Na Mwandishi wetu, Simanjiro
AGIZO
 la Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alilolitoa Julai 7 Mji mdogo wa Mirerani
 Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, la shughuli zote za uuzaji na 
uongezaji thamani wa madini kufanyika Mirerani linaendelea kutekelezwa.
Mkuu
 wa Mkoa wa Manyara, Charles Makongoro Nyerere, ameyasema hayo wakati 
akizungumzia na waandishi wa habari juu ya muelekeo wa uanzishwaji wa 
soko la madini ya Tanzanite Mirerani Wilayani Simanjiro.
Makongoro
 amesema agizo la Waziri Mkuu Majaliwa la shughuli zote za ununuzi na 
uongezaji thamani wa madini ya Tanzanite, kufanyika Mirerani baada ya 
siku 90 linaendelea kutekelezwa ambapo wafanyabiashara 49 wamefungua 
ofisi Mirerani.
"Majengo 
mawili yameshatengwa kwa ajili ya uuzaji wa madini hayo na yameshaanza 
kutumiwa na wafanyabiashara 49 wa madini hayo," amesema Makongoro.
Amesema
 hatua zinazoendelea ni upimaji wa eneo la kanda maalum ya kiuchumi 
(Manyara Special Economic Zone) ili kuwagawia wafanyabiashara wa madini 
waweke miundombinu yao na maeneo ya makazi.
Amesema
 Serikali kwa upande wake inaendelea kuingiza miundombinu muhimu ya 
kuwezesha huduma za maji, umeme, barabara na nyingine kama 
itakavyohitajika.
Amesema
 pia kupitia eneo hilo lililotengwa limepangwa kuwa na huduma muhimu za 
kijamii zikiwemo hoteli, migahawa, kituo cha polisi na maegesho ya 
magari.
"Nitumie fursa 
hii kuipongeza Serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Rais Samia 
Suluhu Hassan la kuhamishia soko la madini eneo la Mirerani Wilayani 
Simanjiro," amesema Makongoro.
Ametoa
 rai kwa jamii kuhakikisha wanatumia fursa hiyo kujiongezea vipato 
binafsu na wale wafanyabiashara wa madini amewakumbusha kulipa kodi na 
maduhuli ya serikali kwa mujibu wa sheria za kodi zilizopo.
Hata
 hivyo, Mkuu wa wilaya ya Simanjiro Dkt Suleiman Hassan Serera amesema 
utekelezaji wa agizo hilo utasaidia kuinua uchumi wa mtu mmoja mmoja, 
vikundi, wilaya, mkoa na nchi kwa ujumla.
"Jambo
 hilo ni kubwa na muhimu hivyo wote tushirikiane kwa ajili ya 
kuhakikisha kuanzishwa Tanzanite City katika eneo la Manyara special  
economic zones  linakamilishwa ipasavyo na kwa wakati uliopangwa," 
amesema Dkt Serera.
Amesema
 wiki ijayo atakutana na wafanyabiashara hao 49 katika kuhakikisha 
shughuli zote za uuzaji madini hayo yanafanyika Mirerani kama 
ilivyoagizwa na Waziri Mkuu Majaliwa.
Amesema
 Serikali ya wilaya ipo tayari na wataendelea kusimamia kikamilifu ili 
watu waweze kuanza kunufaika  moja kwa moja na amewasihi watumie fursa 
hiyo vizuri  ili serikali waweze kwenda pamoja kwani kukamilika kwa hilo
 utasaidia  kuimarisha  uchumi.
Waziri
 Mkuu Majaliwa, Julai 7 mwaka huu, akiwa kwenye ziara yake mji mdogo wa 
Mirerani, aliagiza shughuli za uuzaji na uchakataji wa madini ya 
Tanzanite, ambayo duniani yanapatikana Mkoani Manyara, ufanyike mji 
mdogo wa Mirerani pekee.



Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...