Na. Projestus Binamungu,GCU- WHUSM
Waziri
wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Innocent Bashungwa leo,
Agosti 25, 2021 amekutana na viongozi wa Baraza la Michezo la Taifa,
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) na Mkurugenzi wa Michezo,
jijini Dar es Salam kujadili namna bora ya kutatua changamoto mbalimbali
katika mchezo wa soka nchini.
Kikao hicho ni sehemu ya
utekelezaji wa maagizo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.
Samia Suluhu Hassan aliyeagiza mamlaka zinazohusika na Michezo kufanya
maandalizi ya kutosha ili kuwawezesha wachezaji kuipeperusha vema
bendera ya Tanzania katika mashindano ya kimataifa.
Mhe.Bashungwa,
amefafanua kuwa kikao hicho pia ni hatua ya maandalizi kwa ajili ya
kuiwezesha timu ya Taifa ya Mpira wa miguu (Taifa Stars) kushiriki
mashindano ya kombe la dunia mwaka 2022 Qatar.
Amewaomba wadau
mbalimbali wa Michezo kujitokeza na kushirikiana na Serikali pamoja na
TFF ili kuiwezesha Taifa Stars kufuzu kucheza kombe la dunia.
Amesema
Serikali kupitia Wizara yake inafanya jitihada kuhakikisha inatunza
heshima ya Taifa iliyoletwa na timu ya mpira wa miguu ya vijana wa chini
ya umri wa miaka 23 ambao wamekuwa mabingwa wa Afrika Mashariki na Kati
(CECAFA) kwa mwaka 2021.
Timu ya Taifa ya Mpira wa Miguu (Taifa
Stars) inatarajia kusafiri nchini Kongo mapema mwezi Septemba kwa ajili
ya kushiriki Mchezo dhidi ya timu ya taifa ya nchi hiyo, zote zikiwania
kushiriki mashindano ya kombe la dunia.
Wakati huohuo timu ya
taifa ya wanawake (Twiga Stars) inatarajia kusafiri nchini Afrika Kusini
kwa ajili ya kushiriki mashindano ya COSAFA mwezi Septemba dhidi ya
timu ya wanawake ya nchi hiyo.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...