Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt. Angeline Mabula, akizungumza juzi na watumishi wa idara za ardhi na wadau mbalimbali wa Mkoa wa Singida katika ziara yake ya siku moja ya kukagua utendaji kazi wa sekta ya ardhi. Kutoka kulia ni Mwakilishi wa Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Singida Mjini, Eva Jeremia na Kamishna wa Ardhi Msaidizi Mkoa wa Singida, Shamim Hozza.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt. Angeline Mabula, akimkabidhi hati za Viwanja Afisa wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) Mkoa wa Singida, Vicent Mboya.
Meneja wa NHC Mkoa wa Singida, Judith Mwalongo akisoma taarifa ya utekelezaji katika kikao hicho.

Muonekano wa Jengo la NHC Mkoa wa Singida.


Na Dotto Mwaibale, Singida.

NAIBU Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt. Angeline Mabula amelipongeza Shirika la Nyumba Tanzania (NHC) Mkoa wa Singida kwa kuwa na mikakati endelevu na yenye tija.

Mabula alitoa pongezi hizo mkoani hapa wakati akizungumza na watumishi wa idara za ardhi na wadau mbalimbali katika ziara yake ya siku moja ya kukagua utendaji kazi wa sekta ya ardhi kwenye kikao kilichofanyika Ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Singida juzi.

"Nimeisoma taarifa yenu nawapongeza sana kwa mikakati yenu yenye tija na kazi nzuri mnayoifanya" alisema Mabula.

Akitoa taarifa ya utekelezaji na jinsi walivyojipanga kuongeza mapato Meneja wa shirika hilo Mkoa wa Singida Judith Mwalongo alisema  mwaka huu wa fedha 2021/2022 wamepanga kubadilisha miundo ya baadhi ya majengo yaliyopo mjini ili waweze kupata wapangaji wengi zaidi kwenye maeneo hayo.

Alitaja mkakati mwingine kuwa ni kufuatilia kwa ukaribu makao makuu ya Shirika hilo ili waweze kupata fedha za kuweza kuendeleza na kuboresha nyumba ambazo zimekoma kuingiza kodi sababu ya uchakavu na hivyo kuhitaji ukarabati mkubwa.

Mwalongo alisema wanatarajia kufanya uhakiki wa vipimo kwa nyumba zote za Shirika hilo zilizopangishwa ili kubaini nyumba zenye tozo ndogo kulingana na matumizi ya wakati huu ya wapangaji na kuhakikisha wapangaji wote wanalipa kodi ya kila mwezi kwa wakati kwa kuwafuatilia kwa karibu ili kufanikisha malengo waliojiwkea ya kuwa na bakaasifuri (Nil balance).

Alitaja malengo yao mengine kuwa ni kuongeza wigo wa matangazo ya sehemu zilizo wazi kwenye vyombo vya habari vya ndani ya mkoa na nje ya mkoa pamoja na mitandao ya kijamii.

Aidha Mwalongo alisema wamelenga kulishawishi shirika hilo liweze kuendeleza viwanja vyao vilivyo wazi kwa kujenga nyumba za makazi jambo litakalosaidia kuongeza mapato kwenye shirika na wananchi kupata huduma za nyumba kwa urahisi zaidi.

Alisema wanatarajia kukarabati Jengo la Hotel ya Lake Hill na nyumba zingine za zamani ambazo zilijengwa kwa udongo na kuwa nyumba zote hizo ziko katikati ya mji na zikifanyiwa matengenezo zitaongeza pato ndani ya Shirika na vilevile kupendezesha mji.

Mwalongo aliongeza kuwa mkakati wao mwingine ni kutafuta zabuni za ujenzi wa nyumba au majengo mapya yanayopangwa kujengwa na kuendelezwa na taasisi mbalimbali mkoani hapa ili waweze kuongeza mapato ya Shirika kwa ujumla.

Alisema kwa mwaka wa Fedha 2020/2021 mkoa ulijiwekea lengo la kukusanya kodi kiasi cha Shilingi 587,338,398.74 a hadi wanafunga mwaka huo wa Fedha walifanikiwa kukusanya Shilingi 533,874,759.00 ambayo ni sawa na Asilimia 90.9 (90.9%).

Alisma kwa mwaka huu 2021/2022 wamejiwekea malengo ya kuweza kukusanya kodi kwa kiwango cha asilimia mia (yani kuwa na bakaasifuri). Pia wataendelea kufanya ufuatiliaji wa madeni ya zamani ili kuhakikisha madeni yote ya zamani yashirika yanalipwa. 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...