Na Gaspary Charles

JUMLA ya wakulima 2,001 kisiwani Pemba wamesajiliwa kunufaika na mradi wa Viungo, Mboga na Matunda katika kipindi cha mwaka wa kwanza wa utekelezaji wa mradi huo kati ya wakulima 2,175 ambao walilengwa kufikiwa na kusajiliwa katika kipindi hicho cha utekelezaji wa mradi.

 Hayo yamebainishwa na meneja uendeshaji mradi huo kanda ya Pemba, Sharif Maalim Hamad wakati akiwasilisha tathimini ya utekelezaji wa mradi huo katika mkutano na wataalam wa kilimo pamoja na wakulima viongozi uliolenga kujadili mafanikio na changamoto za utekelezaji wa mradi katika kipindi cha mwaka wa kwanza.

 Alitaja wanawake kuwa ndio walionufaika zaidi katika kipindi hicho ikilinganishwa na wanaume ambapo jumla ya wanawake 1,211 walisajiliwa kunufaika huku wanaume wakiwa ni 790.

 “Katika kipindi cha mwaka wa kwanza tumefanikiwa kusajili idadi kubwa ya wanawake ikilinganishwa na wanaume na hii ni kutokana na kwamba mradi umetoa kipaumbele sana kwa wanawake,” alisema.

 Alisema mafanikio hayo yalitokana na uanzishwaji wa shamba darasa, uendelezaji na ufuatiliaji wa shamba darasa jambo ambalo limewezesha kuwasogezea karibu wakulima taaluma ya uzalishaji bora wa mazao.

 Kwa upande wake meneja mkuu wa mradi huo Amina Ussi Khamis aliwataka maafisa kilimo kushirikiana pamoja kutatua changamoto zinazowakabili wakulima ikiwa ni pamoja na kutoa taaluma sahihi za uzalishaji ili kusaidia lengo la mradi liweze kufikiwa katika kipindi chote cha utekelezaji wa mradi huo.

 Alisema kutokana na mradi kuwekeza nguvu katika kuwasaidia wakulima kuongeza uzalishaji, kupanua wigo wa masoko na kukuza vipato vya wakulima ni lazima wakulima na wataalam wa kilimo kufanya kazi kwa pamoja ili kusaidia ufikiaji wa malengo hayo.

 “Mradi utaendelea kuwasaidia wakulima katika maeneo mbalimbali ikiwemo utoaji wa taaluma ya uzalishaji bora wa mazao na pembejeo lakini pia wakulima wanalo jukumu la kendelea kuchangia nguvu katika baadhi ya maeneo ili kurahisisha upatikanaji wa matokeo kwa haraka,” alisema meneja huyo.\

 Mapema wataalam wa kilimo wakichangia wakati wa mkutano huo walisema utekelezaji wa mradi kisiwani Pemba umesaidia kuongeza hamasa kwa wakulima kujikita katika kilimo hicho kutokana na taaluma ambayo inatolewa kupitia shamba darasa zilizoanzishwa kwenye shehia ambazo mradi unatekelezwa.

 Mbarouk Rashid Juma kutoka shehia ya Shengejuu Wilaya ya Wete, alisema kupitia shamba darasa hizo ambazo ziliwawezesha wakulima kupata taaluma ya kilimo cha kisasa wakulima wamepata fursa ya kujifunza mbinu mbalimbali za kuzalisha mazao jambo ambalo awali hawakuwa na uwezo huo.

 “Tunashuruku mpaka sasa mafanikio kidogo tumeanza kuyaona kwa wakulima kwani hizi shamba darasa ambazo zilianzishwa zimewawezesha wakulima wengi kupata elimu ya uzalishaji bora wa mazao,” alisema.

 Aliongeza kwamba “mafanikio  yote haya yametokana na sisi wataalam wa kilimo kuwapitia wakulima na bahati nzuri wakulima wengi waliamka vizuri na kuanza kujiingiza katika kilimo.”

 Kwa upande wake Dawa Bakar Hamad mmoja wa wakulima viongozi kutoka shehia ya Shumba Mjini Wilaya ya Micheweni, alitaja miongoni mwa taaluma ambayo imewavutia zaidi wakulima ni uanzishaji wa bustani ya nyumbani kutokana na umuhimu wake.

Alisema, “mafanikio ambayo yamepatikana zaidi katika kipindi kifupi ni wananchi wengi kuhitaji kufundishwa kuhusu kilimo cha bustani ya nyumbani kwani imewavutia sana kutokana na kwamba inasaidia kutatua uhaba wa mboga majumbani.”

 Nae Khamis Hamad ambaye pia ni miongoni mwa wakulima wazoefu alisema, “moja ya mafanikio ya mradi ni kwa mabwanashamba kutafta wakulima wazoefu katika kila eneo kushirikiana nao kutoa elimu ya uzalishaji bora, kwakweli katika hili mradi umefanikiwa sana na imesaidia kuwafikia wakulima wengi kwa pamoja.”

 Akizungumzia kuhusu changamoto zinazokabili utekelezaji wa mradi huo, Bakar Said bwana shamba kutoka shehia ya  Finya alisema ukosefu wa maji ndilo tatizo linalokwamisha uzalishaji bora wa wakulima kutokana na maeneo mengi ya wakulima hayana maji ya kutosha.

 “Wakulima wamepewa miche kwaajili ya kupanda lakini mpaka sasa tumeshindwa kupanda baadhi ya miche hasa matunda kutokana na kukosekana kwa pembejeo ya maji. Maji kwa kweli bado ni tatizo kubwa sana kwa wakulima katika mradi huu. Wakulima wanataka sana kulima lakini maji hamna. Kama hatujapata maji hatutaendelea mbele,” alisema.

 Mkutano huo wa kujadili na kutahmini changamoto na mafanikio yaliyojitokeza katika utekelezaji wa mradi huo kwa mwaka wa kwanza ni mwendelezo wa utekelezaji wa mradi wa Viungo, Mboga na Matunda wa miaka minne unaotekelezwa Zanzibar kupitia ufadhili wa Jumuiya ya Umoja wa Ulaya (EU) na kutekelezwa na People’s Development Forum, (PDF), Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, Zanzibar (TAMWA ZNZ) na Community Forests Pemba (CFP). 

 


Meneja mkuu wa mradi huo Amina Ussi Khamis akizungumza na washiriki wa mkutano huo.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...