi na katika kuendeleza utalii.

“Hili pori lina umuhimu mkubwa kwa sababu lina wanyama mbalimbali kama tembo, viboko, mamba na ndege wa aina mbalimbali na lina samaki aina ya Gege anayepatikana ndani ya ziwa Rukwa peke yake, pia ni sehemu pekee ambayo ina mazalia ya nzige wekundu duniani kote”bw. Njau amesisitiza.

Amesema pamoja na changamoto zilizopo mwaka 2020 askari wa wanyamapori walifanya kazi kubwa sana ya kuwaokoa watu waliopata adha ya mafuriko kijiji cha Kilangawana

Mhe. Mary Masanja amehitimisha ziara yake ya kikazi ya kusikiliza kero za wananchi na kutembelea vivutio vya utalii vinavyopatikana katika Kanda ya Nyanda za Juu Kusini.

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb) akizungumza na wananchi wa kijiji cha Nankanga kuhusu Serikali kuweka utaratibu wa kuvua samaki katika Pori la Akiba Uwanda linasimamiwa na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) ambalo lipo katika bonde la ziwa Rukwa katika Wilaya ya Sumbawanga mkoani Rukwa alipofanya ziara ya kikazi kijijini hapo.
Baadhi ya wananchi wa kijiji cha Nankanga wakimsikiliza Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb) (hayupo pichani) alipofanya ziara ya kikazi katika Pori la Akiba Uwanda ambalo lipo katika bonde la ziwa Rukwa katika Wilaya ya Sumbawanga mkoani Rukwa.
Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga, Mhe. Sebastian Waryuba akimkaribisha Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb) (hayupo pichani) kuzungumza na wananchi wa kijiji cha Nankanga alipofanya ziara ya kikazi katika eneo la Pori la Akiba Uwanda ambalo lipo katika bonde la ziwa Rukwa katika Wilaya ya Sumbawanga mkoani Rukwa.
Mbunge wa Jimbo la Kwela, Mhe. Deus Sangu akitoa salamu za shukrani kwa Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb) (kulia) kwa kufika jimboni kwake kwa ajili ya kuzungumza na wananchi wa kijiji cha Nankanga kuhusu mgogoro wa mipaka ya Pori la Akiba Uwanda ambalo lipo katika bonde la ziwa Rukwa katika Wilaya ya Sumbawanga mkoani Rukwa.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb) (kushoto) na Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga , Mhe. Sebastian Waryuba (kulia) pamoja na kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya hiyo, wakiwasili katika kijiji cha Nankanga eneo lilipo Pori la Akiba Uwanda kwenye bonde la ziwa Rukwa Wilaya ya Sumbawanga mkoani Rukwa alipofanya ziara ya kikazi kijijini hapo kwa ajili ya kutatua mgogoro wa mipaka ya pori hilo na eneo linalotumiwa na wakazi wa eneo hilo.

Meneja wa Pori la Akiba Uwanda na Kamishna wa Uhifadhi Mwandamizi kutoka Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA), Honest Njau akielezea historia ya Pori la Akiba Uwanda ambalo lipo katika bonde la ziwa Rukwa Wilaya ya Sumbawanga mkoani Rukwa wakati wa mkutano wa Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb) (hayupo pichani)  na wananchi katika kijiji cha Nankanga.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...