Veronica Simba na Zuena Msuya- Manyara

Naibu Waziri wa Nishati, Wakili Stephen Byabato amesema yeyote atakayekwamisha kazi ya kusambaza umeme vijijini atachukuliwa hatua kali za kisheria na kinidhamu kwakuwa anarudisha nyuma juhudi za serikali kupeleka maendeleo kwa wananchi.

Wakili Byabato amesema hayo Agosti 14, 2021 wakati akizindua mradi wa Usambazaji Umeme Vijijini Awamu ya Tatu, Mzunguko wa Pili katika Mkoa wa Manyara.

Hafla ya uzinduzi huo imefanyika katika Wilaya ya Mbulu ambapo amewasha umeme katika Kijiji cha Mungahay, Kata ya Tumati.

Akizungumza na wananchi waliohudhuria uzinduzi huo, Naibu Waziri amesema kuwa Serikali imetenga fedha nyingi kwa ajili ya kuhakikisha kuwa vijiji na vitongoji vyote nchini vinapata umeme kabla ya Desemba 2022, hivyo haitavumilia kuona mtu yeyote anathubutu kukwamisha kazi husika.

“Hatutamwacha salama mtu yeyote awe Mkandarasi, Afisa kutoka TANESCO, Wizara ya Nishati na hata mwananchi. Lazima tutamshughulikia. Hilo nawaambia wazi,” amesisitiza Wakili Byabato.

Akizungumzia Mkoa wa Manyara, Byabato amesema kuwa Serikali imetenga kiasi cha shilingi Bilioni 65.3 zitakazotumika kusambaza umeme katika vijiji vyote 163 vilivyosalia katika Mkoa huo.

Aidha, amebainisha kuwa Kampuni mbili za Wakandarasi ndizo zilizoshinda kutekeleza Mradi huo wa kusambaza umeme katika wilaya zote tano za Mkoa huo ambazo ni Kiteto, Mbulu, Babati, Simanjiro na Hanang.

Amezitaja Kampuni hizo kuwa ni Nakuroi ambayo itatekeleza mradi huo katika Wilaya ya Mbulu, Hanang na Babati na kuunganisha umeme katika vijiji 138 vya wilaya hiyo kwa gharama ya shilingi Bilioni 35.

Kampuni nyingine ni Giza itakayotekeleza Mradi katika Wilaya ya Kiteto na Simanjiro ambapo itaunganisha jumla ya vijiji 42 kwa wilaya hizo kwa gharama ya shilingi Bilioni 30.

Sambamba na hilo, Wakili Byabato amewataka wananchi hao kutandaza nyaya katika nyumba zao na kulipia gharama ya shilingi 27,000 tu pasipo kulipishwa gharama za nguzo, nyaya pamoja na mita.

Amewataka wananchi hao kutoa taarifa katika ofisi za Serikali za Mitaa, Kata, Wilaya, Mkoa pamoja na TANESCO, pale mtu yeyote atakapomtaka mwananchi kulipia miundombinu yoyote ya umeme ili aunganishiwe huduma hiyo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Amos Maganga amewataka wananchi hao kuwa walinzi wa miundombinu ya umeme katika maeneo yao pamoja na kutoa ushirikiano kwa wakandarasi wanaotekeleza mradi huo.

Vilevile Mhandisi Maganga amewahamasisha wananchi hao kuchangamkia fursa ya kufanya kazi zisizohitaji taaluma maalum, ili waweze kujiongezea kipato na kufurahia uwepo wa mradi huo katika maeneo yao.

Amewakumbusha wakandarasi waliopewa kazi ya kutekeleza mradi huo kuwa Serikali haitaongeza muda kwa mkandarasi yeyote atakayechelewa kukamilisha mradi huo kwa wakati na kwamba atakatwa asilimia kumi (10%) ya malipo yake.



Naibu wa Waziri Wakili Stephen Byabato,akizungumza wakazi wa Kijiji cha Mungahay, Kata ya Tumati, wakati akizindua mradi wa Usambazaji Umeme Vijijini Awamu ya Tatu, Mzunguko wa Pili katika Mkoa wa Manyara uliofanyika Wilayani ya Mbulu



Naibu wa Waziri Wakili Stephen Byabato,(katikati) na baadhi ya Wananchi wakifurahi baada ya kukata utepe wakati wa wakati akizindua mradi wa Usambazaji Umeme Vijijini Awamu ya Tatu, Mzunguko wa Pili katika Mkoa wa Manyara uliofanyika Wilayani ya Mbulu, katika Kijiji cha Mungahay, Kata ya Tumati



Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Amos Maganga akizungumza wakazi wa Kijiji cha Mungahay, Kata ya Tumati, wakati uzinduzi wa Mradi wa Usambazaji Umeme Vijijini Awamu ya Tatu, Mzunguko wa Pili katika Mkoa wa Manyara uliofanyika Wilayani ya Mbulu



Wanafunzi wa Shule ya Msingi, Munguhay na baadhi ya Wananchi wakifurahi wakati Wakamsikiliza Naibu waziri wa Nishati, Wakili Stephen Byabato (hayupo pichani) wakati akizindua mradi wa Usambazaji Umeme Vijijini Awamu ya Tatu, Mzunguko wa Pili katika Mkoa wa Manyara uliofanyika Wilayani ya Mbulu, katika Kijiji cha Mungahay, Kata ya Tumati,

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...