Akizungumza na waandishi wa
habari katika karakana ya Jangwani kabla ya Mabasi hayo kuingia barabarani,
Kaimu Mkurugenzi wa uendeshaji wa DART Mhandisi Dkt. Philemon Mzee alisema
hatua ya kuyaruhusu mabasi hayo kuanza kutoa huduma imefikiwa baada ya taratibu
zote za kisheria kukamilika ikiwemo kupatiwa leseni na Mamlaka ya Usimamizi wa
Usafiri Ardhini LARTA, pamoja na kujaribiwa ubora wake na vyombo mbalimbali vya
Serikali.
“Tumekuja hapa kuuambia umma wa
watanzania na wakazi wa Dar es Salaam kwa ujumla kwamba Serikali yao sikivu
chini ya uongozi wa Rais wetu Mh. Samia Suluhu Hassan imeruhusu kuanza kutumika
kwa Mabasi haya 70 yaendayo kwa Haraka ili kupunguza adha iliyokuwa inawakabili
kwa muda mrefu kutokana na uchache wa Mabasi” Alisema Dkt.Mzee.
Alisema Wakala wa Mabasi Yaendayo
Haraka unaendelea kumsimamia mtoa huduma ili afuate taratibu na kanuni zote za
kuendesha mradi huo wa Mabasi Yaendayo Haraka ili adhma ya Serikali ya
kuwapunguzia kero ya usafiri wakazi wa Dar es Salaam itimie.
Alisema kuanza kutumika kwa
Mabasi hayo mapya 70 kutaleta unafuu wa usafiri katika Jiji la Dar es Salaam
hasa katika kipindi hiki cha mlipuko wa ugonjwa wa Uviko 19, ambapo wasafiri
hawatakiwi kusongamana kwenye vyombo vya usafiri.
Awali Waziri Mkuu Kassim Majaliwa
aliagiza kuachiwa kwa Mabasi hayo ili kusaidia utaoaji wa huduma ambazo
zilizorota kutokana na uchache wa Mabasi katika mfumo wa Mabasi Yaendayo Haraka
Jijini Dar es Salaam.
Aidha Waziri Mkuu aliwahi
kuuagiza Wakala kuendelea kuboresha mradi huo kwani umekua kivutio kikubwa kwa
wageni kutoka nje ya nchi ambao wanakuja kujifunza, jambo ambalo linailetea
sifa Tanzania kwakua ni nchi ya kwanza katika Afrika Mashariki na Kati kuwa na
mradi mkubwa kama huo.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...